MALAIKA SEHEMU YA 1
“Malaika! Malaika mwanangu!”
“Naam mama... mbona unaniita kwa presha hivi, kuna nini tena?”
Mama mkwe aliingia ndani huku uso umemshuka kama amekula ndimu, yaani kuanzia asubuhi alikuwa na jambo lake limekaa kooni. Miaka mitatu sasa imepita tangu Malaika aolewe na mwanawe kule Mwanza, lakini nyumba imepoa kama jokofu. Hakuna hata kichefuchefu cha uongo, wala tumbo kuchomoza—hakuna kitu kabisa! Na kwa mama mkwe, hili jambo lilikuwa linamfanya apandishe mori.
“Malaika,” mama alianza kumpiga dongo, “hivi wewe kwenye hii nyumba ya mwanangu ni pambo la ndani au mke?”
“Hapana mama,” Malaika alijibu kwa upole huku akitetemeka, maana alishajua tu hapa ni mwendo wa mashambulizi. “Mbona unaniuliza hivyo?”
“Unaniuliza swali ambalo jibu unalo?” Mama akamtolea kibezi cha hali ya juu. “Inaonekana Baraka amekuoa ili uwe unapangusa vumbi kwenye makochi tu hapa Arusha. Maana miaka mitatu sasa, hata dalili ya mjukuu sioni!”
Malaika akashusha pumzi ndefu. “Mama, najua unatamani mjukuu, na mimi pia natamani sana—lakini kila kitu ni mpango wa Mungu.”
“Hebu nistue mwanangu, wewe siyo Hana wala Sara wa kwenye Biblia! Usijifananishe na watu wa kwenye vitabu,” mama alimfokea. “Miaka mitatu inatosha sana Mungu kutoa jibu. Jikague vizuri, labda unajua mwenyewe unachokifanya huko sirini ambacho kimeziba tumbo lako!”
“Mama, jamani... mbona husemi hivyo? Tulienda mpaka hospitali kubwa kule Dar, daktari akasema mimi sina tatizo lolote.”
“Sasa unataka kusema mwanangu ndio ana tatizo?”
“Hapana mama, sijasema hivyo...”
“Basi jiongeze unipe mjukuu! Nataka wa kiume, wa kike, mimi sijali. Nataka kitu cha kubeba mkononi, siyo makochi ya Arusha!”
Malaika alihisi machozi yakimlengalenga. Yaani kila mahali ikawa ni kusemwa tu. Hata kule sokoni, wanawake walikuwa wanamtazama kwa jicho la kando kana kwamba yeye ndiye kirusi cha familia. Siku moja mchana, alimsikia mwanamke mmoja akimnong’oneza mwenzake huku anajua kabisa Malaika anasikia:
“Tazama sisi huku tunahangaika kulisha watoto watano, na huyu mwingine hapa ananunua kilo za nyama na samaki wa bei mbaya lakini hana hata mtoto mmoja wa kula naye. Pesa imepotea kweli!”
Kauli hiyo ilimchoma kama pasi ya mkaa. Alirudi nyumbani akajifungia chumbani, akalia sana.
Malaika alikuwa anaishi kwenye jumba la kifahari, maisha ya kishua, lakini hakuwa na furaha. Alikuwa na kijana wa kazi, Sule, ambaye ndiye alikuwa anafanya kila kitu. Malaika alikuwa na wivu sana, hakutaka kabisa mume wake, Baraka, ahudumiwe na binti wa kazi. Aliamini mabinti wa kazi ni "vicheche", wanaweza kumteka mume wake. Ndio maana akaamua kuajiri kijana wa kiume, Sule, ili awe na amani.
Lakini baada ya miaka mitatu ya ukimya, mume wake Baraka naye akaanza kubadilika. Siku moja jioni, Baraka alirudi nyumbani akiwa amefura kama amemeza nyuki.
“Mpenzi, karibu nyumbani. Umetoka kazini?” Malaika alijisogeza kumbeba begi, akijaribu kumtuliza mume wake.
“Kwani nitakuwa nimetoka wapi kwingine zaidi ya kazini?” Baraka alimfokea kishari.
“Mbona unanifokea mpenzi? Kuna tatizo gani?”
“Tatizo ni wewe, Malaika! Wewe ndio tatizo!”
Malaika alistuka kama amepigwa shoti. “Nimefanya nini mume wangu?”
Baraka akazungusha mikono yake huku akitazama sebule yote. “Tazama huku! Unaona nini?”
“Sioni kitu... zaidi ya makochi na samani nzuri.”
“Na hilo ndio tatizo kubwa! Nina pesa, nina magari, nina kila kitu mwanaume anachotaka. Lakini nikirudi nyumbani nakutana na nini? Samani! Hakuna mtoto anayekuja kunikumbatia, hakuna kelele ya mtoto inayoniita ‘Daddy!’ Nataka ninunue peremende na biskuti nirudi nazo nyumbani nijihisi mwanaume. Nataka uhai kwenye hii nyumba!”
“Mpenzi, tunapambana...” Malaika alinong’ona kwa sauti ya chini.
“Sikiliza Malaika, nakupa mwezi mmoja tu! Usipopata mimba, ninaleta mke wa pili!”
Malaika alihisi kama dunia inampasulia. “Kwa hiyo unanilaumu mimi? Unadhani mimi ndio sipendi mtoto?”
“Nilipokuwa kijana kule Mwanza, nilimpa msichana mimba. Japo mtoto alizaliwa mfu, lakini hiyo ilithibitisha kuwa mimi ni mwanaume kamili! Sasa usinicheleweshe. Kama baada ya mwezi mmoja hali ni hii hii, naoa mke mwingine!”
Malaika alijihisi amesukumwa ukutani. Alimpenda sana Baraka, na wazo la kuletewa mke mwingine lilikuwa linamuumiza kuliko kifo. Aliamua kuendelea kujaribu, akisali muujiza utokee.
Lakini mwezi ukakata... hakuna kitu! Baraka akawa mkali kama mbogo. Usiku mmoja, alirudi nyumbani amechelewa, na Malaika akasikia harufu ya pafyum ya kike ambayo si yake.
“Mbona umerudi muda huu? Na hii harufu ya nini?” Malaika aliuliza kwa wasiwasi.
Baraka akamtazama kwa dharau akasema, “Ni pafyum ya mtu tu. Na ikigeuka kuwa mtoto kwenye tumbo la mwanamke mwingine, ndio utaelewa maana yake.”
Hapo sasa, nguvu zote za Malaika zikaisha. Akili ikamruka. Akahisi kama dunia haina usawa.
Alijua lazima afanye kitu... chochote kile... ili kuokoa ndoa yake. Alikuwa na shauku ya kujua, "Hivi kweli mimi ni tasa, au mume wangu ndio anajigamba bure?"
Pale Sule, yule kijana wa kazi, alipopita sebuleni na kumsalimia, “Shikamoo Aunty,” Malaika alimtazama Sule kwa jicho tofauti. Kijana alikuwa na nguvu, mtanashati, na mbichi.
Wazo moja la ajabu na la hatari likamjia kichwani. Wazo ambalo hakuwahi kuliwaza maishani mwake.
“Labda ninaweza kumtumia huyu kijana wa kazi ili nijipime... nione kama kweli tumbo langu ni tasa.”
ITAENDELEA...
Makala nyingine zinazocheza na ladha yako
Mapendekezo haya yanatokana na kile unachosoma sasa + Endelea kugundua zaidi
Maoni