UZI: Pichani ni Marijani Rajabu, akirekebisha mambo studio. Huyu ni mmoja wa wanamuziki mahiri nchini aliyezaliwa mtaa wa Somali, Kariakoo, jijini Dar mwaka 1954 na alilelewa kwa misingi ya dini ya Kiislamu.
Alipokuwa Tambaza Secondary school alikuwa akicheza mpira nafasi ya ugolikipa, na alikuwa anadaka sana. Lakini alipenda sana muziki, hasa wa Tabu Ley wa Kongo na Sorry Kandia wa Guinea.
Akaanza safari yake ya muziki akiwa na umri wa miaka 18 na STC Jazz Band, chini ya Raphael Sabuni, na kufanikiwa kurekodi nyimbo kadhaa nchini Kenya kupitia lebo ya Phillips.
Mwaka 1972, alijiunga na Safari Trippers, ambapo kipaji chake kilionekana zaidi, akiinyanyua bendi hiyo kuwa maarufu kwa vibao kama Rosa Nenda Shule, Georgina, na Mkuki Moyoni.
Hata hivyo, migogoro ya wanahisa iliizima Safari Trippers, na Marijani akajiunga na Dar International, ambako walipata umaarufu kupitia vibao kama "Mwana mpotevu au Mzee Saidi" "Zuena" , "Mwanameka" na vingine kibao.
Hata hivyo, changamoto za kifedha na ukosefu wa haki za wasanii ziliathiri kazi yao, nyimbo zao tisa zikiuzwa kwa Polygram bila ridhaa yao.
Baadaye, Marijani alishiriki Tanzania All Stars, kikundi kilichorekodi nyimbo za Kizalendo zenye ubora wa hali ya juu.
Alipitia bendi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Mwenge Jazz na Kurugenzi Jazz ya Arusha, kabla ya kuanzisha Africulture, ambayo ilikumbwa na changamoto za kifedha.
Kufikia 1992, hali yake ilikuwa duni, akiwa hapigi muziki na huku akiishi kwa kuuza kanda zake.
Jabali la Muziki liliaga dunia Machi 23, 1995 na kuzikwa kesho yake machi 24 katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam, akihitimisha tena utamaduni wetu wa wanamuziki kufa masikini..