"dadaaaa!! dadaaaa!!!" mtoto mdogo aitwae Livia alikimbia mbiombio kuelekea nyumbani akiwa ametokea sokoni, alipofika akaingia ndani na kumkuta dada yake yupo jikoni
"kulikoni Livia?" aliulizwa
"soma hapa!" alionyeshwa kikaratasi akakishika na kutazama akaona tangazo
"linahusu nini Livia?"
"aah dada huoni?"
"sijui kusoma mdogo wangu"
"ooh nimesahau dada ni hivi imeandikwa hapa kuwa kuna mashindano ya mpishi bora ambayo yatafanyika kesho na mshindi ataingia kwenye kasri la mfalme yaani atakuwa mjakazi ndani ya kasri la mfalme"
"kweli unayoyasoma ndiyo yaliyoandikwa Livia?!"
"ndiyo dada Maya sasa mimi nikudanganyaje jamani?"
"jamani lazima niende nika...."
"ukafanyaje??" walisikia sauti nyuma ikiuliza kabla hajamaliza sentensi yake, wote wakageuka na kutazama wakamwona shangazi Leti akiwa amesimama na uso wake wa ukali akiwaangalia, Maya na mdogo wake huyo mtoto wa shangazi huyo walitazamana huku Maya akiwa amekishikilia kikaratasi hicho mkononi amekificha kwa nyuma
"hapana mama ni kwamba nilikuwa namwambia dada Maya kuwa tutaenda tutaenda.." Livia alishikwa na kigugumizi akishindwa kuzungumza mbele ya mama yake huyo mkali
"wewe Livia toka nenda kacheze na wewe Maya nini hicho ulichokificha nyuma?"
"sijaficha kitu shangazi"
"kwahiyo mimi sina macho naongea uwongo siyo?"
"kweli shangazi sijaficha kitu" Maya alijibu huku akitikisa kichwa akikanusha katakata akimuhofia shangazi yake huyo mkali asiye na huruma, ambae alimfuata taratibu na kumsogelea kisha akanyoosha mkono wake akikiomba kitu ambacho Maya amekificha nyuma mikononi, na Maya hakuwa na namna akakitoa taratibu kijikaratasi hicho alicholetewa na mdogo wake, Livia, cha tangazo la mashindano ya mapishi
Maya msichana mrembo sana na mzuri alikuwa ni hodari wa mapishi mwenye kipaji cha pekee ambacho amekirithi kutoka kwa marehemu mama yake ambae alikuwa mpishi hodari sana
Shangazi Leti alikichukua na kukisoma akamtazama Maya kwa jicho kali kisha akakichana chana kijikaratasi hicho vipande vipande na kuvitupa chini
"unafikiri unaweza kupika vizuri mpaka uende huko unapotaka kwenda?"
"nataka kwenda kujaribu shangazi"
"kujaribu tu, unadhani nani atakayekupitisha wewe msichana masikini tena usiye na wazazi ambae hata mimi nilikuchukua tu ulivyokuwa mdogo kama msaada tu ili uishi namimi kwa sababu hata marehemu baba yako sina undugu nae wa karibu ni jamaa tu wa mbali mbali na nimekuleta tu ili ufanye kazi siyo uzubae zubae tu, wewe siyo mwanafamilia humu ni mjakazi tu hakikisha unapika chakula kizuri tunakula tunashiba maana ndo kinachokuweka hapa mjini sawa??!!"
"sawa shangazi"
"eeh ndo hivyo sahau kuhusu kitu kinachoitwa kuolewa au kwenda kwenye mashindano yoyote kwanza hata kusoma kwenyewe na kuandika hujui hapo ulipo unadhani nani atakaekukubali au ni mchumba gani atakayekuja kukuchumbia msichana mjinga mjinga kama wewe?" mwanamama Leti alimwambia Maya maneno ya kashfa, msichana huyo akabaki kimya hana cha kujibu mbele ya shangazi yake huyo, muda huohuo binti mkubwa wa mwanamama huyo aitwae Lidia alikuja jikoni na kumkuta mama yake anamsema Maya
"mama kuna wageni" alimwambia mama yake
"wageni gani?"
"sijajua ila wanaonekana ni watu wa maana sana"
"sawa twende" mwanamama huyo alimjibu bintiye na kutoka nae jikoni wakamwacha Maya peke yake, akashusha pumzi ndefu na kujikuna kichwani, akageuka na kuendelea na mapishi akiwaza mengi kichwani mwake
Maya alikuwa hana wazazi wote wawili wamefariki, alitangulia baba yake kisha akafuata mama yake na huku ndugu wakiwa hawampendi wa upande wa baba kwa sababu alihadithiwa kuwa mama yake ndiye aliyekuwa chanzo cha kifo cha baba yake, na Maya hakuwa mtoto wa kumzaa wa baba huyo alimkuta mama yake Maya tayari ana mtoto ambae ni maya alipomuoa, hivyo Maya akachukuliwa na mmoja wa ndugu hawa wa marehemu baba yake huyo (wa kambo) na kufanywa mfanyakazi wa ndani akitumikishwa kama punda kwa kila aina ya kazi kutwa nzima
"karibuni wageni" shangazi Leti aliwakaribisha ndani wanaume wanne, watatu watu wazima na mmoja ni kijana mtanashati, wakiwa wamekuja na gari (la farasi) usafiri mkuu ndani ya nchi hiyo ya karne ya kumi nane (A. D)
"asante sana" mzee mmoja aliyeonekana ni baba mzazi wa kijana huyo aliutikia wakaingia mpaka ndani na kuketi wakionekana wana jambo muhimu wamekuja nalo kwenye nyumba hiyo
"karibuni sana!" shangazi Leti alitabasamu
"asante sisi siyo wakaaji ndani ya nyumba hii tumekuja kwa sababu maalumu tunamuhitaji baba wa mji huu yupo?"
"amepumzika chumbani kwake ngoja nikamwamshe"
"kabla hujamwamsha tunahitaji kujua kwa msichana Ma..." mzee huyo alionekana kusahau jina alilotaka kulitaja
"Maya baba" kijana wake alimsaidia
"eeh Maya samahani limenitoka yupo?" aliwauliza, shangazi Leti na binti yake mkubwa Lidia wakageukiana na kutazamana, Lidia akamkonyeza mama yake
"mh hayupo tangu jana ameondoka" mama huyo alidanganya
"ooh basi sawa mguu huu tumekuja kwa ajili yake maana mtoto wangu amempenda anataka kumuoa" mzee huyo aliongea na kijana wake huyo akatikisa kichwa huku akitabasamu, kitendo hicho kilimuuma Lidia ambae aliumia kimoyo moyo alipoona Maya anakuja kuchumbiwa na kijana huyo mwenye maisha mazuri kwao wazazi wake wakiwa na gari na huku yeye akiwa bado yupo tu nyumbani, akamwacha mama yake anaendelea kuongea na wageni akaenda jikoni alipokuwa Maya anapika, akamkuta anakaangiza huku anaimba imba nyimbo za kujifariji
"wewe punda wewe?"
"abee!" Maya aligeuka kiunyonge akiitwa majina ya ajabu ajabu yote ni kumdhalilisha tu
"umefanya tukio gani huko mjini sijui sokoni ulipotoka?"
"kwanini dada?"
"askari wamekuja nyumbani wanakuulizia Maya!"
"askari??" Maya alishtuka mpaka akaangusha bakuli la mboga alilokuwa amelishika mkononi akitaka kutia mboga, hakuna kitu alichokuwa anakiogopa kwenye maisha yake kama askari, hata akikutana nao sokoni wakiwa wamebeba silaha zao huwakwepa na kuwakimbia
"ndiyo askari kwahiyo usitoke inawezekana kabisa kuna kitu umefanya au wamekufananisha hata kuongea usiongee sawa?!"
"sawa dada" Maya alimuitikia msichana huyo ambae wanalingana tu umri tena akimpita miezi kadhaa ila kwakuwa anaishi kwao nae ni mtumishi alikuwa anamuita dada na kingine ni kutokana tu na tabia njema aliyonayo Maya ya kumweshimu kila mtu
Lidia alirudi mpaka sebuleni alipokuwa mama yake na wageni
"vipi Lidia Maya yupo?"
"hayupo ametoka" Lidia alimjibu mama yake wakikonyezana
"ndiyo kama mlIvyosikia Maya hayupo ametoka halafu kingine hayupo tayari kuolewa kuna mtu anampenda na kuna binti yangu huyu mrembo anaitwa Lidia yeye hana mtu yupo tayari kuolewa" mwanamama Leti alitabasamu huku akimshika begani binti yake huyo...
*SEHEMU YA 02*
Ndani ya kasri la mfalme Bono, vijana wake watatu mapacha waliofanana, mwanamfalme Piso mkubwa, Teri anayefuata na Adrian wanaitika wito wa baba yao anaowaita kupitia mlinzi wake mkuu jenerali Fidel, wanasogea mbele ya kiti cha enzi cha baba yao na kuinamisha vichwa vyao (salamu ya heshima)
"uishi milele mtukufu mfalme" wanamsalimia wakimwita mfalme ingawa ni baba yao mzazi, mfalme alikohoa kidogo akapewa kitambaa na jenerali Fidel akajifuta kwa sababu anaumwa kwa muda mrefu huku umri wake ukiwa umeenda
"nimewaita hapa nataka jambo moja kwenu nataka kuwaona wakwe zangu, nataka muoe ili muwe na watoto mniletee wajukuu hapa niwabariki kabla sijaenda kwenye makaburi ya baba zangu, nilichelewa kuwazaa ninyi kwa sababu ya matatizo ya uzazi ya mama yenu lakini nakumbuka nina mtoto mahali ambae ni nje ya ninyi, katika kuhangaika kupata uzao nilibahatika kupata mwanamke nje nikampa ujauzito akajifungua mtoto wa kike lakini kwa bahati mbaya sikuwa mfalme wakati huo nilikuwa mwanajeshi tu wa kawaida ingawa nilikuwa ni mwanamfalme kama ninyi, nilijiunga na jeshi kisiri siri ili kuupigania na kuurudisha ufalme alionyang'angwa hayati baba yangu na jenerali wake, sikufanikiwa kumchukua yule mwanamke wala mtoto wangu kwa sababu ya harakati za vita ila ninajua ni wa kike, sikuwahi kuwaambia kitu kama hiki ila leo ndiyo ninawaambia ninyi ni wanaume tupu lakini kaeni mkijua mna dada yenu ingawa ni kwa mama mwingine..." mfalme Bono akakohoa kidogo kisha akaendelea
"ila hilo siyo jambo nililowaitia, nilichowaitia ni kimoja tu, nataka kuwaona wajukuu kabla sijaondoka kwenye uso wa dunia hii, Piso, Teri, Adrian mnanisikia?"
"ndiyo baba tunakusikia" walijibu kwa pamoja wakiwa wameinamisha vichwa vyao chini
"mnaweza kwenda" aliwaruhusu wakaondoka taratibu mbele ya baba yao kila mmoja
Piso alielekea moja kwa moja bustanini akaenda kukaa akiwaza na kuwazua kuhusu alichokiongea baba yake, Piso akiwa na mchumba tayari anayempenda sana anayeitwa Sethi ambae ni mtoto wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo mzee Gonde
Sethi mchumba na mpenzi wa Piso, alikuwa msichana mrembo sana ambae hakuwa tayari kuolewa na Piso kwa wakati huo na kwa sababu zake binafsi jambo ambalo lilimuumiza sana mwanamfalme ambae alihitaji kumuoa msichana huyo waliependana lakini Sethi alimtaka Piso asubiri kwanza
Teri kwa upande wake yeye hupenda sana kuogelea kila wakati, ana mchumba na mpenzi wake ambae ni bintimfalme kutoka nchi jirani lakini Teri hana mpango wa kuoa kwa sababu kwanza hana msichana mmoja ila anao kadhaa yupo anakula ujana kwanza
Upande wa Adrian yeye ndo kabisa hana mpango wa kuoa wala wa kuwa na msichana kabisa kwa wakati huu yeye muda wote ni mtu wa kufanya mazoezi tu ya kupigana kwa mwili na kwa silaha bado hafikirii kabisa kuwa na msichana
Adrian alikuwa na mpango wa kutoka kimya kimya kwa siri ndani ya kasri ili aende msituni akafanye mazoezi binafsi jambo ambalo lilikuwa marufuku kwa mwanamfalme kutoka ndani ya kasri bila ulinzi wowote wa askari, kijana huyo akaamua kuvaa nguo za kike kama mjakazi akajibadili na nywele zake na kujipodoa podoa akijifunika uso kidogo akatoka kimya kimya akipitia dirishani bila mtu kumuona akaenda mpaka kwenye geti kuu la kasri askari wakiwa wamesimama getini na silaha zao
"unakwenda wapi wewe msichana na kwa kibali cha nani?" aliulizwa
"naenda nje nimeagizwa na mwanamfalme Adrian kuna matunda ameniagiza" aliongea kwa kuigiza sauti ya kike tena ile ya kubembelezea
"lete kibali" aliombwa akatoa karatasi ya kibali yenye saini ya mwanamfalme Adrian, askari wakajiridhisha
"nitakusindikiza mimi mrembo"
"hapana nitakusindikiza mimi" askari walianza kubishana kuhusu nani atamsindikiza wote wakipagawa wakijua ni mtoto wa kike kumbe ni mwanamfalme
"mimi nataka unisindikize wewe hapo" alimshika askari mmoja kwa kidole kifuani
"teh teh si umeona mwenyewe mtoto mzuri amenichagua mimi hapa" askari huyo alimcheka mwenzake huyo, akapanda juu ya farasi, mwanamfalme Adrian (aliyejifanya mwanamke) nae akapanda kwa juu nyuma ya askari huyo wakatoka ndani ya kasri huku askari yule mwingine akiwa amechukia sana...
Farasi alitembea taratibu kuelekea nje ya kasri la mfalme, askari akiwa juu ya farasi huyo akicheka cheka huku akigeuka geuka nyuma akimtazama mwanadada huyo aliyedhani ni mjakazi wa ndani ya kasri
"kaka mbona unanitazama sana jamani?" alimwuliza kwa sauti ya kubana kama ya kike
"nimekupenda sana vipi kwani umeolewa au una mchumba?"
"hapana sina naomba simamisha farasi hapo nikojoe tafadhali mkojo umenibana"
"teh teh mrembo mbona unanipa majaribu mie jamani jamani sawa tu!" askari alitangulia kushuka juu ya farasi wakati wakiwa kwenye barabara yenye miti mirefu pembeni, lakini askari huyo aliposhuka tuu ya farasi alishangaa farasi anavutwa nira na kuanza kuuchapa mwendo yeye akiwa chini akaanza kumkimbiza farasi bila mafanikio yoyote
Mwanamfalme Adrian akiwa juu ya farasi huyo aliuchapa mwendo akipandisha njia ya milimani akielekea juu kabisa ili kwenda kutafuta eneo la siri ambalo atajifua vyema kimazoezi na kwa usiri mkubwa, akiwa na kitabu kidogo cha mafunzo ya mazoezi cha siri kutoka nchi ya KUSINI ambacho hakutaka mtu yeyote ajue kama ana kitabu hicho kwa sababu ya uhasama mkubwa walionao baina ya nchi yao na nchi hiyo ya KUSINI uliopelekea vita na kufungiana mipaka ya nchi
Mwanamfalme Adrian alifika mpaka mlimani porini mahali palipotulia asipoonekana mtu akashuka juu ya farasi, kukiwa ni nyika na vichaka kadhaa akashuka juu ya farasi na kutazama kulia na kushoto kisha akatoa kijitabu chake ili aanze mazoezi lakini kabla hajafany chochote
"wrrrrrruuuu!!" farasi aliyekuja nae alilia akiinua miguu ya mbele akageuka na kukimbia mbio mwenyewe
"wewe rudi hapa!" Adrian alimwita farasi huyo akijaribu kumfuata bila mafanikio
"gggggrrrrrh!" ndipo aliposikia muungurumo mzito wa sauti ya mnyama pembeni yake uliomfanya mpaka vinyweleo kwenye mwili wake vikamsimama, Adrian kwa hofu huku akitetemeka akageuza shingo na kutoa macho alipokutana na simba dume mwenye njaa akiwa anamtazama, kumbe ndiye aliyefanya farasi akimbie...
"oooh kaka samahani sana kumbe upo kwenye mawindo sikukuona samahani sana" Adrian alicheka cheka akimuongelesha simba huku akirudi kinyume nyume kwa magoti yakigongana na akihisi kubanwa na mkojo ghafla
"ggggrrrhh" simba aliunguruma kwa sauti ya chini akitembea kwa madaha akimfuata Adrian akiwa wala hana haraka
"teh teh kwanini hujamfuata farasi yule mkimbize tu ndugu yangu wala hajafika mbali na ana minofu kuliko hata mimi, tafadhali usinirarue rarue" Adrian alimuongelesha simba huyo ambae wala hakuwa na mdomo wa kujibu haraka akageuka na kuchomoka mbio, simba nae akaanza kumkimbiza kwa kasi isiyokuwa ya kawaida....
*SEHEMU YA 03*
Maya aliendelea kupika jikoni bila kujua nini kinachoendelea sebuleni maana Shangazi yake Leti na bintiye Lidia walifanya kila walichoweza kuhakikisha binti huyo hapati mchumba kama huyo ambae alikuwa kwao wana uwezo kiuchumi, hatimae wageni waliondoka wakiwa hawajamuona Maya wakiambiwa kuwa hayupo kumbe masikini binti wa watu alikuwepo jikoni ila ni hila tu za mtu na mama yake zimesababisha bahati hiyo ya mtende aliyoipata kupeperuka kama unyoya kwenye upepo
Baba wa nyumba hiyo ambae alikuwa amelala aliamka baada ya kusikia sauti sebuleni kama za wageni ndipo akatoka na kumkuta mkewe mwanamama Leti na binti yao Lidia wakiwa mlangoni na wageni wakiwa wanaondoka wanaishia ishia
"kuna nini?" aliuliza mzee Tando, akimwuliza mkewe
"kulikuwa na wageni tu wamekuja"
"mbona sikuamshwa?"
"niliona nitakusumbua mume wangu"
"wanahitaji nini?"
"walikuwa wamekuja kumuona Maya kijana wao anataka kumuoa ndo Maya amekataa katakata amesema hataki kuolewa na watu masikini kama wao" Lidia alijibu kabla mama yake hajajibu maana aliishiwa uwongo akawa anatafuta uwongo wa kudanganya ikabidi binti yake huyo amsaidie mbele ya baba yake huyo mwenye mengi kwelikweli
"kwahiyo Maya amegoma kuolewa kisa watu masikini haya sasa yeye huyo Maya ni tajiri, mbona yupoyupo tu humu ndani akifanya kazi za ndani, Mayaaaaaa!!" mzee huyo aliita kwa ukali
"abee mjomba" Maya aliitikia jikoni
"njoo hapa haraka mshenzi wewe"
"mume wangu taratibu usimuumize msichana huyo" shangazi Leti alijifanya kumuhurumia Maya ambae alikuja mbio mbio akiwa amelishikilia gauni lake refu na kuu kuu
"abee mjomba" alisimama mbele ya mzee huyo ambae alimtazama Maya tangu chini mpaka juu kisha akamtazama tangu juu mpaka chini kisha mzee huyo akasonya
"nionyeshe utajiri ulionao kiasi cha kukataa mchumba kisa masikini?" alimwuliza Maya akabaki anashangaa maana hajui kinachoendelea
"Baba kuna ni... "
"we Maya kelele acha kumjibu mjomba wako"
Shangazi Leti alimkemea Maya akimzuia kwa makusudi asijitetee, mjomba Tando akamtandika msichana huyo kofi zito la usoni kwenye shavu Maya akabaki amejishika shavu akiugulia maumivu asijue hata kosa alilolitenda masikini
"wewe wa kukataa wachumba kwa utajiri gani ulionao eti pumbavu nenda chumbani huko" Maya alifukuzwa akakimbia mbiombio mpaka chumbani kwake na kulala kitandani kifudi fudi akilia peke yake
"Maya!" shangazi yake alimfuata na kusimama mlangoni kwake
"abee shangazi" Maya akajifuta machozi haraka haraka na mafua ambayo hayakawii kumtoka kila anapolia kisha akasimama na kuinamisha uso wake akimsikiliza shangazi yake
"kaa tu" shangazi yake alimwambia akakaa kitandani
"abee shangazi"
"yule kijana aliyekuja leo unamfahamu?" Maya aliulizwa akasita kujibu kisha akaulizwa tena swali hilo hilo
"ndiyo shangazi ninamfahamu"
"anaishi wapi?"
"nakutanaga nae sokoni baba yake ni mmiliki wa maduka mengi pale sokoni"
"najua ndomana nimekuuliza maana nimeshangaa ujio wao hapa, wamefikaje fikaje?"
"sijui hata wamefikaje shangazi inawezekana amenifuata nyuma nyuma akapajua kwetu maana aliniambia amenipenda anataka anioe"
"kijana muhuni sana yule Maya hakufai usidanganywe na utajiri wake wewe jiulize kwanini awaache mabinti wote wenye uwezo wao aje akufuate wewe, anataka akuharibie maisha tu"
"sawa shangazi nimekusikia" Maya alitikisa kichwa
"haya nenda mtoni bondeni kachote maji hakuna maji humu ndani"
"sawa shangazi" Maya aliinuka kitandani na kutoka haraka haraka chumbani akiwa amelishikilia gauni lake refu linalofunika mpaka miguu lakini limechoka sana akiwa na magauni matatu tu ya kuvaa
"nyau mweusi wewe yaani uolewe na kijana wa kutoka familia yenye uwezo wa kifedha halafu binti yangu Lidia abaki nyumbani tu nani kasema, labda kama mimi siyo mama yake mssssyuuuu" shangazi Leti alisonya na kutoka taratibu na yeye chumbani mwa mwanadada huyo
Maya ambae kutwa nzima hana muda wa kupumzika hata kidogo alitoka ndani akiwa na mtungi wake wa asili wa kuchotea maji chombo maalumu chenye mkono kilichonakshiwa kwa urembo nje, kikubwa cha kujaa maji, akaondoka kwenda kuchota maji muda mfupi tu baada ya kutoka jikoni kuipikia familia hiyo nzima chakula...
Ndani ya kasri la mfalme mfalme Bono, muda wa chakula umefika, familia ya mfalme inakusanyika mezani, mfalme Bono mwenyewe na mkewe malkia Zilpa na watoto wao, na ndugu wachache wa karibu wa mfalme na malkia waishio ndani ya jumba hilo la mfalme, wajakazi wanahangaika kuandaa kila kitu mezani na chakula kizuri cha hadhi ya juu kinaandaliwa na kuanza kuliwa
"Adrian yupo wapi?" mfalme anauliza wote wanatazamana na kugundua kumbe mwanamfalme Adrian hayupo
"hajaonekana muda mrefu mtukufu mfalme" mjakazi mkuu alijibu
"kamuangalie chumbani kwake" malkia Zilpa alimuagiza mjakazi mkuu ambae kabla hajageuka kutoka mbele ya mfalme aliingia askari mbio mbio
"mtukufu mfalme, mtukufu malkia"
"kuna nini?" malkia Zilpa alimwuliza askari huyo
"mwanamfalme Adrian ametoroka hayupo ndani ya kasri..." aliwaambia wote wakageukiana na kutazamana mezani....
Upande mwingine mwanamfalme Adrian akiwa nyikani mlimani alikuwa anaendelea kumkimbia simba aliyekuwa anamfukuza nyuma akiwa na njaa kweli kweli, Adrian alilikunja mpaka kiunoni vazi lake refu la kike alilolivaa na kulitumia kutorokea ndani ya kasri akiwa hageuki nyuma anachanja mbuga huku akiwa peku peku, viatu vya kike alivyovivaa pia akiwa amevitupa akiona vizito na makucha ya simba yalikuwa yanakaribia kumshika miguuni, akaenda mpaka kwenye korongo akatazama chini na kuona mto mkubwa utwao Selebu akageuka nyuma na kumwona simba anakuja kwa kasi ya kimbunga, Adrian akaona kuliko araruriwe vipande vipande na simba huyo mwenye njaa kali ni bora hata ajitupe kwenye korongo hilo refu mto mkubwa ukipita chini, anaweza kufa au kupona, akajitupa mzima mzima na simba alipofika akafunga breki kali akitaka kuangukia korongoni akasimama na kutazama chini akakiona kitoweo chake kinaanguka chini korongoni,
"Grrrrrrh grrrh!!" simba alinguruma akisikitika kuukosa mlo wake huo wa mchana akageuka na kuondoka
Maya alifika kwenye mto huo mkubwa uitwao Selebu akiwa na mtungi wake mkubwa wa asili, akachuchumaa pembezoni mwa mto na kuanza kuchota maji taratibu huku akiimba imba nyimbo anazozipenda, alipomaliza kuchota akaubeba mtungi wake huo taratibu na kujiweka kichwani tayari kuondoka lakini kabla hajageuka akaona kitu kikitoka juu na kutumbukia kwenye maji pwaaaaaaa!! Maya akatoa macho kwa hofu akishtuka sana na ndipo alipogeuka kutaka kukimbia kwa bahati mbaya akajikwaa kwenye kisiki kilichojiotea chini, akapepesuka na kushindwa kuuzuia mtungi uliokuwa kichwani mwake ukamteleza na kuanguka chini puuh, ukapasuka vipande vipande maji yakimwagika yote, Maya akabaki amejiziba mdomo huku ametoa macho
"Nitamweleza nini mimi shangazi jamani uuuwiiii" alijishika kichwa akiwaza jinsi shangazi yake huyo atakachomfanya atakapomwambia kuwa ameuvunja mtungi huo wa maji....
Soma muendelezo kwa sh 1000
Whatsapp 0743433005.