Riziki ni muoga sana akasema yeye hana mpango wa kuwa na mahusiano wala mwanamke, tukaanza kubishana pale mwisho nikaona ngoja nikajaribu mwenyewe, nikaenda hadi pale alipo yule msichana, nilifika na kumsalimia...Mambo " yeye poa" naona umetulia peke yako vipi kuna mtu unamsubiri" hapana nimekuja kuangalia mazingira ya huku ufukweni" inaonekana wewe ni mgeni wa maeneo haya" ndio lakini sio sana "
Nikaongea nae pale,na alionekana ni mwenye furaha, nikamtongoza kama utani nikamwambia japokuwa tumekutana kwa mara ya kwanza lakini mwenzio nimeshakupenda hivyo, alicheka na kuniambia kweli leo tu,umeshanipenda au umenitamani? nikamwambia yote sawa lakini ndio ukweli wangu,nikamuuliza jina lakini akaniambia tukionana wakati mwingine ataniambia na jina lake, ila mimi nikawa nimemtajia jina langu kwamba naitwa Saad; Kisha mimi nikamuacha pale yule msichana. nikamfuata Riziki tukaendelea na safari zetu,
Baada ya muda kukakutana na Goma kisha akatuambia tujiandae usiku kuna sehemu tunaenda kuchukuwa mtumbwi, ikabidi tujiandae mida ya usiku tukawa tumekutana na kuelekea kwenda kuchukuwa mtumbwi, lakini Goma akatupeleka kulekule kwenye ule mtumbwi wa maajabu, kisha akatuambia inabidi tuuchukuwe huu mtumbwi na tuondoke nao, sababu yale maeneo yalikuwa yamezuiliwa kwa muda hivyo hapakuwa na walinzi wa kutuzuia, tukauchukuwa ule mtumbwi na kuondoka nao, lakini mimi nilikuwa nahofu labda yanaweza yakatokea kama ya mwanzo sababu tulichukuwa ule mtumbwi wa maajabu, lakini mtumbwi tuliuendesha kawaida tu hadi kwenye maeneo yetu ya kufanyia kazi.
Tukawa tayari tuna mtumbwi na kazi ya uvuvi ikaanza, ule mtumbwi kwa macho ya kawaida ulikuwa ni mtumbwi wa kawaida sana, ule mtumbwi tulikuwa tunaingia nao baharini kisha tunaenda kwenye kina kirefu cha maji na tunavua samaki bila shida lakini tulikuwa tunavua samaki wengi hadi wanajaa kwenye ule mtumbwi na tunarudi bila shida, mimi na Riziki tukajikuta tayari tumeanza kunogewa na pesa za uvuvi, sababu tulikuwa tunavua samaki wengi na kuwauza kwa bei ya juu,
Lakini kule ambapo walikuwa wamefungiwa kufanya shughuri za uvuvi ikaonekana kwamba kuna mitumbwi imeibiwa ikabidi wale wenye mitumbwi waanze kufanya msako kila kambi ya wavuvi, walikuja hadi pale kwenye eneo letu lakini hawakuuona ule mtumbwi, na tulikuwa tumeuweka peupe wala hatukuuficha, waliangalia maeneo yale mwisho wakaamuwa kuondoka, walipoondoka Riziki akauliza kwahiyo hawa jamaa walikuwa hawauoni mtumbwi wakati tumeuweka peupe namna hii, mimi na Goma hatukumjibu chochote Riziki. sababu tunaelewa hekaheka za ule mtumbwi.
Mama akawa amepata taarifa kwamba mimi nimenza shughuri za uvuvi, mama alikuwa hataki mimi niwe mvuvi hivyo alinifokea sana, lakini nikamwambia mama mimi kwa sasa ni mkubwa na ninaelewa ni nini nafanya kwahiyo wewe kubali kwamba mimi kwa sasa tayari nimesha kuwa mvuvi, mama hakuwa na namna ya kunikataza sababu tayari nimeshaanza maisha yangu, ikabidi niendelee na kazi ya uvuvi, lakini wakati huo nilikuwa bado naishi pale nyumbani na mama.
Badae ikabidi tukutane kwa ajili ya kwenda kuvua, uvuvi wa usiku ulikuwa unaogopwa na wengi lakini sisi wakati wote tulikuwa tunaingia baharini kuvua samaki mida ya usiku, lakini wakati tunafanya maandalizi ya kuingia baharini yule jamaa ambaye ndio mmiliki halali wa ule mtumbwi akatukuta usiku ule na kutuambia, sitaki kesi wala maneno mengi,nimeijia mtumbwi wangu sababu nina uhakika nyie ndio mliuiba, mimi kwakuwa naelewa maajabu ya ule mtumbwi nikaanza kujiuliza au na huyu mwenye huu mtumbwi anaelewa kwamba huu mtumbwi sio wa kawaida, sababu wakati tunafanya kazi ya ulinzi mtumbwi ulipotea na baada ya kupotea tulimlipa mwenye mtumbwi lakini leo ametufuata eti anataka mtumbwi wake Mh. tulikuwa tayari tumeshaweka nyavu zetu ndani ya ule mtumbwi Goma akasema toeni kila kitu na mumpatie mtumbwi wake,
Kweli tukatoa kila kilichochetu tukampatia mtumbwi akaondoka nao, na ilikuwa ni mida ya usiku, sisi kwakuwa tumekosa mtumbwi ikabidi tuendelee na kazi zingine kwanza, Goma akasema tutapumzika siku tatu wakati yeye anafanya utaratibu wa kupata mtumbwi mwingine, lakini wakati huo mimi na Riziki tulikuwa tayari tunapata pesa nyingi tofauti na mwanzo ingawa bwana Goma alisema kwamba tutafanyae kazi hadi arudishe pesa yake lakini tukajikuta maisha yanakuwa mazuri na yule Goma alikuwa anatugawia pesa kila baada ya kuvua samaki na kuuza,
Siku tatu za mapumziko nikaanza kuzitumia nikiwa na Latifa, ikabidi niende kujitambulisha hadi kwao, wazazi wa Latifa hawakuwa na ubaya wakanikubali na kunikaribisha kama mchumba wa Latifa, lakini pia nikakaa na mama na kuongea nae nikamueleza kila kitu kuhusu mimi na Latifa, mama yeye alionekana kunipinga kidogo sababu alitaka mimi nioe mwanamke ambaye sio wa karibu na maeneo yetu, lakini nikamwambia mama Latifa hana shida. ila wakati huo nilikuwa bado namuwaza pia yule msichana mrembo ambaye nilikutana nae kule ufukweni mwa bahari,
Badae ikabidi nimtafute Goma ili nimuulize kama ameshapata mtumbwi mwingine, nikawa nimekutana na Goma nikamuuliza akasema kwamba hatuna sababu ya kutafuta mtumbwi mwingine ila ule mtumbwi utarudi wenyewe na tutaendelea na uvuvi, nikamuuliza sasa inakuwa vipi ule mtumbwi unapotea na kurudi, Goma akaanza kunisimulia machache kuhusu ule mtumbwi, akaniambia...ule mtumbwi una miaka mingi na watu wengi huwa wanautumia kwa ajili ya uvuvi, lakini pia ule mtumbwi umewapoteza watu wengi sana, ule mtumbwi umempoteza kaka yangu wakati huo mimi bado kijana wa makamo, ule mtumbwi inavyosemekana umewapoteza zaidi ya watu mia moja na hakuna aliyewahi kurudi, baada ya mimi kumpoteza kaka yangu nikaanza kufanya upelelezi kwa siri sana,na nikagundua watu wengi waliowahi kuutumia ule mtumbwi wote walipotea kwenye mazingira ya kutatanisha, na kitu pekee kinachosababisha watu wengi kupotea wakiwa na ule mtumbwi ni kwamba ule ni mtumbwi wa bahati ukiingia nao baharini huwezi ukakosa samaki, kingine ule mtumbwi huwa haujai hata kama mkiwa watu zaidi ya mia moja bado mtaenea, mimi nilifanya upelelezi wangu nikaenda hadi kwa wataalamu wa kienyeji wakanipatia mashariti ya kuuendesha ule mtumbwi, lakini siri ya ule mtumbwi ukijuwa namna ya kuuendesha kwa njia isiyokuwa ya kawaida basi lazima utakufa, sasa kwanini mimi niliweza kuuzamisha ndani ya maji nikiwa na wewe na bado naishi!? kwa leo tuishie hapa lakini nitakusimulia mengi sana ila usimwambie chochote rafiki yako wala mtu yeyote.
Nilianza kuogopa kuhusu matukio ya ule mtumbwi, lakini nikawa nawaza huwenda na baba yangu alipotea akiwa na ule mtumbwi. baada ya muda kidogo tukaachana na Goma na kuambiana tutaonana wakati wa kazi ukifika, mimi nikaona nijaribu kupita yale maeneo ambayo nilikutana na yule msichana, nilifika hadi pale kwenye yale maeneo lakini sikumkuta ikabidi nikae kidogo nione kama naweza nikamuona lakini baada ya muda kidogo nikamuona kwa mbali akiwa anakuja maeneo yale, (nikamsubiri hadi akafika)
Alipofika tukasalimiana akanitajia na jina lake kwamba anaitwa Salha; nikamuuliza kuhusu jibu langu, lakini kabla ya kunijibu akaniuliza umesema unanipenda je una malengo gani na mimi...
Itaendelea...✍🏻
~Daudi~.