Niliondoka zangu nyumbani huku nikiwa mtu mwenye mawazo sana kufuatia maongezi ambayo mume wangu aliokuwa amewasiliana na mtu katika simu. Niliwaza ni nani ambaye alikuwa akiongea na mume wangu, dada yake gani ambaye alikuwa akipangiana mpango ule ambao wao waliuona kuwa ni mzuri lakini ungeenda kuhatarisha maisha ya Mama
Kichwa changu muda wote hakikuacha kunipa maswali kama sio msongo wa mawazo. Nilijiuliza "kwanini nimekuwa na mwanaume ambaye hamthamini mama yangu? kwanini nimekuwa na mwanaume huyu ambaye ni m'baya kupindukia? Kuna kosa lolote lile ambalo nimelifanya kwake?" Maswali yangu yaliniumiza kichwa kwakweli. Nilijaribu kurudisha siku nyuma labda ningekumbuka ni baya gani ambalo nimelifanya lakini sikuona.
Ilifikia hatua nikawa nadondosha machozi ndani ya gari, maumivu makali yalikuwa yanaendelea kunimaliza katika mwili wangu hata nilipokuwa hospital sikuacha kudondosha machozi. Nafsi yangu iliumia, moyo wangu uliumia hata sura yangu ilibadilika kabisa. Kuna muda watu ambao walikuwa wakinipita hawakuacha kuniuliza nami nilizuga ni afya ya Mama ndio inanifanya niwe vile. Lakini ukweli haukuwa hivyo, nilikuwa namuwazia mume wangu na chuki dhidi ya Mama.
Wapo ambao walinipa pole na wapo ambao waliendelea kupambana na hali zao kama unavyojua hospital kila mmoja anajali jambo lake. Muda wa chakula kwa wagonjwa ulipofika niliingia katika chumba cha mgonjwa wangu, nilimkuta Mama akiwa amechoka mno.
Nami nilisogea pembeni ya kitanda kisha nikaa karibu yake na kumgusa kichwa chake. Machozi yalinidondoka taratibu, moyo wangu uliniuma kumuona mwanamke ambaye amepigana na mimi kwa hali na Mali akiwa katika hali ile.
"Mama unaendeleaje?" Nilinyanyua mdomo wangu kwa mara ya kwanza huku nikifuta machozi ili kumpa imani mama.
"Naende, naendelea vizuri. Naendelea vizuri mama" alinijibu lakini jibu lake halikuwa la kuridhisha, alijibu ili kunipa imani juu ya afya yake lakini ukweli hakuwa anaendelea vizuri.
Nilimtazama kisha nikalitazama hotpot ambalo lilikuwa katika mapaja yangu. Nilitoa na kuweka kitandani kisha nikamtazama Mama.
"Kuna hichi chakula mama, si tunaweza kula wote" nilisema
"Sawa usijal ila mimi sijisikii kula"
"Mama inabidi ule, ule ili upate nguvu si unajua unatumia dawa ambazo zina nguvu sana"
"Nahisi kushiba mwanangu"
"Hakuna cha kushiba hapo mama, kinachokufanya udhani kwamba umeshiba ni huo ugonjwa ebu kula bwana" nilisema na kuanzakumlisha Mama yangu kwa kutumia kijiko
Kama unavyojua kwa wauguzi wengi huanza kwanza kumlisha mgonjwa kabla ya kwao, ndivyo ilivyokuwa kwangu. Nilianza kumlisha kwanza Mama kisha nilipomaliza nilirudisha hotpot nje katika eneo ambalo kulikuwa na mizigo yangu mengine.
Niliweka halafu nilielekea katika chumba cha Daktari ili kupata maelezo ya hapa na pale juu ya afya yake.
"Kwanini mmechelewa kumleta hospital Mama?" Daktar aliniuliza akiwa ananitazama na muda mwingine aliinamia katika daftari sijui hata alikuwa akiandika nini?
"Alikuwa anaishi kijijini, mara kadhaa nilikuwa natuma hela huko kwa kuimani kwamba wangempatia matibabu lakini haikuwa hivyo. Nimekuja kujua juzi tu"
"Aise, pole sana"
"Asante Dokta"
"Hm! Mama anaumwa tena sana tu, tupo kama jopo la madaktari tunaendelea kupigania uhai wake na naimani kwamba atakuwa sawa" Daktar aliniambia.
Maneno na kauli zake zilinipa imani na kuamini kwamba Mama angepona na maisha mengine yangeendelea. Nilishapanga kwamba kama nikitoka naye pale hospital basi ningeenda naye nyumbani, sikujali nini kingetokea lakini nilichokuwa nahitaji safari hii ni kuishi na Mama yangu.
Hatimaye Jioni ikaingia, haikudumu sana iliweka ustarabu katika mkoa wote na kufanya hali ya amani kuwako katika eneo lile. Madaktari waliendelea kumsaidia Mama yangu kwa kumpa matibabu kwa kadri muda ulivyozidi kwenda.
Nami sikuacha kumpigia simu mume wangu ili niweze kumpa taarifa na kumjulia hali si unajua mtu chake. Ila jambo la kushangaza ni kwamba kati ya simu 20 ambazo zilitoka kwa siku nzima, hakuna hata moja ambayo aliishika. Ni kama tulikuwa tumegombana lakini ukweli haukuwa hivyo. Tuliacha poa kabisa siku ambayo nilitoka pale na sikudhani kama kulikuwa na tofauti yoyote ile baina yetu.
Alidharau simu yangu, hakuwa hata akihitaji kuzungumza na mimi. Nilipoona nimempigia mara nyingi, nikajiambia kwamba natakiwa kulinda amani ya moyo wangi. Kama angeniona wa muhimu basi angenipigia. Sikujua kama ndio nilikuwa nachimba kaburi la mawasiliano yetu kwa muda wote kwani nilitahamaki kukiwa kumepambazuka, asubuhi nyeupe ilikuwa mbele yangu lakini simu ya mume wangu sikuiona.
Iliniumiza ndani ya mtima, niliumia nisiwe muongo. Unajua kumpigia mtu ambaye unampenda kutoka moyoni halafu asijibu simu yako inaumiza sana, ndivyo ilivyokuwa kwangu. Lakini baadaye nilikaa na kuwaza nikasema labda kutakuwa na sababu nyingine kama vile kuwa mbali na simu, ama kuwa busy na mambo yake hasa ya kibiashara lakini swali lililokuwa likiniumiza kichwa ni "sawa alikuwa busy ndio missed call 20 hazistuke na kujiuliza kwanini nampigia muda wote?" Nilijiuliza ila niliacha kujiuliza pale ambapo Daktari alinihitaji katika chumba chake.
Nilienda kwa mara ya pili kumsikiliza ukiachana na ile ya jana. Nilipofika niliweka makalio yangu katika kiti na kumtazama.
"Mama anaendelea vizuri sana, sikutegemea kama angekuwa mtu wa furaha kiasi kile" alisema yule Daktari.
"Mh! Inamaana dawa zimemsaidia?"
"Ndio halafu jambo la kushangaza ni kwamba hizi dawa wengine wanachukua hadi mwezi wapo hapa lakini kwa Mama imekuwa tofauti aise"
"Asante sana Mungu, asante sana" nilisema na kunyoosha mikono yangu usoni.
Sikuamini kama ile taarifa ambayo nilikuwa napewa ina ukweli hadi pale ambapo nilikwenda kumtazama Mama yangu. Nilimkuta Mama akiwa na uzima ingawa sio sana lakini itoshe kusema kwamba alikuwa na mabadiliko makubwa sana katika mwili wake.
Ama kwa hakika Mungu anaweza kukuinua ili wabaya wako waumbuke nakuumia zaidi hasa pale ambapo watakuona unafanikiwa ilhali walitaka ushindwe. Ndicho kilichokatokea kwani mara baada ya Mama kula chakula chenye sumu. Sumu ile ilienda kusafisha ugonjwa ambao Mama alikuwa anaumwa na sio kumuua tena.
Kula kwake chakula ndiko kulimpa uhafadhari kama sio nafuu katika maisha yake. Kwa mara nyingine nililiona tabasamu la Mama yangu likiwa mbele yangu, niliona Mama akicheka na kuniimbia huku akinikumbusha wimbo wa Kidaripoo ambao nilikuwa naupenda sana.
Nilifurahi kuliona tabasamu la Mama, nilifurahi kumuona mwanamke yule muhimu katika maisha yangu akirudi tena kuwa na afya tele. Tulizungumza mengi hata aliponiuliza kuhusu mume wangu kama alikuja pale, ilinibidi nimfiche kwa kumwambia
"Ndio alikuja na alikuona muda ambao ulikuwa umzidiwa ila ameondoka" ilinilazimu niseme uongo ili kumlinda mume wangu maana sikutaka aonekane m'baya.
"Zamda mwanangu, maisha yako yameshikiriwa na mume wako. Hakikisha kwamba huyu unamheshimu, unampenda na kumtamini mchukulie kama sehemu ya watu wako wa muhimu waliobakia duniani ukinitoa mimi" Mama aliniambia
"Maa, nitajitahidi kadri niwezavyo ili kuendelea kudumisha upendo na Kazumar. Sitakubali nimpoteze na nitampenda kila leo katika maisha yangu. Asante sana kwa kunikumbusha Mama yangu" nilimwambia Mamaa huku machozi yakinitoka.
Jioni ilipofika nilielekea nyumbani kwangu kuandaa chakula kwa mara nyingine. Nilipofika sikumkuta mume wangu, sijui alikuwa amekwenda wapi? Nami sikuona kama napaswa kumpigia maana zile meseji ambazo nilimtumia pasi kuzijibu zilitosha kunithibitishia kwamba alikuwa busy tena ukijumlisha na simu nilizopiga ndio kabisa.
Niliingia zangu chumbani ambako niliendelea bafuni na kuoga kisha nilirudi tena jikoni. Nikaanza mapishi kama ilivyokuwa kawaida yangu hadi kufikia saa 11 nilikuwa nimekamilisha kila kitu.
Niliweka chakula katika hotpot kisha niliondoka zangu kuelekea hospital kama ilivyokuwa kawaida. Nilipofika tulikula na kucheka, tena ilikuwa mbele ya Daktari ambaye hakuacha kunisisitiza kwamba niwe karibu na Mama maana ameshakuwa mzee sasa.
"Tunazitamani pepo ndio maana tunamwabudu Mungu, mtunze sana Mama. Mpe mapenzi ya dhati maana kuna watu hawajawaona Mama zao tangu walipoingia duniani na wengine hawakunyonya kabisa maziwa. Ukiwa na mwanamke ambaye amekuleta duniani basi mthamini na kumjali" aliniambia yule Daktari.
Maneno yake ingawa yalikuwa ni machache lakini yalinidondosha machozi, yalinifanya nilie mbele ya Mama ambaye nilimkumbatia. Niliumia ama kulia sababu kuna kipindi nilikuwa namtenga, si jwa ubaya ama kutaia bali ni mume wangu ndio alinifanya niwe mbali na mama, basi nilizidi kumkumbatia na kumwambia "Nakupenda mama, nitapambana nawe kwa hali na mali"
"Usisahau kumpenda na Kazumar mwanangu, najua haya matibabu ni yeye ndio ametoa idhini" Mama alisema. Nilitamani nimwambie ukweli juu ya Kazumar kutokushika simu zangu ila nilificha sikujua kama naficha maradhi ambayo siku ya kifo yangeniumbua.
Basi siku hii iliisha kisha ikaingia siku nyingine ambayo Daktari alinipa ruksa ya kurudi nyumbani nikiwa na Mama. Niliondoka pale hospital kama saa 10:34 Jioni na kuelekea nyumbani kwangu.
Nilipofika ama tulipofika nilimkuta Mume wangu akiwa na ndugu yake ambaye anaitwa Sofia. Kama ukiniambia nimwelezee alikuwa anaonekanaje basi nitambua. Alikuwa ni mrefu sio wa kuzidi futi 5.8 wala wa kupungua futi 5, hakuwa na ubaya hata kidogo. Sura nzuri ya kumvutia kila mwanaume ingawa hakuolewa ilimfanya kuwa na maringo tele.
Mwanya mdogo ulikuwa katika meno yake ya juu, komwe dogo kiasi ambalo lilimpa uzuri wa sifa pamoja na umbo namba nane. Huyu ndio alikuwa Sofia, nadhani maswali kuhusu kwanini hakuolewa jibu lake linakuja pale utakaposema 'Mungu hakupi vyote' kipo ambacho atakunyima.
Sofia licha ya kupewa uzuri kupindukia kimuonekano lakini alipewa roho ya korosho, alipewa roho ya wahindi kwa waafrika. Alipewa roho mbaya, alikuwa sio mtu hata kidogo. Umri wake wa miaka 25 ambao mimi nilimzidi miaka miwili, lakini kwake nilionekana kama mtoto wa miaka 15 hivi. Sio mimi tu hata Mama yangu pia.
Sasa baada ya kufika kama ilivyokuwa kawaida ya watu wenye dhana mbaya uficha makucha ili hata watakapokurahua usijue, ndivyo ilivyokuwa kwao.
"Anh! Mama samahani karibu" Kazumar ambaye ni mume wangu alisema huku akisimama na kumkaribisha Mama katika sofa. Uso wake ulikuwa na tabasamu mno
"Asante baba"
"Baby kumbe unakuja na mama husemi?" Mume wangu alinigeuzia kibao.
Kwakuwa mahala pale kulikuwa na Mama ambaye nilishamwambia uongo kuhusu Mume wangu ikiwa kama sehemu ya kumlinda basi niliona napaswa kuwa mjinga kwa kufunika kombe, nikasema.
"Simu yangu imezima tangu asubuhi, nisamehe sana. Naona umekuja na wifi"
"Ndio, niliona anapaswa kuwa hapa ili awe karibu na Mama wakati sisi tukiwa katika mizunguko yetu"
"Anh sawa, karibu wifi"
"Asante"
"Sawa acha mimi nikaoge kwanza" niliongea kisha niliondoka zangu huku nikielekea chumbani.
Nikiwa chumbani nilisikia kama mlango mkubwa wa kutoka nje ukifunguliwa, sikio langu la kulia lilitega vyema tu maana baada ya mlango kufunguliwa nilisikia sauti zikija upande wa chumbani ila kwa nje. Lakini sikubahatika kusikia sauti zao vizuri, ilibidi nisogee hadi bafuni ili kupata kusikia vizuri nini ambacho walikuwa wakikiongea.
"Nilikuambia huyu Mama ni mchawi, ona kapona licha ya kusema umemwekea sumu" sauti hii ilikuwa ya Sofia na nilisikia vyema kabisa.
"Unajua siamini kama amepona, nilikuita hapa ili uje tusherekehe kwa pamoja msiba ila mh! Hapana aise" mume wangu naye alisema
"Kwahiyo sasa utafanyaje na mzigo umeshakuwa hapa kwako, yule atakula na kufanya kila kitu kama cha kwake hata ndugu zake ambao walimdharau huko kijijini kwao watakuja hapa kujifanya wanamuuguza"
"Na walivyokuwa na familia kubwa"
"Shaulako, mimi ndio nakuambia. Mwisho wakuroge wewe uwe chizi uokote makopo"
"Kwahiyo dada nifanyaje sasa?"
"Ufanyaje kuhusu nini? Muue tu, uwa tena mwekee hata chupa katika juice unadhani atachomoka. Au unataka kuwa masikini si ndio?" Sofia alisema huku akigandamiza na swali.
Nilishindwa hata kusikiliza maongezi yao na kujua kile ambacho kilikuwa kinaendelea. Nilijikuta nakuwa na hasira mno, mwili wangu ulitetemeka. Hakuna lingine ambalo nililipanga zaidi ya kutoka nje ili kwenda kuwaonesha........
Tupo kwenye dunia huru na salama zaidi. Raha ya kununua ipo pale ambapo muuzaji anakuambia, Lipia kwa pesa unayotaka. Leo, simulizi hii unaweza kununua kwa pesa yako mwenyewe. Nitext WhatsApp, namba ni 0717255498. Nunua kwa pesa yako..