SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), limemteua mwamuzi wa kati, Pierre Ghislain Atcho kutoka Gabon kusimamia mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho kati ya wenyeji, RS Berkane ya Morocco dhidi ya Simba kutoka nchini Tanzania.
.
Simba itaanza kampeni za kusaka taji hilo kubwa Afrika kwa kucheza fainali ya kwanza ugenini Mei 17 ikiwa Morocco, kisha baada ya hapo itarudi jijini Dar es Salaam kwa mechi ya marudiano itakayopigwa Mei 25, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huku kombe likiwa uwanjani.
.
Atcho anakumbukwa zaidi na Simba, kwani aliwahi kuchezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, ambayo timu hiyo ya Msimbazi ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, Disemba 19, 2023.
.
Atcho atasaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja, Boris Marlaise Ditsoga wa Gabon, msaidizi namba mbili ni Eric Ayimavo Ayamr Ulrich wa Benin, huku refa wa akiba mezani atakuwa Patrice Tanguy Mebiame wa Gabon.
.
Kwa upande wa Teknolojia ya Video Assistant Referee (VAR), katika mechi hiyo itaongozwa na Abongile Tom wa Afrika Kusini akishirikiana na Maria Packuita Cynquela Rivet wa Mauritania, huku msaidizi wa pili ni Diana Chikotesha kutokea Zambia..