Tanzania imepoteza kiongozi wa kipekee, nami nimempoteza rafiki mpendwa. Prof. Philemon Sarungi hakuwa tu daktari bingwa wa upasuaji na mzalendo wa dhati, bali pia mmoja wa wanachama waaminifu na wenye mapenzi makubwa kwa familia ya Simba SC.
Upendo wake na kujitoa kwenye klabu ya Simba vilidhihirika nilipopata heshima ya kumkabidhi Tuzo ya Maisha ya Simba—tuzo aliyostahili kwa mchango wake mkubwa na wa kudumu kwa klabu yetu.
Zaidi ya soka, Prof. Sarungi alikuwa nguzo muhimu katika sekta ya afya na utumishi wa umma nchini. Akiwa daktari bingwa wa upasuaji na mkufunzi mwenye weledi mkubwa, alileta mageuzi chanya katika huduma za afya Tanzania. Alitumika pia katika wizara mbalimbali, zikiwemo Afya, Elimu, Uchukuzi na Ulinzi, akitoa mchango wake wa thamani kwa taifa.
Pengo aliloacha ni kubwa, lakini urithi wake wa hekima na matendo mema utaendelea kuishi milele. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi .