DO YOU LOVE ME 17 (S2)
NO, I AM NOT WRONG
Kabla ya kujibu kile nilichoulizwa, nilijifikiria kwa muda mrefu sana. Nikajibu.
“Hapana” Jibu langu nikadhani huenda lingemstua sana Rely lakini hakuwa na wasiwasi wowote. Alijilaza kitandani. Nikastuka! Kwanini aulize halafu nimjibu na kulala pasipo hata kuendeleza maongezi? Sikupata jibu. Nami ilinibidi nijilaze. Nikawa ni mwenye mawazo mno hata usingizi haukuja vizuri.
Usiku huu hatukuongeleshana lolote hadi palipokucha. Asubuhi iliyokuwa na baraka ilitia timu. Rely akawa wa kwanza kuamka, akaandaa chai na kuniletea kitandani. Hapa napo nilistuka. Inakuaje hadi ananiletea chai ikiwa hatuna maelewano mazuri? Anataka kuniua? Sikujipa majibu sahihi ya maswali yangu.
“Nataka kujua ukweli” Rely alisema akiwa ameshikilia mlango, ananitazama usoni. Niliacha kunywa chai, nikamtazama na kumuuliza.
“Upi?”
“Najua mimi si wa thamani tena kwako”
“Nani kasema”
“Moyo wako unamajibu yote lakini nami nijibu swali langu”
“Lipi tena Rely?”
“Rola anakuja saa ngapi?” swali lake likanifanya nikumbuke kumbe kulikuwa na mazungumzo na Rola.
Haraka sana nilichukua simu yangu na kuiwasha kisha nikatafuta namba ya Rola hadi nilipoipata nilipiga. Aliniambia tayari amefika na mara kadhaa amejaribu kunipigia simu lakini sipatikana kama ninaweza basi nijiandae kumfuata.
“Ok, nakuja hapo” nilimjibu na kukata simu. Nikamgeukia Rely na kumwambia “yupo ameshafika” niliweka chai pembeni kisha nilianza kujiandaa kwa ajili ya kuondoka.
Wakati nikiwa najiandaa, Rely naye alikuwa akijiandaa. Kitu ambacho kiliniacha njia panda. Anajiandaa kuna sehemu anakwenda? Kama ndio ni wapi? Sikupata majibu. Nikawa katika wakati mzito na mgumu, ilinibidi nimuulize.
“Unaenda wapi?”
“Umesema ameshafika?”
“Nani?”
“Kwani unaenda kumpokea nani?”
“Kwahiyo unataka kuja ninakoenda?”
“Kuna dhambi yoyote?” Rely aliuliza.
Mie nikapiga kimya. Moyoni nikijiambia kwamba maamuzi yoyote atakayoyachukua ni yeye mwenyewe ndio atajua. Nilifanya yangu hadi nilipomaliza. Nikamtazam Rely alikuwa bado hajamaliza kama mjuavyo wanawake tena kwa kujiandaa. Hii ikanipa auweni ya kunipunguzia mzigo maana sikutaka kuongozana naye. Niliondoka huku nikiimani kuwa Rely asingeweza kunifuata na hata kama angenifuata basi asingeweza kujua niliko ni wapi? Nikijipa imani kuwa Jiji la Dar es salaam ni kubwa.
Lisaa na nusu mbele nilifanikiwa kufika sehemu husika. Nilishangaa kuona mtu kama Rely akiwa anaongea na kina Rola, aliponiona mimi kwa mbali aliaga na kuondoka. Nikastuka ni yeye kweli ama sio yeye? Ilinibidi niende hadi walipo. Nikasimama na kuwasalimu. Rola aliniambia baada ya salam.
“Rely alikuwa hapa muda si mrefu”
“Acha masiara basi, nilimuacha nyumbani ujue?”
“Kweli tena” Alinisisitizia. Nikabaki njia panda maana sikuamini kile ambacho alikuwa ananiambia. Rely amefikaje katika eneo lile ikiwa nilimuacha nyumbani? Bado majibu sikuyapata.
Nusu saa mbele tulianza safari ya kumpeleka katika nyumba ambayo alitaka aishi. Nilikuwa nimeshaipata na kuagizia watu wafanye ukarabati katika baadhi ya maeneo. Kwahiyo, sikuwa na shaka sana kama ingekuwa na muonekano mbaya.
“Umeishiana vipi na Hussein?” Nilimuuliza tukiwa bado katika usafiri
“Kwanza nisamehe kwa nilichokufanyia. Mimi sio binadamu ambayo nastahiki kupewa msamaha wako lakini nisamehe sana”
“Usijali, nilishakusamehe. Niambie, umefikia wapi na Hussein?”
“Anashikiriwa na polisi, kesi yake ni kubwa maana hajaanza kunidhurumu mimi pekee. Kuna watu wana kampuni zao kama tatu, nao pia kawadhurumu. Namchukia”
“Pole sana” Nilimjibu huku moyoni mwangu kukiwa na furaha maana yule mshenzi ambaye nilihisi angenipa kikwazo kwa Rola, hayupo na jeshi la polisi linashughulika naye.
“Rely ananiambia kwamba haoni tena umuhimu wa yeye kuendelea kuishi. Kwani mlikuwa mkiishi maisha mabaya?” Rola aliniuliza.
“Hapana”
“Alikuwa analia. Alionekana kama mtu ambaye mwenye mawazo kupitiliza. Sura yake haikuwa na tabasamu tena”
“Kuna nini?” Nilimuuliza. Kimya kikachukua nafasi, hakukuwa na jibu tena.
Nikiwa nasubiria jibu kutoka kwa Rola, simu yangu iliingia meseji. Nikaifungua, ilikuwa ni meseji ndefu kutoka kwa Rely ikisema.
“Nilifanya makosa kutaka kuwaaminisha watu kuwa unaweza ku’force upendo na ukapendwa. Nilifanya makosa pia hata pale ambapo nilipopata nafasi ya kupendwa niliyoilazimisha, niliichezea. Raheem, najua nini unajua kinachoendelea kuhusu huu ujauzito. Kuhusu maisha yangu kwa ujumla na kadharika. Najua unajua pia kuhusu mateso yote ambayo nimepitia hadi mimi na wewe kuwa pamoja. Tukaishi katika masemango na maneno, tukaishi katika furaha na huzuni lakini mwisho wa siku ukweli utabakia kuwa palepale. Ukweli ambao unanimaliza ndani kwa ndani. Kabla yako kuonana na Rola, mimi nilikuwa naye hapo. Nikamuaga na kumtakia maisha mema akiwa na wewe. Nami nakuaga Raheem. Sina pa kwenda zaidi ya kaburini. Mimi na kiumbe ambaye yupo tumboni, wote tutatangulia sababu siwezi kukupa mtoto ambaye sio wako wala siwezi kumlazimisha yule mwanaume kulea mimba ambayo amekwisha ikataa na hataki kusikia lolote. Muishi kwa amani na mnisamehe kwa kuwakosea” meseji ilikomea hapa. Nikaganda nikiwa nimetumbulia macho simu yangu. Inamaana Rely anataka kujiua? Kwanini afanye hivyo sasa? Nilijiuliza maswali..... ITAENDELEA.