STORI:
Saa sita na nusu usiku, zilisikika kelele za mama mjamzito akishushwa kutoka kwenye gari, mumewe akimtia moyo na kumpa maneno ya faraja, lakini maneno hayo hayakuweza kumpunguzia uchungu aliokuwa akiusikia. Aliendelea kulalamika akisema:
"Mume wangu nakufa, tumbo linanikata kata, sijui kama naweza kuiona kesho. Oh, ooo, mwenzenu tumbo langu mie..."
Mumewe alidondosha machozi kwa kumuhurumia. Alitamani ule uchungu uhamie kwake.
"Najua ni kiasi gani mke wangu unaumia. Kama uliweza kuvumilia manyanyaso, kashfa, dharau, kutukanwa na ndugu zangu kisa hujawai kuzaa... Pia uliweza kuvumilia wakati tunahangaika kwenda mahospitalini, kwa waganga wa kienyeji ili kupata tiba ya tatizo la kutokuzaa kwako. Hatimaye baada ya miaka 20 Mungu amesikia kilio chetu, tunaenda kuitwa baba na mama. Usilie mpenzi, onyesha furaha."
Muda huo walishafika mapokezi, nesi alimpokea kwa maneno ya kejeli:
"Mtoto wa kike, jikaze bwana, unalia lia unafikiri hapa kwa mama yako? Ndiyo ujue, mwanzo wa utamu mwisho wake uchungu."
Mmewe alimgeukia nesi akimuomba apunguze ukali wa maneno kwa mkewe.
"We unanifundisha kazi?? Unataka nimbembeleze? Amekuwa mtoto mdogo?? Ajikaze, analegea utadhani ni mimba ya kwanza!"
"Ndiyo nesi, katika maisha yetu ya ndoa hatukubahatika kupata mtoto. Hii ni mimba ya kwanza kwa mke wangu."
Nesi kidogo upole ukamshika na kuuliza:
"Kweli? Umri wote huu hamna mtoto??"
"Ndiyo hivyo nesi, mm mkubwa."
"Haya, nisaidie kumnyanyua tumpeleke kwa daktari."
Dr. Mery akiwa ofisini kwake, mlango ulifunguliwa akaingizwa yule mama mjamzito. Chupa ya uzazi ilishapasuka na alianza kutiririsha damu. Dr. aliamuru apelekwe chumba cha kujifungulia haraka. Alipopelekwa, njia ya kutokea mtoto ikawa ndogo.
Mumewe alikuwa nje akifurahia, muda mchache ujao ataitwa baba:
"Tumehangaika sana hospitalini, kienyeji, mke wangu aweze kuzaa. Kweli nimeamini mvumilivu hula mbivu."
Akaona kitanda kikitolewa kwa kasi, akauliza kwa hamaki:
"Nesi, nini tena?"
"Mkeo ameshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida, hivyo tunampeleka chumba cha upasuaji."
"Upasuaji tena??"
Wala hakujibiwa, naye alichofanya ni kufuata kwa nyuma.
Dr. Mery ndiye aliyekuwa anaongoza upasuaji. Walifanikiwa kukitoa kichanga salama, lakini pete aliyovaa Dr. Mery ilitoa mwanga. Hiyo iliashiria kuna ujumbe anatakiwa kuupokea. Aliipeleka pete hiyo sikioni, akasikia sauti ikimwambia:
"Tunakiitaji hicho kichanga huku kuzimu."
Sauti ikakata. Alimshona mzazi na kumwamuru nesi ampeleke wodini, wakati yeye akiendelea kushughulika na kile kichanga.
Mme wa yule mzazi alisimama baada ya kuona mlango wa chumba cha upasuaji ukifunguliwa. Alimuona mkewe akiwa bado hajitambui, nesi alitabasamu akimpa hongera kwa kumpa hongera ya kupata mtoto wa kiume. Aliruka ruka kwa furaha, akimbusu mkewe mfululizo ambaye alikuwa anapelekwa wodini.
Huku nyuma, Dr. Mery alikatazama kale kachanga ambacho kanatakiwa kapelekwe kuzimu. Kalikuwa katoto kazuri kavulana mwenye afya njema. Aliinamisha uso wake chini, akachukua vidole vyake viwili na kubana pua ya kale katoto. Maskini, kalishindwa kupumua, kakakata roho.
Nesi baada ya kumfikisha mgonjwa wodini, alimwambia mme wa yule mama:
"Ngoja sasa nikakuletee jembe lako,"
akimaanisha mtoto wa kiume.
"Halafu umwangalie mkeo, maana akizinduka hapo atataka akae. Si unajua ana mshono?"
Akizipiga hatua kuelekea chumba cha upasuaji, alipofika hakusikia kelele za mtoto kulia. Alimuona katulia, ikabidi amuulize Dr:
"Aka katoto vipi? Mbona nashindwa kukaelewa?"
Dr. Mery alimjibu:
"Huyo mtoto si rizki."
"Dr. mbona nashindwa kukuelewa? Si rizki kivipi??"
"Unashindwa kunielewa nini? Ina maana maiti huijui?"
"Haa Dr. apana! Mtoto ametoka akiwa na afya njema hana tatizo, eti amekufa?!!!!"
Dr. Mery akamwambia:
"We unamuona mzima huyo??"
"Imekuwaje akafa Dr.?"
"Mi siyo Mungu, nenda kamwite mzazi wa hii maiti apewe taarifa ya kifo cha mtoto wake."
Nesi aliyejulikana kwa jina la Nesi Tina akiwa mwenye mawazo, akishangazwa na kifo cha ghafla cha yule kichanga. Pia anawaza atakavyowaambia wazazi wale waliokuwa na shauku kubwa ya kupata mtoto baada ya kuhangaika takribani miaka ishirini.
Kule wodini, mzazi alizinduka kutoka usingizini. Cha kwanza aliomba apewe mtoto wake.
ITAENDELEA...
FULL 1000
๐ 0699286085.