Mtunzi: Lipeta s Shaaban
Katika mji wa Mugoroka, usafiri wa DANHEKI ulijulikana sana kwa kelele, mizaha na hadithi zisizoisha. Ndani ya basi hili la rangi ya njano lililokuwa limechakaa kidogo lakini lina roho ya watu wa kawaida, kila abiria alikuwa na mchango wake – wengine kwa stori, wengine kwa kelele, na wengine kwa kuvunja mbavu kwa vicheko.
Siku moja ya Jumatano, jua likiwa kali kana kwamba limetumwa na shetani mwenyewe, mama mmoja aliyejulikana kwa jina la Mama Nkamia alikwea basi la DANHEKI. Alijulikana mjini kwa mavazi yake ya gharama na mdomo wake usiotaka kushindwa – yaani alikuwa anafoka kama redio ya mkoloni.
Aliingia ndani ya basi akiwa amevaa kitenge cha rangi kali, mikufu mingi shingoni, na uso wake ukionyesha kiburi cha "mimi si wa kawaida kama ninyi." Abiria wote walinyamaza kwa muda wakimwangalia – wengine kwa mshangao, wengine kwa hasira.
Lakini hakukuwa na kiti. Kwa bahati mbaya, alikalia tu kile alichodhani ni kiti cha plastiki – kumbe! Ni ndoo ya samaki ya mtu mmoja aitwaye Mzee Jashua, ambaye alikuwa ameitumia kuwekea vibuyu vyake vya dagaa na kuishika kwa mguu wake tu.
Ndani ya sekunde, ndogo hiyo ilimshika vibaya. Akashindwa kuamka. Nguo yake ikakwama, ndoo ikavuta kitenge chake hadi chini! Wote wakapigwa butwaa – lakini si kwa huruma – bali kwa mshangao wa kufurahisha.
Watu wakaanza kucheka. Mama mmoja akasema, “Eeh! Hapo siyo kiti, ni mtego wa madharau!” Konda akatoa megaphone, akasema kwa sauti ya kuchekesha:
> “Habari ya leo: Mama wa mtaa wa Mzuka amevua kitenge kwa ndoo ya dagaa!”
Kicheko kikatawala. Hata dereva, Bwana Masinde, akashindwa kuendesha vizuri kwa kicheko kilichomlemea. Watu walikuwa wanamnyooshea vidole huku wengine wakilia kwa vicheko.
Mama Nkamia akajaribu kuvuta kitenge chake, lakini ndoo ikawa kama imeapa – haiachi mpaka aachane na kiburi chake.
Akiwa amedhalilika, uso wake ukibadilika kuwa mwekundu kama pilipili kichaa, akasema kwa hasira:
> “Hamjui mimi ni nani? Nitamripoti kila mmoja wenu!”
Lakini maneno yake yaliishia kwa kicheko kingine kikubwa. Hatimaye, aliweza kujinasua na kutelemka kituoni akitokota kama chungu cha maharagwe ya usiku.
FUNZO LA SIMULIZI: Usimdharau yeyote kwa mavazi au hali yake. Kiburi kinaweza kuvuliwa hadharani, mbele ya watu waliokuogopa kwa muda mfupi. Na usiingie basi la watu wa kawaida ukiwa na moyo wa kifalme – maana unaweza kujikuta ukikalia ndoo ya aibu.
---.