YAMENIKUTA; Alinifungulia Duka nikatembea na Jirani nikidhani atanioa!
Nimeolewa, ndoa yangu ina miaka 7 sasa. Mwaka jana mume wangu alinikfungulia biashara ya duka la spea. Hapa nilipo, jirani kuna duka jingine la lingine la spea kubwa sana. Sasa kuna baba mmoja mtu mzima ambaye alikuwa anapenda kuja kunisalimia mara nyingi. Yeye ameoa ila mke wake ni mara chache sana mke wake anakuja hapa dukani. Ni mama wa nyumbani hivyo mara nyingi anakuwa bize na familia.
Baada ya mimi kuja hapa dukani, nikajikuta tunaanza kuwa karibu na huyu baba, tukaanzisha mahusiano naye. Ni baba ambaye anajali na kila siku alikuwa ananipa mipango mikubwa, akiniahidi mambo mengi. Hela aliyokuwa ananipa ni ndogo, sanasana elfu kumi, kubwa sana ni laki. Ila alishaniambia mpaka ataninunulia kiwanja.
Alishanipeleka mara mbili kuangalia viwanja lakini sikuvipenda. Akaniambia ataendelea kutafuta. Alinipa uhuru wa kuingia dukani kwake ninavyotaka, mpaka kuhesabu pesa ingawa sikuchukua ila wafanyakazi walikuwa wanajua na kuniheshimu kwani mara nyingi anakua mkali sana na kama mfanyakazi asiponiheshimu.
Kutokana na ukaribu wangu naye, nilijikuta naanza kumdharau mume wangu. Mume wangu ni mfanyakazi wa serikali, kipato chake ni cha kawaida tu, hivyo hata kufungua hilo duka alichukua mkopo ili tusaidiane majukumu. Lakini baada ya kumpata huyu mwanaume, nilijikuta namdharau mume wangu. Nasafiri kununua mzigo na kukaa hata wiki bila kupokea simu za mume wangu.
Akiniuliza, namjibu vibaya na kumuambia tuachane. Mume wangu alikuwa anavumilia, mara nyingi yeye ndiye hutaka suluhu na kuomba misamaha hata kama hajanikosea! Kwa mfano, nikiwa safarini akinipigia simu nisipopokea nitamlalamikia yeye kuwa ananifuatilia sana na kumpigia kila mtu kuwa ana wivu!
Wiki mbili zilizopita nilimpigia simu mwanaume, akapokea mke wake. Nilimwambia nataka kuongea na mwenye simu, akauliza "wewe ni nani?" Nikaanza kumtukana na kumwambia mimi mke wa mume wako nataka mwenye simu. Nilimtukana sana yule mama, yeye hakunijibu. Nilifanya hivyo kwa kuwa nilikuwa na jeuri ya mwanaume, kwa kuwa ananipenda na kuniruhusu kuingia dukani kwake kwa uhuru.
Baada ya kuridhika kuwa ameshanitambua, niliakata simu. Baadaye mwanaume alinipigia na kuniomba tuonane naye. Mimi nilijua ni mambo ya mapenzi ila aliponiona alini*piga sana. Alini*piga nusu kun*iua, alinambia hivi unaelewa ni wapi tumetoka na mke wangu? Umenivunjia ndoa yangu kwa ujinga wako. Alisema hanitaki.
Ilikuwa dukani kwake na wakati anamaliza kunipiga, watu walijaa kuangalia kumbe mume wangu alikuwa pale anaangalia kila kitu lakini hakufanya chochote. Nilijizoa na kuondoka, nikachukua PF3 na kwenda kuripoti lakini haikusaidia kwa kuwa mzee anajulikana na kila mtu. Kesi iligeuzwa kuwa mimi ni mwizi na mambo mengine kibao.
Nilirudi nyumbani sikumkuta mume wangu, hakurudi mpaka kesho yake. Hakuniuliza kitu chochote mpaka siku iliyofuata ndiyo akaenda kumchukua mama yangu akaja akanikabidhi kwa mama yangu na kumwambia kuwa yeye ameshindwa na hanitaki tena. Kwa wakati huo akili ilikuwa haijakaa sawa, niliamini kabisa kuwa mume wangu hana ujasiri wa kuniacha pia nilidhani labda yule baba hasira zitapungua atakuja kuniomba msamaha.
Haikuwa hivyo. Mume wangu siku ile aliniacha nyumbani, nikalala kwa mama, ila kesho yake ndiyo tuliondoka alinindikia talaka yangu. Kuja kuangalia kumbe yule baba zile ahadi ni za uongo, nyumba ambayo ina fremu zake ni za wakwe zake, wamepewa tu pia mtaji wa kwanza ni baba mkwe alimpa hivyo familia ya mke wake iko vizuri hataki kunisikia. Nimerudishwa nyumbani na talaka na ninavyoona mume wangu hana mpango wa kunirudia.
Bado nampenda mume wangu, ni shetani tu alinipitia. Huyu baba kaniharibia maisha yangu. Najaribu kumpigia simu tuongee hataki. Mume wangu nimejaribu kumuomba msamaha ananiambia hapana hanihitaji, na kwamba watoto atalea mwenyewe kwani kabaki nao wote. Nisaidie, sijui nafanya nini, najua nilikosea lakini nashindwa nifanye nini kurudisha ndoa yangu!
OFA! OFA! OFA! Kama unataka kujifunza zaidi kuhusu ndoa, basi soma kitabu cha "NDOA NI FURAHA".
Bei yake ni Tsh. 15,000/- lakini leo unaweza kuninunua kwa Tsh. 9,999/- au usubiri ndoa ikishavunjika uje kununua kwa bei halisi."
Kukipata, unalipia TSH. 9,999/- kwa M-Pesa No. 0742-381-155 au Tigo Pesa No. 0657-552-222.
Hakikisha jina linakuja Iddi Makengo, kitabu unatumiwa kwa WhatsApp/Email/Facebook.
MWISHO.