“Jamani msaada, msaada, naombeni mfanye haraka asije kujifungua katika gari. Ebu pelekeni machela haraka jamani” ilikuwa ni sauti ya moja ya muuguzi katika hospital ya Seketule jijini Mwanza.
Sauti iliyojaa taharuki ya kuomba msaada iliendelea kusikilizwa na watu mbalimbali ambao walimwangalia muuguzi yule aliyekuwa akikimbia kama chizi. Hii ndio ilikuwa kazi yake naye alitaka kuifanya kwa weledi kabisa.
Alihakikisha kwamba anapata machela kwa uharaka ili kusaidia Maisha ya mwanamke ambaye alitaka kuleta kiumbe kipya katika uso wa dunia. Baada ya dakika mbili alifanikiwa kupata machela huku wauguzi wengine wakimuunga mkono na kwenda kumtoa mgonjwa katika gari la wagonjwa na kumweka kwenye machela.
Kwa ushapu wa hali ya juu walifanikiwa kumpeleka hadi kwenye chumba wodi ya wazazi.
“Samahani naombeni mkae nje kidogo” Alisema yule muuguzi kumwambia mwanaume na mwanamke ambao walikuwa kama sehemu ya waangalizi wa mwanamke yule.
Nao bila kupinga walisogea kwa pembeni huku wakiwa wamechanganikiwa mno, vichwa vyao muda wote viliwaza kuhusu hatima ya Mama na mtoto. Sio moja wala mbili ambalo lilikuwa linakuja akilini.
“Shemeji usijali, Mayner atakuwa sawa” alisema mwanamke huku akimuita mwanaume kwa jina la Mayner
“Iwe hivyo, unajua akili yangu umevurugika kabisa. Sijioni nikiwa mzima kama akishindwa kujifungua salama maana hizi mimba za kwanza nasikiaga zinasumbua sana”
“Hata kama ndio mimba yake ya kwanza ila atakuwa sawa, usijali” yule mwanamke alisema kisha alitazama wodi ya wazazi, akaweka tabasamu baada ya kusikia sauti ya kichanga ikisikika kwa ndani.
“Nahisi itakuwa tayari sijui?” alisema
“Mh! Mbona mapema hivyo?”
“Hata kama ni mimba yake ya kwanza, kuna wengine Mungu anawajalia wanakuwa sawa” alieleza yule mwanamke.
GARMA OLANI AHMED ndio mpenzi halali wa Mayner ambaye leo hii yupo katika chumba cha wazazi kwa ajili ya kuleta kiumbe kipya katika uso wa dunia. Mapenzi yao yalikuwa na misuko suko mingi lakini walifanikiwa kuivuka na sasa walikaribia kuitwa Baba na Mama.
Jambo kubwa ambalo lilikuwa linasumbua penzi lao ni tabia ya Mama yake ambaye hakutokea kumpenda Mayner, kwake alimchukulia kama mwanamke wa hadhi ya chini mno. Mwanamke ambaye hapaswi kulala kitanda kimoja na mwanawe.
Kila kukicha hakuacha kumpigia kelele mtoto wake kutafuta mwanamke mwingine wa kuoa lakini sio Mayner ila mapenzi ya dhati yalimuendesha Garma hakutaka kumsikiliza Mama yake. Kwake aliamini kwamba Mayner ni mwanamke mzuri na anapaswa kupewa heshima ya ndoa.
Hata kama walikuwa hawajaoana lakini tayari walikuwa wanaishi pamoja, hii ilikuja mara baada ya Mayner kushika ujauzito. Kitu ambacho kilimfanya awe na kila sababu ya kumpenda kiumbe kipya hata kabla hakijaja duniani, hivyo aliamua kumvuta katika nyumba yake iliyopo maeneo ya Busweru jijini mwanza.
Maisha hayakuwa mazuri sio kwa sababu Mayner alikuwa na mimba lakini Mama yake hakuonesha ushirikiano kabisa, alikuwa anamchukia Mayner kupita maelezo na mara kadhaa alimkuta akimpiga bila hata ya sababu ya msingi.
Licha ya kujua kwamba Mayner alikuwa na ujauzito lakini kwake hakuliweka mbele hilo, lengo lake lilikuwa ni kumuua kiumbe yule. Aliimani kwamba endapo angefanya jambo hili kwa wepesi basi ingekuwa ni rahisi kwake kumpandikiza mtu ambaye anampenda kwa mtoto wake kisha akamuoa na sio kumuoa Mayner.
Leo hii Mayner yupo Hospital lakini Mama wa Garma hana hata habari ndio kwanza yupo zake nyumbani anaangalia runinga.
“Mama! Twende basi hospitali, kidogo wewe ni mtu mzima unaelewa hizi mambo”
“Khe! Niende hospital kumsaidia mwanamke gani? Huyu mwenye dimpozi kama mpuliza moto katika jiko la kuni au kuna mwingine? Nendeni na huyo mtoto lazima afe, hawezi kuwa hai”
“Mama! Maneno gani haya unaongea?”
“Lipi neno baya? Lipi baya hapo? Halafu Garma usitake kunipanda kichwani tafadhari nakuambia”
“Ok, ila haya nitamwambia Dada na tusilaumiane huko mbeleni. Naenda hakuna shida” maongezi haya yaliranda katika kichwa cha Grama wakati yupo hospitali.
Alijikuta akifuta machozi kisha akamtazama shemeji yake ambaye alikuwa anaitwa Laila, huyu alikuwa ni Rafiki wa Mayner ambaye alikuwa akifanya kazi maeneo ya poster hivyo alimuomba ili aje ampe kampani naye alikubali kufanya hivyo.
“Kwanini mama hajakuja leo, nilitegemea angekuwa hapa nawe” Laila alisema
“Mama anaumwa, hajisikii vizuri”
“Na vipi kuhusu dada yako? Kaenda wapi?”
“Rasma kasafiri, ameenda Mara moja kuna mambo ambayo niliyafanya kule, kaenda kusimamia, ila hakuna shida kila kitu kitae….” Garma aliamua kuficha ukweli juu ya familia yake lakini hata kabla hajamalizia.
Daktari wa kike alitoka katika chumba kile huku akionekana kama mtu ambaye alikuwa na furaha hivi.
“Dokta tayari ameshajifungua?” Garma aliuliza huku akipiga hatua kumkaribia yule dokta
“Ndio, subiri nakuja” alisema Daktari kisha aliondoka mahala pale. Garama aliweka mikono juu na kumshukru Mwenyezi Mungu, tabasamu lilikuwa katika uso wake.
Kwa hatua za kawaida alienda hadi ofisini kwake kisha alitoa simu katika mfuko wa nguo aliyokuwa ameivaa, akaiwasha kwakuwa alikuwa amezima. Akachezea kidogo na kuweka sikioni.
“Hellow Ninah”
“Niambie, umekamilisha kila kitu au bado?”
“Tayari, ila bado sijaweka sumu kwa yule mtoto?”
“Fanya haraka wewe, halafu hakikisha damu yake ya uzazi inapatikana”
“Damu tena?”
“Ndio, nataka kufunga kabisa kizazi chake mbwa huyo. Kila siku anaambiwa apendwi lakini haelewi. Vipi uliongea na Mama wa Garma au naye kaja hapo?”
“Thubutu, yupo sijui na nani ila sawa hakuna shida nitakuja kukuambia. Hela yangu si ipo tayari maana hakuna ushoga katika hili. Nahatarisha Maisha ya kazi ujue” alisema yule Daktari huku akiigandamiza simu kwa kutumia bega na sikio.
“Ndio, hela ipo we fanya jukumu lako acha mambo mengi basi. Unapenda hela kama mchaga kha!”
“Hahaaha! Hela muhimu, basi hakuna shida mwaya acha nikamuue mtoto kabisa” Daktari alisema kisha alikata simu.
Alirudisha simu katika mfuko wake huku akiizima na kutazama kulia ambako kulikuwa na kabati lenye kila aina ya dawa pamoja na sindano ambazo zingefaa katika maangamizi. Alichagua moja ya dawa ambapo alichanganya.
“Soft poison, hakuna ambaye atajua kama mtoto ameuawa” alisema huku akiweka tabasamu.
Alipomaliza kuchanganya alitoka ndani kuelekea katika wodi ya wazazi huku akionekana kama mtu ambaye alikuwa na haraka hivi. Aliingia hadi ndani na kuwakuta wauguzi wengine, akawatazama na kuonesha ishara kwamba waondoke nje.
Nao hawakutaka mambo mengi waliondoka mahala pale huku wakitazama, naye alitupa jicho katika kitenga maalumu ambacho kilikuwa na mtoto. Akaweka tabasamu na kumsogelea lakini kabla hata hajamfikia alisita kidogo.
Kusita huku kulitokana na kuhisi kama Mayner ambaye alijifungua muda mfupi uliopita kuzinduka. Lakini hakukuwa na ukweli wowote badala yake alikuwa amelala huku maumivu yakiwa pembeni yake.
“Kalala kweli” alijiuliza na kupiga hatua za kinyume nyume hadi alipomfikia Mayner na kupitisha pitisha mkono katika uso wake “Yeah kalala”
Alipogundua kuwa ni kweli amelala, alipiga hatua hadi eneo ambalo mtoto alikuwepo kisha alimdunga sindano katika eneo la unyayo wa mguu wa kulia. Alifanya hivi kwa makusdi akiimani kwamba hakuna mtu ambaye angejua kama mtoto amedungwa kitu.
Sauti ya maumivu kutoka kwa kichanga ilisikika, ilikuwa si sauti ya kawaida kama waliavyo watoto wengine badala yake alilia haswa hadi Mayner alizinduka kutoka katika usingizi mzito akasema “Mwanangu” sauti yake ilimstua daktari ambaye kwa haraka alificha sindano lakini kwa bahati mbaya ilidondoka chini kutokana na wasiwasi ambao ulimfanya asijue wapi alikuwa anaweka sindano ile…. ITAENDELEA.