Ijapokuwa huzuni kitakapopita kicheko, umasikini ukiweka kambi katika malango yako.
Ama pepo la utajiri likikupitia, iwe kwa ugumba ama kwa maradhi mshukuru yeye aliye juu.
Maana yeye, Anajua kwa nini anakupitisha katika hayo, hakuna jambo linalokuja kwa akili zako mwenyewe, usijikweze.
***
Katika moja ya baa maarufu yenye hadhi ya nyota tano “five star” iliyokuwa imejibebea jina katika jiji la Dar es salaam, ilijulikana kwa jina la crown hotel baa hii ilikuwa maarufu sana maana ilipendwa na watu wenye hadhi kubwa, watu walioshiba ukwasi wa fedha. Kwa wale walala njaa wasingaliweza kusogeza hata pua zao maana bei ya bidhaa zake ilikuwa kubwa sana, kama soda ya elfu moja mtaani ila katika baa hiyo siyo chini ya elfu tatu mpaka elfu nne. Katika moja ya meza iliyopatikana ndani ya baa hiyo alionekana mama mmoja mwenye miaka kati thelathini mpaka thelathini na maja, alionekana akitumia pombe kali huku akinuwia maneno na alionekana kuwa kunajambo ambalo limemtatiza sana. Kila alipomeza fundo moja la kinywaji hakuacha kusema neno moja tu, tena, kwa sauti ya kilevi.
“Hivi wewe mwanaume nini unanitenda, kama hunitaki si useme tu siyo kunisaliti, unaniacha nyumbani pekee yangu harafu wewe unaenda kwa hao, eti nyumba ndogo mh!, nimekuzalia watoto na mambo mengine ya nyumbani nakuhudumia vizuri, vizuri kabisa, ila wewe unanisaliti?"
Kila aliposema maneno hiyo alikunywa kinywaji kwa hasira sana huku machozi yakitoka na kupita katikati ya mfereji uliotenganisha pua yake na mashavu yake, kisha machozi yale yangeshuka mpaka kidevuni hatimaye yanadondoka chini.
Aliendelea kukaa eneo lile mpaka alipomaliza chupa nne na wahudumu kukataa kabisa kuendelea kumuhudumia maana ilikuwa imetahadharishwa kuwa kunywa taratibu ila yeye alifakamia kwa pupa na ghadhabu kumkomoa mmewe. Baada ya kuona hahudumiwi aliamua kurudi kwake huku akiwa amelewa tilalila, kila aliyemwona alimshangaa na kusema yake ila swali ambalo lilikuwa limechukua nafasi kubwa kwa kila aliyemwona ni moja tu,
“mh, ama kweli dunia Hadaa ulimwengu shujaa, Maskini mama Dorini, mbona siyo mlevi..kipi kimemsibu mpaka alewe kiasi hicho?”
Kila aliyemwona alikuwa akijiuliza swali hilo na kumuhuzunikia sana mama huyo ambaye tumefanikiwa kufahamu kuwa anaitwa mama Dorini. Kwa hiyo mama Dorini aliendelea kwenda nyumbani kwake huku akiongea mwenyewe maneno ambayo aghalabu husikika yakitamkwa na walevi huku akiwayawaya barabarani. Baada ya muda alifika nyumbani kwake na kupokelewa na ukimya mkubwa maana watoto wake walikuwa tayari wameshalala, alifungua mlango na kuingia mpaka ndani huku akiendelea kuongea mwenyewe. Alifunga mlango wa sebule kisha kwenda chumbani kwake akiamini atamkuta mumewe, ila ajabu hakumkuta.
Moyo wake ukasononeka kisha kuchukua simu yake na kumpigia mtu.. mara simu ikapokelewa, wakaanzisha mazungumuzo
“Hallo”
Alisema mama huyo huku akivua viatu vyake na kujitupa kitandani kama mzigo.
“Ndiyo bosi nakusikia”
Sauti kwenye simu ilisikika
“Upo wapi now”
“Nipo kwenye uchunguzi, ili kukuthibitishia ukweli kuhusu mumeo”
“Uchunguzi gani Toni?”
“Ninakutumia sasa hivi kwa WhatsApp”.
Baada ya kusema hayo simu ilikatwa, mara ujumbe ukaingia kwenye whatsapp yake naye haraka akaifungua.
Alichokiona kwenye simu yake msomaji hatokaa asahau mpaka kifo chake. Alishuhudia video iliyokuwa ikimuonyesha mumewe akiingia gesti na mwanamke mwingine, huku wakifurahishana kwa malavidavi na mabusu kedekede na huku mwanaume huyo akifululiza kumsifia mchepuko wake huyo eti ni mzuri kuliko mke wake.
Wahenga walisema “Mwana kulitafuta mwana kulipata”, mwanamke huyo alitamani kujua kuhusu mmewe sasa kajua presha juujuu, pombe zikamwisha huku akiendelea kuirudiarudia video ile maana hakuwa akiamini kama ni kweli mmewe anamsaliti, sasa leo kajua alichokuwa akikitafuta na kukihisi, hakutaka kuondoka eti kwenda kwenye fumanizi, aliamua kuzima simu yake akajibwaga kitandani pwaaa! na kulala kungoja kesho mmewe akija.
Asubuhi kweli mmewe alirudi kutoka kazini, alipofika hatua ya kwanza ilikuwa ni kusifia kuwa mkewe ni mzuri, alipoulizwa wapi alikuwa hakusita kusema kuwa alikuwa na kikao kazini mpaka asubuhi ndiyo maana hakurudi usiku ule, kwa jinsi alivyokuwa Serious mwanaume wawatu usingeliweza kumuhisi kuwa anadanganya. Mama huyo hakusita kuuliza kwa mara nyingine, akiulizwa mmewe ni wapi alikuwa usiku wa jana, ila majibu yalikuwa yaleyale eti alikuwa kazini kwenye kikao mpaka asubuhi, mama wawatu akasema usinitanie akawasha simu kisha kumuonyesha mumewe ile video yake iliyokuwa ikimuonyesha akiwa na mwanamke mwingine. Loooh!! kwanza mwanaume huyo alichoka kisha kuvua miwani yake na kumuangalia mkewe kwa mara nyingine na kumuuliza ni wapi hiyo video ameitoa.
Kwa hasira mama Dorini akafoka
"Hivi wewe mwanaume nini unakosa kwangu mpaka uniaibishe kiasi kikubwa hivi!!"
Baba Dorini alimwangalia mkewe kwa macho ya dharau sana na kwa kujiamini akamjibu akisema
"Shida yenu nyie wanawake mnajiona ninyi ndiyo ninyi mnapo wafumania waume zenu. Sikia mimi nilikuwa nabadili ladha tuu! aaagh.. ila si basi yemeisha..Sintorudia tena..Sawa mke wangu".
Mama Dorini alimwangalia mumewe na huku akiwa na kilio cha kwikwi akasema
"Mh! eti kubadili ladha, kama umenichoka bora uniambie tu niondoke kuliko kunidhalilisha hivi, mr Thomas mimi siwezi kudharaulika hivi nikafurahi eti ulikuwa unabadili ladha..narudia tena kama hunipendi bora uniambie niondoke kuliko kuzidi kunidhalilisha hivi".
Baba Dorini alishangaa na kuanza kucheka kwa dharau sana kisha akasema
"kwamba unadhani naogopa wewe kuondoka, ushanitibua mbwa wewe kama unaondoka nenda, namaanisha unatoka naleta chuma kipya kizuri zaidi yako"
mama Dorini aliangua kilio na kusema
"Sawa nitaondoka ila ipo siku utanikumbuka pasipo kuniona tena"
Baba Dorini akacheka kwa dharau na kusema
"una maajabu we mwanamke yaani unaondoka huku bado umekaa kwenye sofa langu nyanyuka ukachukue nguo zako usepee"
kwa hasira mwanamke huyo akanyanyuka alipokuwa amekaa na kwenda kuchukua nguo zake na kuondoka, watoto wake walimfuata na kumuomba asiondoke ila hakuwasikilizaka kabisa, badala yake alilia na kuwaambia wabaki salama wamuheshimu baba yao ipo siku wataonana kama Mungu akipenda, watoto hao baada ya kuona mama yao hawezi kuwasikiliza tena maana kashafukuzwa na baba yao waliamua kwenda kumsihi baba yao kuwa amrudishe mama yao ila baba yao badala ya kutekeleza ombi la watoto wake aliwafokea kwa hasira sana na kuwatimua wakajiandae waende shule.
SURA YA PILI.
Leo naomba nianze kwa kukuelezee kidogo kuhusu watoto hawa ili uwafahamu maana tayari umefanikiwa kumfahamu baba na mama ila watoto bado. Familia hii ilikuwa imefanikiwa kuwa na watoto wawili, moja anaitwa Dorini na mwingine anaitwa Frank.
Dorini ni mtoto wa kwanza mwenye umri wa miaka sita huku akifuatiwa na mdogo wake huyo anayeitwa Frank mwenye umri wa miaka miwili. Watoto hawa wamezoea sana kuishi maisha ya upendo kutoka kwa mama yao hivyo hawakuwahi kupata kabisa upendo kutoka kwa baba yao, hali iliyo wafanya kukosa furaha kabisa baada ya mama yao kuondoka.
Kesho yake baada ya Baba Dorini kupata uhakika kuwa mama Dorini harudi na ndiyo kaondoka moja kwa moja, alimleta mke mwingine na mwanamke huyu ndiye aliyesababisha ndoa hii kuvunjika maana alimganda baba Dorini kama ruba, akawa hataki kabisa kumuacha, hapa ndipo ule msemo usemao tukiachana asubuhi jioni natangaza ndoa unapochukua nafasi, yaani jana tu kaachana na mkewe ila leo kaoa mwanamke mwingine na kwa kufuru kamleta kwenye kitanda kilekile cha mkewe. Mwanamke huyu anaitwa Lissa mzaramo halisi namaanisha aliyezaliwa kijiji cha Chole kata ya Samvula katika wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani na kukulia hapohapo jijini Dar es Salaam. Basi kwa mara ya kwanza mwanamke huyu alianza kuonyesha upendo feki kwa watoto hawa baada ya baba Dorini kumtambulisha kuwa ndiye mama yao mpya. Watoto hawa hawakumkubali, katika mioyo yao bado walimkumbuka mama yao mzazi tu ila ndiyo hivyo tena hawana usemi juu ya kauli ya baba yao ikabidi wabaki kulia tu maana waliambiwa waziwazi kuwa mama yao hatorudi tena aslani!.
Maisha yakasonga watoto hawa wakamzoea mama yao mpya hii nikutokana na jinsi alivyo wateka kwa huo upendo wake bandia, kwa hakika alijifanya kuwapenda sana na kuwalea kama watoto wake wa kuwazaa, hii ni kawaida ya mama wa kambo wengi, mwanzo huwapenda watoto ili kuteka hisia zao kwa lengo la kumfanya baba wa watoto hao ampende zaidi, ila pindi anapo pata mtoto wa kumzaa yeye basi ule upendo huyeyuka kama barafu kwenye jua kali. Ndivyo ilivyo kuwa kwa Lissa, ile siku anatoka kujifungua mtoto wake hapo ndipo mateso ya watoto hawa yalipoanza, hakujali kuwa watoto hao bado ni wadogo, alianza kuwafanyisha kazi za shuruba bila ya huruma hata kidogo, ila ndiyo hivyo mtoto ni mtoto kila walipoteswa walipigwa na mkwara mzito eti wasimwambie baba yao akidai eti siku watakapo thubutu kumwambia ataua mmoja bada ya mwingine basi walikuwa wakiogopa sana.
Siku moja Lissa alimuita Dorini, baada ya Dorini kufika mama huyo akasema,
"Dorini hebu fua haya madaso ya mwanangu"
alisema hayo huku akimwangalia Dorini kwa macho ya dharau na nyodo sana.
"Mama bado sijajua kufua vizuri labda nijifunze"
alisema Dorini huku akimwangalia mama yake wa kambo kwa macho ya hofu maana alihofia kupigwa.
"Ama kweli mama yenu ni mjinga, ndiyo maana nilimkimbiza kwenye hii ndoa sababu hana hadhi ya kuishi na huyu mwanaume, alishidwa kuwalea, mimi nitawanyoosha vinyago nyie, tena hebu toka hapa kafue vidaso vya mwanangu, ole wako libaki linanuka kinyesi hapo ndipo utautambua upande wangu wa pili, pumbavu".
Alisema mama wa kambo Lissa huku akimuangalia Dorini kwa macho makali kidogo hali iliyomfanya Dorini kuwahi kufua kwa kuchelea kipigo. Wakati Dorini anafua alisikia huko ndani sauti ya Lissa ikimfokea mdogo wake, haraka aliwahi ili atazame nini anafanyiwa mdogo wake, alipofika alichokiona kilimfanya adondoshe machozi nguvu zikamwishia kabisa akajikuta akipiga magoti mwenyewe kwa kutetemeka maana anachokiona mbele yake kwa hakika ni ukatili mkubwa. Kama nilivyo kwambia mwanzo msomaji kuwa mdogo wake Dorini anaitwa Frank na ana umri wa miaka miwili au mitatu kasoro tu, hivyo kilichomfanya Dorini ajikute na simanzi kubwa ni baada ya kumshuhudia mdogo wake akipigishwa deki na mama huyo wa kambo, tena akifokewa kana kwamba anayefokewa ni kijana mvivu wa miaka ishirini au zaidi. Kwa hakika kazi ile kwa Frank haimstahili kabisa hivyo Dorini akaamua kuwahi kumsaidia kudeki, ila aliambulia kufukuzwa kwa matusi na viboko vya kutosha.
Basi Dorini huku akilia kimyakimya kwa kwikwi alirudi na kuendelea kufua madaso yaliyokuwa yamejaa kinyesi cha mtoto mchanga, kila alipo sikia sauti ya kuomboleza ya Frank alijikuta machozi yakimtoka zaidi huku akishidwa kujizuia kabisa na kuangua kilio kisicho cha kawaida, mara honi ya gari la baba yao ilisikika getini akihitaji afunguliwe geti. Hapo mama wa kambo akawahi na kumuasa Dorini aende akakae sebuleni huku akimtahadharisha kuwa asijaribu kusema kilichotokea na kumwambia kama akithubutu kumwambia atampiga viboko ambavyo hatosahau mpaka kifo chake, mtoto wa watu hana nyongeza akawa ameitikia kwa kichwa na kuwahi kumuangalia mdogo wake. Basi baba mwenye nyumba akawa amefika na kuwaonesha upendo ambao hakuwahi kuwaonesha tangu wamezaliwa, maana aliwaletea zawadi na kila mmoja kumkisi kwenye paji la uso, kisha akasema
"Enhee! Dorini mbona macho yenu ni mekundu hivyo kama mlikuwa mnalia nini kimetokea mwanangu?"
aliuliza hayo Baba Dorini huku akiwaangalia watoto wake ambao walikuwa kimya wakimwangalia mama yao wa kambo kwa hofu na mashaka, mara Lissa ambaye ndiye huyo mama yao wa kambo akadakia kusema,
"Dah! hawa watoto wako bwana walikuwa wanapigana nisingekuwa karibu ungekuta wametoana ngeu hapo".
Palepale baba Dorini akamkazia macho Dorini na kumuuliza kwa sauti kali
"Anachosema mama yako ni kweli na kama ni kweli utaniambia vizuri kwanini unampiga mdogo wako!?"
Dorini alibaki akimungalia mama yake wa kambo kwa hofu, maana hakuwaki kusema uongo toka amezaliwa maana mama yake mzazi amekuwa akimuasa kuwa aepuke uongo, sasa leo mama wa kambo anamuasa kuwa aseme uongo ili kujiokoa mwenyewe.
Dorini hakumjibu baba yake akabaki tu kumuangalia mama yake wa kambo huku nafsi mbili zikipingana ndani yake, moja ikimwambia aseme uongo ili asipigwe huku nyingine ikimwambia aseme ukweli kama mama yake mzazi alivyomfundisha.
Mara alishtushwa na sauti iliyojaa mamlaka kwa uzito wa besi yake, ikimuamuru aseme haraka kabla hajampiga, ilikuwa ni sauti ya baba yake, palepale alijikuta anasema yote kuanzia alivyoambiwa kwenda kufua madaso akaendelea kuelezea jinsi mdogo wake alivyo pigishwa deki bila huruma kabisa. Maelezo hayo yalimfanya Lissa amfuate Dorini na kumpiga kofi zito ambalo lilimzungusha mtoto huyo na kunguka chini kwenye sakafu hali iliyofanya Dorini damu kumtoka mdomoni baada ya fizi zake za meno kuchanika. Baba Dorini alichanganyikiwa na ghafla alijikuta akinyanyuka kwa hasira sana na kumshambulia Lissa kwa kipigo cha mbwa koko bila huruma mpaka alipoiona damu ya Lissa pia ikitoka mdomoni. Baba Dorini akamuangalia Lissa kwa hasira na kusema
“Alaaa, kumbe unanitesea watoto wangu bila ya kuwa na huruma hata kidogo!, wewe kweli ni mkono wa shetani maana binadamu wa kawaida hawezi kuwa katili kiasi hicho, tena nakuonya wewe mpuuzi ole wako urudie kunitesea wanangu”
Palepale Lissa alidakia kwa kusema kwa sauti iliyojaa hasira na yenye kilio cha kwikwi huku akimuangalia baba Dorini kwa hasira na kusema
“Unadhani hao watoto wako nitawatesa lini na wakati leoleo ninataka talaka niende kwetu, na kingine ni kwamba sihitaji kabisa kukuachia mtoto wangu hivyo ili nikamlee mwenyewe ninataka talaka tena siyo ya maandishi tu bali mali zako zote tunagawana pasu kwa pasu”
Kwa jazba na sauti ya kufoka baba Dorini akamjibu Lissa
“Ama kweli wewe ni mwanamke mpuuzi tena mjinga kabisa, yaani hizi mali nimesota kuzipata eti leo kilaini laini tugawane pasu kwa pasu kwa kisingizio cha kwenda kumlea huyo mtoto, we malaya kweli, nitamlea mtoto wangu mwenyewe sihitaji msaada wako nadhani umenielewa”
Kwanza Lissa akacheka kisha akamjibu baba Dorini kwa dharau huku akiwa amemshikia kiuno kwa mkono wake wa kushoto huku mkono mwingine ukifuta damu iliyokuwa ikizidi kumtoka mdomoni
“sikia wewe mwanaume kazi ya malaya ni kutafuta pesa kutoka kwa wanaume, sasa mimi sijaishia tu kukupatia burudani ili unilipe bali nimekufugia mpaka mtoto wako tumboni kwangu sijamuua ndani ya miezi tisa, unadhani hiyo kazi ni nyepesi eeh? ninataka tugawane hizi mali ili mimi nikajue huyu mtoto wako nitamleaje mpaka akue ili aje akusaidie ama hutaki nitaenda ustawi wa jamii na nikienda huko nitabadili maamuzi nitataka robo tatu ya mali zako”
Kwa sauti ndogo iliyojaa majuto baba Dorini akawa akijisemea
“ningejua, nisingemfukuza mke wangu maana yule kaniachia wanangu wawili wala hakutaka mali zozote ila huyu hata mwaka hatujaumaliza anadai mgao wa pasu kwa pasu kisa tuu kazaa na mimi daah! ningejuaa”
Lissa akamkejeli kwa kusema
“Unajuwa baba Dorini neno ningejua huja baada ya tukio baya kumkuta mtu na sikuzote ningejua ni neno la mkosaji kama wewe na wale wanaotanguliza tamaa mbele na kusahau majuto huja baadae, kiukweli yule mwanamke wako wa kwanza alikuwa akionekana kukujali na kilichokuwa kimemleta kwako ni ndoa na siyo mali, tofauti kabisa na mimi, maana mimi kilichonileta hapa ni mali na siyo ndoa..habari ndiyo hiyo!”
Baba Dorini alihisi kuchanganyikiwa baada ya kusikia maneno hayo kutoka kwa Lissa kuwa yeye hakuwa na mapenzi ya kweli bali alikuwa na haja na mali pekee, muda wote huo Dorini alikuwa amekaa akiangalia hiyo mizozo ya baba yake na huyo mke wake wa pili, huku moyoni akimuomba Mungu wake huyo mwanamke aondoke ili baba yao amrudishe nyumbani mama yao mzazi.
Follow page yangu Riwaya Tanzania
Leo tuishie hapo tukutane kesho asubuhi...
Lakini naomba kutambua walio soma wa like, maana mji like ndio napata moyo wa KUPOST simulizi kwa kasi mpaka mwisho..
Gosga like, kisha mshauri chochote Mr Thomas.
   
Hakuna ratiba iliyopangwa kwa sasa.