...Mimi na Riziki tukawa na wasiwasi sababu ule mtumbwi tunafahamu kwamba ulishapotea, na tupo kwenye mpango wa kulipa.! tukawa tunashangaa huu mtumbwi ulikuwa umepotea lakini inakuwa vipi leo tunaukuta hapa! kwakweli tulibaki tumeduwaa,mbaya zaidi ndio mtumbwi ambao tumeambiwa tuuchukuwe na kwenda nao baharini kwenda kuvua samaki.
Bwana mmoja ambaye tulikuwa nae alikuwa anaitwa Goma; na ndiye kiongozi wetu, yule bwana Goma akachukuwa ule mtumbwi ambao una tabia ya kupotea, kisha tukaisogeza mitumbwi kwa pamoja hadi kwenye maji kina cha usawa wa mapaja, kisha yule bwana Goma ambaye ni kiongozi wetu akaniambia nitapanda,nae kwenye ule mtumbwi wa kupotea, nikakataa lakini yule bwana Goma akasema kwakuwa mimi na Riziki sio wataalamu wa kuendesha mtumbwi kwahiyo ni lazima mtu mmoja asiyejuwa apande na mtu anayejuwa, ikawa hakuna namna, tukapanda kila mtumbwi wawili wawili tukaingia baharini kuvua samaki lakini mimi na Riziki ni mara yetu ya kwanza,
Tukaenda umbali mrefu kidogo, baada ya kuwa tumeenda umbali mrefu wale jamaa wakatupatia maelekezo kidogo namna kazi inavyotakiwa kwenda,kisha tukatoa nyavu lakini nyavu zao zilikuwa ni tofauti kidogo na nyavu za wavuvi wengine, tukatupia nyavu zetu ndani ya maji,tukaanza kuvua samaki, tumevua samaki,hadi mtumbwi mmoja ukawa umejaa ambao ni mtumbwi ule aliopanda Riziki na yule jamaa mmoja, kisha yule bwana Goma niliyenae kwenye mtumbwi wa kupotea alitoa kamba mfano wa nyavu kisha akafunga mtumbwi ambao yupo Riziki na jamaa mwingine, harafu akawaambia wao wabaki pale ili sisi tuanze kuivuta ile nyavu kwa kwenda mbele,
Tulianza kuivuta ile nyavu yenye mfano wa kamba huku tukisogeza mtumbwi wetu mbele,na mimi ndiye niliyekuwa naendesha,ingawa kwa kupewa maelekezo, lakini wakati tunazidi kwenda mbele ule mtumbwi ulianza kuongeza kasi bila kuendeshwa na mtu, hadi ile kamba ikakatika, yule bwana Goma akaniambia usiogope ni hali ya kawaida, ule mtumbwi ulizidisha kasi,ghafla mawimbi ya bahari yalianza kuwa makubwa kiasi kwamba maji yakaanza kuingia ndani ya mtumbwi wetu, nilianza kuogopa sababu mawimbi yalianza kuubeba mtumbwi wetu na kuupeleka juu,chini, wakati huo wale wenzetu tayari tumeshawaacha mbali na hawaonekani, ule mtumbwi ulizidisha kasi kuliko kawaida, lakini mimi kwa uoga nilitaka kujirusha ndani ya maji lakini yule bwana Goma akaniambia usijaribu kujirusha ndani ya maji shikilia wala usiachie,
Baada ya muda kidogo hali ya hewa ilianza kutulia, ule mtumbwi ulianza kupunguza mwendo na kuanza kwenda polepole hatimaye ule mtumbwi ukasimama kisha maji yakaanza kuingia ndani ya mtumbwi, lakini mimi naogopa sana sababu mambo yanayoendelea sio ya kawaida, yule bwana Goma akaniambia tulia hivyohivyo usifanye chochote, kweli nikatulia,ule mtumbwi ulianza kujaa maji taratibu hadi ukaanza kuzama, mtumbwi ulipoanza kuzama yule bwana Goma akaniambia endelea kutulia, tumetulia hatimaye na sisi tukaanza kuzama huku tumekaa ndani ya mtumbwi (maji yakafika mabegani) yule bwana Goma ananiambia nitulie (maji yakafika hadi shingoni) bwana Goma akawa yupo kimya, hatimaye maji yakafika hadi puani yule bwana Goma yupo kimya, nikajikuta nimeanza kukosa pumzi sababu maji tayari yanaelekea kufunika kichwa changu,
Nikaanza kukosa pumzi, hatimaye nikaanza kujihisi nipo kwenye mwanga mkali, Dah nikaona hapa nitakufa niliuachia ule mtumbwi na kutokezea juu kisha nikaanza kuogelea, baada ya muda kidogo yule bwana Goma na yeye alitokezea kwa juu akiwa na mtumbwi na kunishika kisha akanitupia kwenye mtumbwi na kuniambia umefanya nini,sasa nimekwambia utulie harafu wewe hujaelewa, nikamwambia niliona nakosa pumzi ndio maana nikashindwa kuvumilia, yule bwana Goma akaniambia twende turudi lakini usiseme chochote kwa hiki ulichokiona leo,
Kwakweli sikuelewa bwana Goma alikuwa na malengo gani, ikabidi tuanze kurudi kule walipo wenzetu, tulikuwa tumefika mbali lakini wakati wa kurudi tulitumia muda mchache sana tukawa tumefika pale tulipowaacha wenzetu, baada ya kukutana na wenzetu ikabidi tuanze kurudi pale tulipochukulia mitumbwi. lakini wakati wote nilikuwa nawaza kile kilichotokea hadi nashindwa kuelewa,
Tukarudisha ile mitumbwi tuliyochukuwa kisha wale walinzi tukawapatia na wao samaki, sisi tukaondoka na samaki waliobaki. Tukaenda kufanya maandalizi ya kuwauza wale samaki, tulipowauza wale samaki, ikabidi tulipe kule tunapodaiwa, yule bwana Goma aliamua kutoa na yeye pesa yake ya ziada kutulipia lile deni,
Yule bwana Goma alipotulipia lile deni la mtumbwi akatuambia kwamba kwakuwa yeye amejitolea kutusaidia hivyo tutaendelea kuvua samaki na tukiwa pamoja hadi pale atakapokuwa amerudisha pesa yake ambayo ametulipia kwenye mtumbwi, hatukuwa na namna ikabidi tukubali, lakini rafiki yangu Riziki sikumwambia chochote kuhusu kile kilichotokea baharini,
Mama alikuwa bado hajui kama mimi naenda baharini kuvua samaki, baadae nikakutana na Latifa, tukaongea mengi kama kawaida yetu, lakini Latifa alikuwa ananipenda sana. Ndio hivyo tena mapenzi yakaendelea. lakini mimi wakati huo nilikuwa bado nafikiria kuhusu kile kilichotokea baharini.
Baada ya siku kadhaa pale ambapo tulikuwa tunaenda kuchukuwa mitumbwi, pakaonekana kwamba kuna wavuvi wanafanya uvuvi haramu katika yale maeneo, ikabidi pafungwe kwa muda ili uchunguzi ufanyike kwa wanaofanya uvuvi haramu, lakini mimi na Riziki tuliposikia taarifa za uvuvi haramu tukaona huwenda wale jamaa zetu tunaoshirikiana kwenye uvuvi huwenda ndio wanaofanya uvuvi haramu, sababu tulikuwa tunaingia baharini,na muda mchache tu, tunatoka na samaki wa kutosha.
Baada ya muda yule bwana Goma alitutafuta na kutuambia kwamba wale jamaa zake wameshaacha kazi kwahiyo tumebaki watu watatu, mimi Saad; na rafiki yangu Riziki pamoja na yeye Goma, tukaungana watu watatu na kuanza kupanga mipango ya kazi. Goma akatuambia kwakuwa hatuna mtumbwi inabidi tuangalie sehemu ya kwenda kuchukuwa mtumbwi ili tupate kianzio, tukamuuliza ni mtumbwi wa kununua au"? akasema yeye ataangangalia na atatupatia maelekezo.
Wakati tunasubiri siku ya kuanza kazi. Mida ya Jioni mimi na Riziki tukiwa tunatembea maeneo ya ufukweni, tukawa tumemuona msichana mmoja mzuri akiwa amekaa peke yake juu ya mtumbwi,ambao umeegeshwa kando ya bahari, nikamwambia Riziki,wewe si huna mpenzi nenda kaongee na yule msichana huwenda akawa ni bahati yako...
Itaendelea...βπ»
~Daudi~.