DOLLAR: ( DAKTARI WA HUBA )
Sehemu ya Pili
Mtunzi: Layman Donsue
Siku iliyoanza kama kawaida chuoni iligeuka kuwa sinema ya bure. Mvulana yule aliyeuliza swali gumu kwa Dollar "Wewe mwenyewe unajua kupenda au ni maneno tu?" hakuwa mtoto wa kawaida. Alikuwa na jina la ajabu sana. Aliitwa Mtangazaji, lakini hakuwa na kipindi chochote. Alijieleza kuwa ni mtangazaji wa hisia, mawazo na mitetemo ya moyo.
Mtangazaji hakuvaa kama mwanafunzi wa kawaida. Wakati wengine walivaa jeans na T-shirt, yeye alivaa kaunda suti ya pinki na tai ya njano. Viatu vyake vilikuwa vinalia kila akitembea kama mtu aliyekanyaga mbata wa plastiki. Alipotokea mlangoni mwa darasa, hata lecta alinyamaza kumtazama.
Siku hiyo Mtangazaji aliamua kwenda kwa Daktari Dollar na si kwa ushauri, bali kama mgonjwa wa moyo. Alifika kwenye mti wa kliniki akiwa ameshika maua ya plastiki, akasimama mbele ya Dollar na kusema kwa sauti kama anatoa hotuba ya uchaguzi:
"Leo nimekuja si kwa tiba, bali mimi ndiye nataka kutibiwa. Ugonjwa wangu si kawaida, ni mkusanyiko wa mapenzi yaliyokataa kuingia moyoni mwako!"
Wanafunzi waliokuwa wamesimama kwa foleni wakashangilia kama jamaa kasoma beti la somo la literature. Mmoja alisema:
"Hii kliniki sasa imegeuka kuwa shindano la ngonjera bwana!"
Dollar alimtazama Mtangazaji na kucheka. Alimtupia jicho la juu-chini, kisha akamwambia,
"Una hakika umevaa hii suti kwa akili timamu au ni stress ya kutolipwa boom?"
Mtangazaji hakushtuka. Alitoa kijitabu cha mashairi akasema, "Naomba ruhusa nikusomee kipande kimoja cha moyo wangu."
Kabla hajaanza, jamaa mmoja wa mwaka wa tatu aliyekuwa kwenye foleni alikasirika. Alisimama na kusema,
"Kama mashairi ni tiba, basi hata sisi wenye malaria tungesoma stanza mbili tukapona!"
Vicheko vililipuka kama bomu la pilipili.
Mtangazaji alinyamaza, akaweka maua pembeni kisha akaondoka kwa mbwembwe. Alikanyaga gogo la mti akaanguka vibaya, miguu juu kama kinanda cha kanisani kilichoangushwa na upepo. Badala ya kuumia, aliinuka na kusema,
"Nilikuwa nacheck gravity tu kama ipo bado!"
Hapo wanafunzi walilia kwa kicheko, Dollar akaanguka kwa mgongo huku akisema,
"Hii chuoni kuna watu si wa dunia hii kabisa!"
Lakini siku haikuisha hapo. Mchana huo, Daktari Dollar alipokea mgonjwa mwingine wa ajabu dada mmoja aitwaye Saumu Mcharuko. Saumu alikuja akiwa amevaa dera la wedding lakini alivaa viatu vya ndondocha, huku akisema:
"Daktari Dollar, nisaidie. Mapenzi yananitafuna kama njugu kwenye meno ya kipofu!"
Dollar akainua jicho akasema, "Tatizo nini, Saumu?"
Saumu akajibu kwa sauti ya kulia:
"Mpenzi wangu amenitumia meseji ya ‘K’ tu baada ya mimi kumtumia paragraph tano za mapenzi! Tena ‘K’ kubwa kabisa, si ya kawaida!"
Wanafunzi waliokuwa hapo walishindwa kuvumilia. Mmoja alishika tumbo la kulia, mwingine akainama chini kama anaomba msamaha kwa mbavu zake. Dollar alipojibu, alisema:
"Hiyo ‘K’ ni kifupi cha ‘Kaendelee!’ Yaani hamtaki tena hata kusoma feelings zako!"
Baada ya kutibiwa, Saumu alitoka kwa madaha kama aliyeshinda kesi mahakamani. Aliwaambia wote, "Nimepona, nitapenda upya na kwa staili mpya. Hakuna mwanamme mwenye leseni ya kuniua kwa emoji!"
Lakini usiku huo huo, Dollar alipokea meseji ya WhatsApp kutoka kwa namba ngeni. Ilisema:
"Usidhani unaweza kutibu mapenzi yote bila wewe kuumizwa. Siku zako za kucheka zinahesabika."
Dollar alitazama meseji hiyo na akapigwa na butwaa. Nani alikuwa anamtisha? Kwa nini? Na je, kliniki ya huba ilikuwa inakengeuka kuwa uwanja wa vita?
ITAENDELEA....