DO YOU LOVE ME 06 (S2)
SAD MOMENT
Niliingia mtaani kumtafuta Mama Rely kwa zaidi ya masaa 12 lakini sikuweza kumpata. Nilirudi nyumbani majira ya saa nne usiku nikiwa hoi bin taabani. Nikapoteza nguvu na akili ikafubaha sababu yule aliyesababisha hadi mwanamke huyu kupotea ni sehemu ya maisha yangu (Mama) kwahiyo mimi ndio nilipaswa kuwajibika mwanzo mwisho.
"Enh! Umemuona mume wangu?" Aliniuliza Rely kwa sauti ya upole iliyojaa kitetemeshi.
"Sijafanikiwa lakini kesho nitaenda tena"
"Hakuna ambaye alikuambia kuwa amepatikana?"
"Hakuna ila usijali" Nilimpatia moyo.
Asubuhi ilipopambazuka, sikuwa na muda wa kupiteza kabisa. Jambo la kwanza lilikuwa ni kwenda katika masoko kumtafuta. Ebwana nilikanyaga kila eneo ila sikumuona. Wasiwasi ukazidi kunipanda huenda atakuwa amekufa ama la! Kufika saa 12 ya jioni nilirudi nyumbani nikiwa nimechoka kama kawaida.
Rely alikuja na kudondisha machozi huku akidai kwamba huenda mimi na Mama yangu tulikuwa tumecheza mchezo wa kumpoteza Mama yake kwa makusudi.
"Kama mmeona hakuwa na haki ya kuishi hapa kwenu, kwanini msingenipatia Mama yangu nikaenda kuhangaika naye mwenyewe huko nje? Upo wapi upendo wa mwanamke huyu aliuonesha kwangu na kwenu pia wakati nakuhitaji? Inamaana Mama yako ameshindwa kuyakumbuka yale yote mema ya Mama?"
"Mke wangu, katika hili nakuomba uniachie mimi. Nakuahidi kwamba nitahakikisha namtafuta. Tafadhari usiongee maneno yenye kuniumiza ndani ya moyo wangu. Binafsi sipendi hili ambalo linaendelea, sitapenda kuona unakosa amani kila siku ndani ya nyumba hii. Nipe muda na amini kwamba nitamrudisha mama katika mikono yako" Nilimuahidi.
"Mama yako anaonesha chuki waziwazi kwa Mama yangu au mpaka afe ndio aje msibani kwa majonzi? Kwanini hampendi ikiwa hamkosea lolote lile? Ameshindwa kuniambia Rely kuna hili na lile Mama yako analifanya humu ndani na usafi wake utashughulika wewe hadi aende akamtupe kweli?"
"Baby, nimesema hili lipo chini yangu. Mimi nitahangaika na kuhakikisha kwamba tunampata Rely popote pale katika hii nchi. Kwanini unashindwa kunielewa?"
"Rahim, Mama yangu anateseka. Mama yangu ananyanyasika huko nje. Siku ya pili leo hayupo nyumbani, tunajua anakunywa nini? Anakula nini tunajua? Mama ni muhimu kwangu hata kama nyie wengine mnamuona hana thamani"
"Please, naomba unipe nafasi kesho nitaingia kumtafuta Baby" Nilimsisitiza na kumsihi huku nikimuomba.
Moja ya sifa nzuri ambayo Rely alikuwa nayo ni kwamba, alikuwa ni mpole na mwelewa sana hasa ninapomweleza jambo. Katika hili licha ya kudondosha machozi lakini aliniamini na kunisisitiza kwamba niongeze bidii na kama ikishindikana kabisa basi nikatoe taarifa polisi kwa uchunguzi kamili.
Lilikuwa ni wazo nzuri lakini kwa upande wangu niliona ama kuhisi kwamba lingeenda kumuangamiza Mama sababu polisi wangetaka kujua mazingira ya upoteaji wa Mama Rely na hapo ndipo ningemkamatisha Mama yangu. Basi, nikajipa ukimya na kuendelea kumtafuta taratibu.
Siku iliyofuata tulifunga safari na Rely hadi Kongowe ambako kuna mtu nilienda kuonana na mshikaji wangu (Jael). Tukawa tunaongea mipango ya hapa na pale sababu nilikuwa natafuta chumba cha kuishi huko. Tukiwa katika mazungumzo, nilimuona mtu kama Mama Rely akiwa anakatiza barabarani.
Nikamtazama kwa umakini wa hali ya juu mno, macho yangu yaliniambia kuwa yule ni yeye. Nilipomuuliza Rely, alithibitisha kwamba yule hakuwa mwingine bali ni Mama yake. Haraka sana nilienda kumfuata na kumshika mkono. Tukavuka barabara lakini wakati tunavuka, mwenzangu alinitingisha mkono akitaka atoke. Akatoka kweli.
Akili yake ilimtuma kurudi kule ambako alikuwa ametoka. Masikini! Mama Rely kama angejua wala asingethubutu kung'ang'ana kurudi kule tulikotoka. Kwani ilichukua sekunde 30 za yeye kusimama wima na sekunde zilizobakia zilimtupa katika mtalo.
Aligongwa na gari aina ya Mark II ambayo ilikuwa katika kasi ya ajabu kisha huyo dereva aliondoka zake. Watu wote tukaenda kumtazama Mama Rely kama yu mzima ama la! Kwa wakati ule alikuwa na afya ingawaje sio nzuri lakini haikutisha sana.
Tukajiambia tumpeleke hospital ambako angepatiwa matibabu, kumbe siku hii ndio tulikuwa tunampeleka katika shimo la umauti. Mama Rely alipoteza maisha dakika 40 mara baada ya kufika hospital.
Kwa mujibu wa Daktari alisema kwamba 'Damu ilichanganika sana katika eneo la kichwa jambo ambalo lilifanya ashindwe kuhema vizuri. Kitendo hichi kilipeleka Mama Rely kupoteza maisha'
Wakati mgumu na usiosimulika ukamgeukia Rely pamoja na Mimi pia. Wakati wa vilio na simanzi ulikuwa ni huu hapa. Wanasema Mama ni Mama hata kama awe chizi bado atabakia kuwa Mama. Siku hii Rely aliitambua thamani ya Mama yake kwani alilia kuliko kawaida.
"Yote haya kayataka Mama yako, kayataka. Si angeniachia tu mama yangu pale nyumbani kwenu kwani ningeharibika nini? Tazama sina Mama wala baba tena katika huu ulimwengu. Lipi Mama yako tumemkosea katika maisha yake? Kwanini ananipa adhabu nzito hivi? Kuna raha gani ya mimi kuendelea kuishi ikiwa sina ndugu hapa duniani? Si nitanyanyasika, bora na mimi nife sasa ili mama yako na ndugu wengine wafurahi" Rely alizungumza akiwa analia. Nikajua angeishia hapa lakini niliona akisogelea katika ukuta na kujibamiza kwa zaidi ya mara 10, mwisho alidondoka chini na damu zikatapakaa sakafuni. ITAENDELEA
..