TULIPOISHIA ILIKUWA HIVI
Mama mkwe amemtuma Daktari amchome mtoto wa Mayner (mkwewe) sindano yenye sumu ili mtoto huyo afe na iwe mwanzo wa mkwe wake huyo kufukuzwa nyumbani kwao..! Kwa bahati mbaya mtoto baada ya kuchomwa sindano, analia na Mayner anasikia sauti hiyo. Anaamka usingizini na kudai mwanae. Je, ilikuaje baada ya hapo? Karibu katika sehemu ya pili
Bahati ilikuwa kwake kwani Mayner hakufanikiwa kuiona sindano ile zaidi ilikuwa ni kutaka kujua mwanae anaendeleaje. Kama ilivyokuwa kwa mwanamke yoyote pindi mtoto wake anapokuja duniani huwa na furaha, ndivyo ilivyokuwa kwa Mayner ambaye alihitaji zaidi kuwa na mtoto wake.
Daktari alimchukua mtoto kisha akampeleka karibu na Mayner na kumweka kwa pembeni.
“Huyu hapa halafu kafanana na wewe” alisema huku akiweka tabasamu
“Ahsante sana, mwanangu unalia nini Mama” Mayner naye alimtazama mtoto wake ambaye aliendelea kulia si kikakwaida
“Kawaida ya watoto kulia hata usijali, si ndio mtoto wako wa kwanza au?”
“Ndio, ndio mwanangu wa kwanza hapa sitaki hata mtu mwingine amshike” alisema Mayner huku akimweka sawa mtoto wak “Mume wangu yupo wapi aone zawadi ambayo nimemletea?” aliuliza huku akimtazama zaidi mtoto wake.
Sura yake ilionesha kabisa kwamba alikuwa na tabasamu, dimpozi lake lilijitokeza vyema huku akimtazama mtoto wake ambaye taratibu sauti yake ilianza kupoza, ni wazi kuwa alihitaji kumbato la Mama yake.
“Siku moja utakaa hapa kisha kesho utaondoka. Mumeo yupo nje ngoja nikuweke sawa kisha atakuja kukuona” Daktari alisema kisha akaendelea na mambo mengine.
Ilikuwa ni asubuhi ya furaha kwa Mayner, ilikuwa ni saa nne ambayo dunia yote iliona tabasamu la mwanamke yule ambaye hakuacha kumtazama mtoto wake. Alimwangalia kila muda, kila sekunde huku akiwa na shauku ya kutaka kulipokea tabasamu la Garma kama Baba wa mtoto wake.
Aliimani kuwa hata mume wake atakapomuona basi kutakuwa na tabasamu ambalo atalipata. Alikumbuka jinsi ambavyo alisemwa na Mama mkwe wake kipindi wanatoka pale nyumbani “Eti mtoto lazima afe, mama ana roho mbaya yule. Na sitataka hata amshike mtoto wangu asije kumuua bure” alisema huku akifyonza na kumtazama mwanae.
Alikuwa ni pacha wake, walifanana kwa kila kitu. Sura nzuri, macho makubwa kiasi, kope ambazo zilikuwa zinashawishi kutazamwa pamoja na vidole venye kunyooka vyema. Kwakuwa alikuwa ni mtoto wa kike Mayner ndio alizidi kuwa na furaha mno.
“Mwanangu bora umekuja kunipa tabasamu, hata Baba yako akiondoka pale nyumbani nitabakia na wewe mama. Ninakupenda sana” alisema na kumtazama Daktari kisha alimuuliza
“Ulisema kwamba mume wangu anakuja saa ngapi?”
“Mh! Inaonekana una nguvu jamani hata unaongea hivyo”
“Nilikuwa mtu wa mazoezi sana, yeye alikuwa ananifanyisha mazoezi. Enh niambie ni saa ngapi anaruhusuiwa kuingia maana naona unanizungusha tu badala ya kujibu swali?”
“Sasa hivi tu, nilikuwa naweka mambo sawa” Daktari alisema na kuondoka huku akimtazama Mayner.
Ndani ya moyo wake kulikuwa na mishonyo zaidi ya 100 huku akilitengeza tabasamu feki ambalo lilikuwa katika uso wake.
“Ungejua ana siku mbili tu ili afe hata usingetabasamu lakini sawa tabasamu maana akifa si utalia bwana” Daktari alisema na kufungua mlango.
MAYNER RAMADHA alikuwa ni mtoto pekee wa familia iliyokuwa kaburini kwa hivi sasa, kwake alikosa utamu wa kufurahia Maisha akiwa kama mtoto ambaye ana wazazi kwani Baba na Mama walifariki miaka nane iliyopita wakati wakivuka ziwa viktoria. Kuzama kwa boti ama meli kulimsababishia Mayner kuwa mmoja wa watu ambao hawana ndugu Jijini mwanza.
Upande wa ndugu zake ulikuwa ukiishi Kigoma naye hakupenda kwenda huko licha ya kufariki kwa wazazi wake, aliamua kuyaanza Maisha ndani ya jiji la mihamba. Akapambana na kujijenga hatimaye katika pilika pilika akakutana na Garma ambaye alimuajiri katika kampuni yake ya ushonaji na utengenezaji wa viatu.
Yeye alikuwa kama afsa masoko katika kampuni huku mume wake akiwwa ni mkurugenzi, hawakubahatika kuingia katika ndoa lakini ahadi pekee ambayo iliwaongoza ni kwamba mara baada ya kujifungua basi ndoa ingefuatia.
Hivyo kujifungua kwake kuliambatana na furaha za aina mbili, furaha ya kwanza ni kupata mtoto wa kwanza katika Maisha yake na pili ilikuwa ni kwenda kukamilisha ahadi ambayo ilidumu kwa muda mrefu katka moyo wake.
Akiwa bado kitandani, mlango ulifunguliwa. Macho yake yalisafiri kwa kasi ili kuona ni nani ambaye alikuwa akiingia ndani, hakuwa mwingine bali ni Laila pamoja na Garma, alijikuta akiweka tabasamu kisha akasema.
“Mume wangu kaja wa kike”
“Woooooow! Woooooow! Hata sijui nisemaje lakini hii ndio zawadi yako” alisema Garma huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa pete.
Hakuna ambaye aliamini sio Laila wala Mayner, alijikuta wakiwa na mshangao mkubwa maana halikuwa ni jambo ambalo kila mmoja walilitegemea bali ni mshangao kwa maana ya surprise
“Nafanya hivi kwa ajili yako mke wangu, nilichobakiza ni ndoa tu. Shahidi pekee wa pete hii ya uchumba ni mtoto wetu. Huyu ndio anashuhudia namna gani nakupenda” alisema Garma huku akipokea mkono wa kushoto wa Mayner na kutenga kidole cha pili kutoka mwishoni.
Akamtazama Mayner ambaye alikuwa na tabasamu mno, uso wake ulianza kunawili. Maumivu ya kuleta kiumbe mpya yalipotea ghafla.
“Sijui hata nikupe nini zaidi ya mapenzi ya dhati lakini nayo pia naona haitoshi, sijui nikupe moyo wote ubakie nao kwako. Nashindwa kuelezea namna ya mwanaume gani ulivyo kwangu. Lakini acha niiambie dunia kwamba nakupenda, nakupenda na nakupenda tena” alisema Mayner huku machozi yakimdondoka.
Pete ilizama kidoleni huku Laila akichukua video ya tukio lile, lilikuwa ni tukio la ghafla ambalo liliambatana na fursa. Hakika Garma alidhamiria kabisa kuishi na Mayner licha ya mama yake kumchukia mrembo huyu.
Kama wapenzi walizungumza mambo mengi, wakajadili kwamba baada ya pale kituo kinachofuata ni suala la ndoa ambapo waliambiazana kwamba mwezi mmoja mbele yaani siku ya 40 ya mtoto ndio ndoa itafungwa.
Ilikuwa ni taarifa ya muhimu kwa Mayner, kwake muda wote alitokwa na machozi huku akimshukuru mume wake ambaye alimchukulia kama shujaa. Alimuona kama ni mtu ambaye amekuja duniani ili kuziba pengo la Mama na Baba yake.
Hakuacha pia kumshukuru Laila juu ya mchango ambao ameutoa kwake kama sehemu ya mtu wa karibu, alifurahia kuona amekuwa akimpa ushirikiano katika kila nyakati ngumu ambazo amekuwa akipitia katika Maisha yake.
Hatimaye masaa 24 yalipita na waliruhusiwa kutoka hospitali, hakuna ambaye alifahamu kama mtoto amedukwa sindano ambayo kwa mujibu wa Daktari alisema ina sumu laini. Sumu ambayo ingeanza kuondoa uhai wa mtoto taratibu mno.
Walipofika nyumbani walikutana na Mama Garma akiwa sebure anatazama runinga naye alipowaona aliweka tabasamu na kusimama akasema
“Naomba nikupokee mtoto”
“Ungemtaka mtoto ungekuja hospital” alizungumza kwa hasira mno huku akitetemeka mwili wake
“Garma unasikia dharau za unayemuita mke wako? Kwahiyo hakujua kama mimi nilikuwa naumwa?” Mama naye alikuja juu
“Kuumwa unaumwa nini? Umeshindwa hata kuja eti unasema kabisa kwamba mtoto atakufa? Aya nenda kaburini basi kachukue maiti yako uichekelee” Alisema Mayner huku akiacha na msonyo mkubwa
“Kwenda bwana, mtoto utapata wewe. Mtoto kaja mweusi kwanza sio damu ya mwanangu. Utatafuta Baba wa mtoto mbwa wewe” Mama Garma alisema kwa hasira huku akirudisha makalio yake katika sofa.
Ilikuwa ni kauli ambayo ilimuacha Laila hoi, alibaki ameduaa huku akiwatazama. Kile ambacho kiliongelewa kwa upande wake hakikuwa kizuri lakini aliamua kuyaona kama ya ngoswe tu.
Mayner aliingia ndani na kukaa kitandani huku akimtazama mwanae ambaye alikuwa amemlaza. Akarudisha macho kwa mume wake ambaye alikuwa amesimama karibu na mlango, akaweka tabasamu na kusema.
“Laila unaweza kutupisha kidogo?” Laila ambaye alikuwa kitandani hakuona kama alipaswa kuipinga kauli ile zaidi ni kukubali kuondoka, aliwapisha… ITAENDELEA
Hakikisha umenifollow ili upate muendelezo kwa wakati....