NAKUPENDA BILA MIPAKA 1 - 12
:01
Natafuta ni wapi nianzie na ni wapi nimalizie, sijui kabisa yaani kwa maana moyo wangu, roho yangu, na hisia zangu vyote kwa pamoja vimejawa na furaha isiyo kifani.
Maisha yangu ni ushuhuda, maisha yangu ni Mungu, na nipo hapa kumtolea Mungu ushuhuda wa maisha yangu na yote mazuri mengi ameyafanya kwangu.
Mwanzo sikuwahi kuona njia, kila kitu niliona ni laana, ni mabalaa, ni matatizo. Sikuwahi kujua kuwa Mungu anazo njia nyingi sana za kufanya ufanikiwe.
Mimi ninaye kaka yangu, ninaye mama yangu na katika yote nilibahatika sijui niseme nilikosea nilizaa na ninaye mtoto wa kike hapa nyumbani.
Kitu ambacho mama yangu kinamuuma na kumuumiza hata aliniambia kwa upole “Nazwi binti yangu, kwani mama yako nimekosea wapi mwanangu. Nimekuhangaikia sana, ni Sawa umemaliza diploma yako, badala tuhangaike uje nisaidia mama yako na wewe tena unaleta mtoto. Kaka yako una muona kichwa chake, ni pombe, bangi, uhuni tu na wewe ndiyo tegemeo langu. Sasa mwanangu nini tena umefanya.”
Mimi nipo hapo sasa sina hata la kufanya, najisikia aibu, maumivu nalia tu huku nikisema “mama yangu nakuomba nisamehe, mama nisamehe sana mama yangu.”
Mama anatokwa machozi hata najisikia kupasuka maana hayo yamenikuta kwa mwanaume ambaye nimezaa naye nayo ni majanga basi naona moyo wangu unapasuka kwa maumivu na kujiona mjinga mama yangu vile analia naumia sana kusema kweli.
Mama alinitazama na kusema kwa upole na maumivu “umenivua nguo mwanangu, wewe peke ndiyo nilikuwa nakutegemea haya sasa mwanangu, tutafanyaje maisha ndiyo Kama unavyoona hapa nyumbani mimi mama yako sina lolote na sasa maradhi yananisumbua eenh si unaona umri.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:02
Nilitokwa na machozi nikisema kwa upole “najua nimekuumiza mama yangu, najua mimi ni nguo ya hii familia. Naomba mama yangu, nakuomba fungua moyo wako kwaajili yangu, nakuomba fungua moyo na unisamehe mama.”
Mama alinitazama na kusema “unafikiri nitakutupa binti yangu?, Hapana mimi siwezi kufanya hivyo. Wewe ni mwanangu mimi, wewe ni binti yangu mimi, siwezi kukutupa kabisa. Hapa ni nyumbani na mtoto ni baraka. Lakini unatakiwa uchangamke sasa, sijui ufanye nini ila huwezi nitegemea mimi tu lazima tusaidiane.”
Nilivuta kamasi zangu na kusema kwa upole “Asante sana mama, nashukuru sana mama. Nitapambana kwaajili yetu sisi wote. Nisamehe mama. Sikuwa na lengo La kukuumiza.”
Mama alinitazama na kusema “Futa machozi binti yangu, Futa machozi. Usikubali kulia kila siku, wewe sasa ni mama, kumbuka mama sio mzembe, mama hachoki, mama haumwi, mama Hana machaguo kwasababu kuna mtoto anakutegemea. Pambana binti yangu na unatakiwa kuwa mvumilivu.”
Nilitabasamu na kuinuka, Nilienda chumbani kwangu na kumtazama mwanangu pale kwa godoro. Nilijikuta natabasamu, halafu nikakumbuka ghafla kuhusu mwanaume ambaye nimezaa naye machozi yalinimwagika. Roho yangu ni Kama ilitaka kutoka kwa Yale nimepitia. Yale matukio na maisha yangu na yeye.
Nilikaa, nilikuwa sielewi nifanye nini, kazi adimu, mimi nimesomea uuguzi nafanya kazi najitolea hospitali mbalimbali lakini hakuna malipo.Unafanya hapa na pale unaacha maana Hakuna kitu cha maana una pata zaidi ya mateso tu.
Sasa hapa ndiyo maisha yalianza, nilianza maisha na mama yangu, kaka yangu na mtoto wangu ingawa hayakuwa rahisi lakini tulipambana, tulibebana na kusaidiana huku ugomvi wa mama na ndugu yangu Mara kwa Mara juu ya tabia zake unajua tena watoto wa kiume unasikia anasema “tatizo lako bi mkubwa unapenda tu kufoka mimi nishakuwa mtu mzima sasa, eenh sasa michongo gani unaniletea.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:03
Mama na yeye anasema “Kama mtu mzima si ukapange kwako hapa kwangu unatafuta nini eenh unatafuta nini Muone alivyo.”
Mimi tena nasema “hivi wewe Baraka ni maneno gani unamwambia mama lakini eenh, lugha gani unatumia.”
Mama utasikia anasema “Nazwi mwanangu muache, wewe muache yeye si amekua na mimi ananiona mdoli wake wa kuchezea wewe Muache tu”
Baraka anakasirika hapo anaondoka, mama ana baki ana ugulia tu na Mimi tena ndiyo nasema “mama Acha kujiumiza wewe Baraka unamjua alivyo mzoee tu.”
Mama analia akisema “uzazi unauma. Wewe ni mama sasa siku utaelewa tu.”
Haya ndiyo yalikuwa maisha yetu lakini katika yote sisi wote tulikuwa tunapendana sana. Tulikuwa tunapenda, mama yangu alikuwa msaada mkubwa sana kwangu kuanzia malezi ya mwanangu na vingi sana mpaka mwanangu alifikisha miaka miwili hivi sasa anazidi kukua.
Mama yangu anaye rafiki yake, huyo rafiki yake ana watoto na Kati ya wanaye watatu Ana binti ambaye naye kwangu kawa rafiki. Huyu tunazungumza mengi sana. Anaitwa Dorice. Siku moja alikuja nyumbani akiwa na furaha sana.
Moja kwa moja alikuja chumbani kwangu akiita kwa fujo “Nazwiiii!!, wewe Nazwiii Upo wapi?”
Nilijisemea ndani ya moyo wangu “kumekucha sasa kumekucha, Dee kelele jamani kuna nini?”
Alifika chumbani, na wakati huo mwanangu naye anakuja na kilio, nikamuuliza “eenh mwanangu nini shida?”
Basi anaongea vitu hata sielewi, ila nikamwambia “nitamchapa huyo, haya nenda kwa bibi mimi nizungumze na aunt Dee.”
Dee alitabasamu na kusema “huyo naye kwa kudeka sasa.”
Tukacheka, vile tumemaliza tu kucheka simu yake iliita alinitazama akisema “shemeji yako naye hapumziki!!.”
Nikabinua tu midomo, yeye akapokea pale anadeka mwenyewe huku akisema “dakika 20 tu baby, nipo kwa Nazwi Nina jambo muhimu naongea naye please!!”
Baada ya muda akakata simu, mimi nikasema “kudeka sasa.”
Akacheka akisema “hivi na wewe Ina maana kuwa na mpenzi Tena hutaki kısa baba Priya.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:04
Nilitabasamu tu, Kisha aliniambia “shauri yako, unajiumiza bureeeee haya Ngoja nikuambie kilichonileta.”
Nilitabasamu na kusema “Hilo sasa ndiyo la maana.”
Alitabasamu na kusema “nisamehe rafiki yangu kama nitakuwa nimeingilia maisha yako, lakini unajua nakuhurumia ndiyo maana nimeona tu hii itakufaa hata kwa muda na nimeona wanalipa vizuri sana.”
Nilimtazama na kusema “niambie haraka, ni kazi si ndiyo?”
Alinitazama na kusema “ni kazi, tena ni kazi yenye malipo nzuri na inahusu ulichokisoma.”
Nilitabasamu na kusema “hospitali gani hiyo, Dee sitaki kujitolea tena tafadhali. “
Akacheka kidogo na kusema “Jamani rafiki yangu sio kujitolea. Si unajua kule nafanya kazi eneh, sasa Boss wangu alikuwa ana Omba tumsaidie kutafuta nesi yoyote mzuri ambaye ana upendo anaweza kukaa na mgonjwa huko kwa matajiri si unajua.”
Nilimtazama, akanitazama kwa woga akasema “nilisema nina ndugu yangu anaweza kufanya. Rafiki yangu mshahara mzuri, fikiria kwa siku unaondoka 30k unakula hapo, jioni unarudi zako mimi mwenyewe nilitamani niwe nesi.”
Nilimtazama na kusema “30k kıla sıku, hutanii si ndiyo?”
Alinitazama akisema “Boss wangu unamuonaje kwanza ile süpermarket yake?, unafikiri atakuwa na marafiki wa ajabu ajabu watu wanaishi huko Mikocheni sijui ndiyo Masaki mimi sijui mambo ya watoto wa kishua shoga yangu.
Mimi mwenyewe mshahara laki tano fikiria wewe 30 kwa siku Mara mwezi si laki 9 hiyo eenh bado chenji chenji. Ndugu yangu usikatae hiyo nafasi nakutamani ujue.”
Nikamtazama nikitabasamu na kusema “kwa maisha yalivyo nichapa, mama yangu mpaka pesa ya pedi namuomba rafiki yangu naomba tu niambie ikawaje.”
Akanitazama na kusema “si unajua Boss anavyoniona mchapakazi. Akafurahi balaa akasema nimpe namba yako ili ampe huyo rafiki yake. Nikaona siwezi kutoa sasa mpaka nije kuongea na wewe.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:05
Nilimtazama na kumuuliza “una akili nzuri?, toa namba wewe, mpe namba yangu nipo tayari kuanza kazi hata leo hii, nipo tayari.”
Tukacheka nikisema “chezea elfu 30 kwa siku wewe. Mungu wangu nipo tayari.”
Tulicheka sana na rafiki yangu aliniambia “sina mazoea ya kuwasiliana na boss maana alivyo mkali Mungu wangu. Shoga yangu habari ndiyo hiyo, kukuche kesho kazini nitampa Kisha tusubiri muujiza.”
Nilifumba macho yangu nikisema “eenh Mungu wangu, wasipate mtu mwingine ni nafasi yangu ya kulea familia yangu.”
Dorice alinitazama na kutabasamu, Nilitabasamu nikisema “Kipenzi Asante kwa kunifikiria kwenye fursa nakupenda si unajua.”
Alitabasamu akisema “rafiki mzuri ni Yule anayeweza kutaja jina lako kwa mazuri sehemu yoyote ile. Nakupenda rafiki yangu najua ukipata wewe ipo siku utanifaa uongo rafiki yangu?”
Tulikumbatiana tukicheka, hata mama alitukuta tunacheka akisema “Binti zangu mkishaanza umbea sasa eenh nisimulieni.”
Dorice alisema akitabasamu “mama tulia kwasasa tuombee heri jambo likifanikiwa tu umbea naumwaga.”
Tuliendelea kucheka sana. Na mwisho aliondoka zake na mama pale chumbani niliwasikia wakicheka huku Dee ana aga na mimi nilibaki chumbani.
Kutoka moyoni hii habari ilikuwa kubwa sana kwangu. Hivi kweli mimi nimehangaika na maisha siku zote hizo halafu tu kwenda kwa mgonjwa iwe kazi na kitu nimesomea. Kiukweli sijui huyo mgonjwa anaumwa nini, ana hali gani ila hapo kwenye malipo na ni kazi yangu eenh jamani nilishindwa jizuia.
Nilitabasamu nikisema “Eenh Mungu bariki na hili, nisaidie nipate.”
Ndani yangu, nilitamani sana hii nafasi iwe nafasi yangu. Natamani sana .Hapa nilipo natamani kesho ifike halafu kesho hiyohiyo nipigiwe simu, natamani sana. Lakini yote kwa yote inabidi niwe mvumilivu sana.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:06
Usiku huu wakati namlisha mwanangu nilipata muda wa kuzungumza na mama juu ya hili.
Mama alitabasamu na kufurahia akisema “eenh mwanangu ukipata sasa ndiyo walau tutapata nafuu na sisi ya maisha.
Mungu atukumbuke jamani, Mungu atuone 30k kubwa sana lakini mwanangu pengine Labda kazi ngumu sana huwezi jua mgonjwa ana hali gani.”
Nilitabasamu na kusema “mama uuguzi nimesomea, upendo ndiyo kıla kitu. Nipo tayari kuishi na mgonjwa yeyote Yule ili mradi tu daktari atanipa maelekezo ya muhimu kuhusu mgonjwa wake. Ila siwezi kushindwa nakuahidi.”
Mama alitabasamu akisema “nakujua mwanangu, una moyo mzuri sana. Tumuachie Mungu tu, lakini nina amini kabisa tunafanikiwa kwenye hili.”
Nilitabasamu nikisema “nitafurahi sana mama.Nitafurahi.”
Nilikuwa natabasamu tu, nilikuwa naona Kama kesho haifiki Dee aniambie nini kinaendelea.
Nikiwa kitandani najigeuza huku na kule huku ndani ya moyo wangu nikisema “Mungu wangu nikumbuke Mimi, nisaidie niweze kumlea mtoto wangu. Nisaidie mwanangu asiishi maisha ambayo Mimi nimeyaishi.Mungu nisaidie.”
Hapo mwanangu amelala Hana hili wala lile mama yake ninavyohangaika.
Nililala nakuambia asubuhi na mapema nimeamka, natamani nimpigie Dee Ila moyoni najiambia “Nazwi na wewe mbona mapema sana kuwa na subira.”
Basi pale nikaanza kujifanyisha kazi za hapa na pale, mama yangu na yeye akawa anahangaika na mambo yake ya kuchoma maandazi unajua Tena Mimi nipo hapo naangalia simu. Mama kuna muda alinitazama na kusema “wewe Tena hiyo simu nini shida?”
Nilitabasamu nikisema “hakuna mama, Hakuna.”
Mama alisema “emu Njoo tusaidiane kwanza kazi.”
Nilitabasamu tu.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:07
Mpaka saa 6 mchana uvumilivu ulinishinda nikiwa zangu nachambua mboga za majani. Nilimtumia ujumbe Dee niliandika “Shoo, vipi mbona kimya Ina maana bado tu?”
Hakuchekelewa kujibu kwanza alianza kwa kucheka na kusema “si utulie na wewe, muda sio mrefu atafika nitazungumza naye.”
Nilimjibu kwa upole “naona siku imeganda mwenzako, maisha magumu haya.”
Hakujibu, namuelewa Kazi yake ni ngumu kusimama siku nzima sio mchezo.
Niliendelea na kazi zangu huku nikijiambia jikaze mwaya ukuhitajika utaitwa. Basi nikawa naendelea na mambo yangu, tumemaliza kula sasa vile naondoa vyombo ndiyo ujumbe ukaingia kwa simu yangu, haraka nilifungua alikuwa ni Dee ananiambia “Nimempa Boss namba yako. Amesema atampa huyo rafiki yake na utapigiwa. Ila anasisitiza unatakiwa uwe makini na ujitambue sana maana huyo Boss sio mtu wa masihara kazini.”
Ninatabasamu tu vile nasoma, maana naona sijui anaongea nini maana suala la utulivu, umakini Mimi hivi nilivyoteseka kupata kazi eti jamani nichezee fursa aku haiwezekani, haraka nilimjibu “Mungu akubariki sana Dee, wewe ni dada yangu mzuri. Nakupenda mwenzio.”
Hapohapo akajibu “kione kama nakuona, haya baadaye ndiyo utulie na uwe karibu na simu yako sasa.”
Nilitabasamu tu.
Basi kuanzia ile siku naangalia tu simu, ikawa siku ya kwanza ikapita, ya pili simu ikiita haraka napokea Kumbe hata sio wao nachukia, nikikaa macho kwa simu, kila ninachofanya macho kwa simu yangu. Ilikuwa siku ya tatu usiku, nimekaa na mama yangu.
Alinitazama na kusema “Mwanangu, kila muda macho kwa simu, unaweza sahau Hilo pengine hawahitaji tena.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:08
Nilimtazama mama na kusema kwa upole “Labda mama, nilikuwa nategemea sana, nilifurahi sana kupata nafasi hii. Ila ndiyo hivyo nianze tu kutafuta sehemu zingine.”
Mama alinitazama akisema “uzuri ni kuwa binti yangu roho ya kukata tamaa huna kabisa. Nenda kalale, achana na hili suala Baada ya muda binti yangu kila kitu kitakuwa sawa na utafurahia.”
Nilitabasamu tu ingawa ndani kabisa ya moyo wangu najisikia kuumia kwa kukosa nafasi hii nzuri, nafasi ambayo nilikuwa nina amini kabisa itabadilisha maisha yangu kwa namna moja au nyingine.
Nilienda kulala sasa nikiwa nishachoka kuhusu kusubiri simu sasa nawaza mambo mengine. Nakumbuka vile usingizi ulikuwa mgumu sana kwangu siku hii.Nilikuwa tu nahangaika huku nahangaika kule si unajua ukiwa na mawazo usingizi nao unakuwa unasumbua. Nilichoka sana kusema ukweli Ila nitafanya nini inabidi nijikaze.
Nakumbuka, asubuhi sana, saa moja hivi hata sikuwa nimeamka. Simu yangu ilikuwa inaita, nilishtuka usingizi kutazama ni namba mpya. Nilijisemesha mwenyewe “eenh, Nani tena asubuhi yote hii wakiwa matepeli Leo tunagombana.”
Nilipokea kwa upole “hello.”
Nikasikia upande wa pili sauti ya mwanamke “Naitwa Dokta Kabale, unaweza kufika Mikocheni muda huu, bila Shaka ulishaambiwa kuhusu kazi.”
Unajua usingizi ulikata, pale pale nilijikuta nimepata uchangamfu, sina hata mia Ila nilisema “naweza, naweza, Nipe maelekezo tafadhali.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:09
Dokta Kabale alisema “changamka tafadhali, nipo hapa nakusubiri nikupe maelekezo.Maelekezo kuhusu unafikaje nakutumia.”
Alikata simu. Nilitazama ile simu, nilijikuta nacheka. Nilifurahi hata nikaanza kuita “mamaa!!, mamaaa!!, mama upo wapi?”
Vile natoka sasa nakutana na kaka yangu, alivyo niona na furaha akaniambia “vipi tena shangwe asubuhi asubuhi utamuamsha ankali.”
Vile anaongea Mimi naona tu ananipigia kelele.
Vile nimefika nje mama anahangaika na jiko lake kuniona alishangaa akisema “nini tena asubuhi yote hii.”
Nilitabasamu na kumkumbatia mama yangu nikisema “mama, nina furaha sana, nimepigiwa simu natakiwa kwenda.”
Mama alifurahia akiuliza “unasema kweli?”
Nilitabasamu, nilimtazama mama na kusema “Naomba nauli mama.”
Mama alisema “kajiandae sasa, eenh na usiache kumwambia dada yako Dee umeitwa sijui unanielewa.”
Nilitabasamu, nikarudi ndani na furaha huku namsikia kaka akimuuliza mama na mama anajibu “utamuweza dada yako kapata kazi huyooo.”
Baraka sasa anafurahia tu, mbali na mapungufu yake familia yetu Ina upendo sana. Basi nilipofika ndani nilimpigia rafiki yangu hakupokea, nikamuachia ujumbe Kisha nilianza kujiandaa.
Nilianza kujiandaa na ujumbe wa huyo dokta Kabale uliingia ukiwa na maelekezo na ukionesha kukazia nisisahau kubeba vitu muhimu kuthibitisha Mimi ni muuguzi kweli na vitu Kama hivyo. Nilitabasamu tu nikisema ndani ya moyo wangu “mbona nitabeba mpaka sare zangu.”
Basi nilivaa, nilivaa vizuri, nikapendeza sana. Nilivaa kiheshima sana. Mimi napenda kuvaa hivyo, Muonekano wangu ni wa msichana mwenye heshima. Basi na ule uzuri wangu kiasi chake basi ukiniona unasema Mungu ameumba. Zaidi ya yote Mimi ni msichana mpole sana, mwenye heshima, na mnyenyekevu sana.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:10
Nilitoka mama alinitazama Nikatabasamu. Akasema “umependeza sana binti yangu.”
Nilitabasamu na kusema “nashukuru sana mama. Priya amelala bado usisahau.”
Mama alitabasamu na kusema “Priya yupo salama Mimi bibi yake nipo.”
Nilitabasamu na kusema “husemi lolote mama.”
Mama alitabasamu akisema “Nakutakia kila zuri binti yangu, tukafanikiwe kwenye hili, Mungu akusimamie.”
Nilitabasamu na kusema “kwaheri mama.”
Mama alitabasamu tu. Nami nilianza kufuata njia ya kuelekea mahali nitapata usafiri.
Nilifuata maelekezo na nikafika mahali nikachukua pikipiki kwa kufuata maelekezo na mwisho nilifika mpaka kwenye hiyo nyumba. Kwanza huku mtaani kupo kimya Hakuna hata watu wanatembeatembea.
Hapo Mimi natamani hata nishuke nipige picha huyu mkaka wa pikipiki ananiambia “yaani sister huku hata picha hutakiwi Ukianza tu kupiga wana kamera zao wanaona unakuta unafuatwa unakatazwa.”
Mimi nashangaa tu, watu wana ishi maisha bwana, achana na sisi kuna watu maisha Yao sio mchezo. Pesa sio shida zao sema lingine.
Nilipofika hapo nikawa nagonga geti na huu ushamba wangu, hapo namwambia boda “usiondoke Subiri kwanza kama nimekosea Je?”
Başı yule kaka ananiambia “usigonge geti bonyeza hapo kengele.”
Miye Tena kubonyeza kengele, simu yangu iliita, alikuwa Dokta Kabale.Aliniambia “nimeshakuona, utafuatwa sio muda.”
Eenh mimi tena nashangaa Ina maana na ujinga nafanya hapa getini naonekana ndani. Watajijua wenyewe kıla mtu mshamba kwa namna yake. Başı nakuambia mlinzi akafungua, akaniambia “Karibu sana.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:11
Nilitabasamu na Kisha nikamwambia boda tu aende. Mimi nikaingia. Nilipofika ndani nikapewa daftari La kuangusha taarifa zangu. Eenh nikaona hii kiboko sisi huko tunavyojua tembeleana bula hata kuandikishana hapa kıla mgeni unaandikishwa.
Mara alitoka mama mdada mkubwa kwangu hata kwa Dee mkubwa. Alinisalimia na kuita jina langu “Nazwi eenh.”
Nilitabasamu, akanitazama na kuniambia “karibu sana. Mimi naitwa dada Maria.”
Nilitabasamu, namna amevaa anaonekana na yeye ni mfanyakazi hapa, amevaa kijikoni jikoni na amependeza kwa namna yake. Sasa nikisema nielezee hii nyumba nitakuchosha tu, kama huko nje, huko mtaani ndiyo kupo vile vipi kuhusu hii nyumba.
Ni tajiri tena tajiri haswa.Nyumba Ina vitu vya thamani hatari. Mimi kıla nikisema nijikaze nisishangae nashtuka tayari nishashangaa, ningekaa kwa mama Nazwi huko ningeona wapi haya. Sasa hii ndiyo Dar ile tunaonaga kwa Tv sio hii niliyokuwa naishi mimi. Ni pazuri sana.
Nakuambia sasa tumefika ndani, Mungu wangu!!!, Mungu wanguuu!!, Mungu wangu!!, nyumba hii ni nzuri. Kuna picha na mapambo mengine mazuri sana. Halafu kuna picha ukutani kubwa ya kioo nzuriii sana.
Huyu mwanaume pale ukutani ni miaka 45 mpaka 50 hivi kwa nilivyo muona mimi lakini ni very smart, Kama kijana mdogo vile, halafu anaonekana kuwa serious sana. Halafu tena kuna picha ya mama mtu mzima, pengine ndiyo huyo mama labda mimi sijui.
Najiuliza maswali najijibu. Ndugu yangu ndani ni kusafiiiiii, wanafanyaje usafi mimi na wewe hatujui Ila sioni hata pakutoa kasoro, mimi naona maajabu tu, najionea raha tu. Sema tu vile napenda usafi başı nasikia amani mpaka ndani ya moyo wangu.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:12
Huyu dada Maria aliniambia “Karibu uketi.”
Mimi natabasamu vile nakaa sasa kiti inanesanesa balaa. Kuna sehemu ukikaa tu unapata amani. Hapa ni pazuri sana sijawahi hata kuwaza nitatembelea sehemu ya hivi.
Niliulizwa kinywaji aibu tena mimi nikasema nipo vizuri, zikapita kama dakika 20 hivi nimekaa nasubiri tu. Ndiyo Mara namuona huyo dada mzuri akiwa amevalia koti lake la udaktari kapendeza. Mzuriiiiii, hiyo rangi yake kwanza ama Hakika ni mrembo mwenyewe nikawa natabasamu tu.
Aliponifikia alinitazama akitabasamu kidogo “Nazwi, nifuate tafadhali.”
Unajua sijapata hata nafasi ya kusalimia, nifanye nini sasa, niliinuka na kuanza kumfuata. Nilimfuata mpaka kwenye hiko chumba ambacho ni kama ofisi ya nyumbani, nilikutana na huyo mwanaume sasa ameinama anapitia vitu vyake kwa karatasi.
Nilisimama, nilivyo sasa nikasalimia “shikamoni.”
Dokta Kabale aliitikia na Kisha huyu mwanaume sasa ndiyo aliinua uso wake. Nikuambie tu picha ya sebuleni ilimkosea, ilimkosea sana, ni mwanaume mzuriiii, mwanaume mzuri sana Ila ni mkubwa kwangu, anavutia, ana mwili fulani hivi, nashindwa kuelezea ni mwanaume mzuri mno na vile Ana rangi fulani hivi, hapo sasa namtazama lakini yeye uso wake hacheki na yeyote.
Alikuwa ananitazama tu, na Kisha Mimi niliinamisha kichwa changu nikisema “Mungu wangu nini hiki, mbona anaonekana ni mkali sana. Anavutia lakini mhhh, wacha tuone itakuaje.”
Nikasikia sauti yake, hiyo sauti sasa, sauti nzito, sauti ya mamlaka, sauti ya kishindo, sauti nzito na nzuri kuanzia anavyotamka maneno yake akisema “
Ndiyo kwanza tunaanza mliosoma Dating My boss kitabu msipitwe 😂😂🙌🙌
Makala nyingine zinazocheza na ladha yako
Mapendekezo haya yanatokana na kile unachosoma sasa + Endelea kugundua zaidi

Maoni