Kutoka kwa Abuu Qataada Al-Answaarii Radhiyallaahu anhu Amesema kuwa Mtume Swallallaahu aleyhi wasallam aliulizwa kuhusu Sawmu ya siku ya Arafa akasema “Hufuta madhambi ya mwaka uliopita na unaobakia, Akaulizwa kuhusu Sawmu ya siku ya ‘Ashuuraa akasema “Inafuta madhambi ya mwaka uliopita. Akaulizwa kuhusu Sawmu ya siku za Jumatatu, akasema “Hiyo ni siku niliyozaliwa na siku niliyopewa Unabiy na ni siku niliyoteremshiwa Qur-aan. HADITH Muslim
Hii inamaanisha kuwa dhambi ndogo hufutwa kwa sababu ya Sawmu lakini dhambi kubwa hufutwa kwa kutubu tu. Ama kuhusu haki za watu, madeni ni wajibu kurudisha kwa wenye haki, kuhusiana na mdaiwa kusamehewa kunategemea matakwa ya watu wanaomdai. ‘Arafa ni jina la siku ya 9 ya mwezi wa Dhul-Hijja (Mfungo tatu au mwezi wa kumi na mbili wa Kiislamu), na Ashuuraa ni siku ya 10 ya mwezi Muharam yaani Mfungo nne au mwezi wa kwanza wa Kiislam. Mtume Swallallaahu aleyhi wasallam alipenda kufunga siku za Jumatatu lakini hakuelezea juu ya thawabu zake. Na Allaah Anajua zaidi.