Ingia

Sema Jambo

Unsplashb
750+ Trending Pictures | Download Free Images on gonga94
  never give up harmonize

Chozi la mdogo wangu SURA YA SABA

7th Aug, 2025 Views



zikupita siku nyingi Frank alipona na kurudi kwenye hali yake ya kwaida, siku hiyo ndiyo daktari huyo aliwapeleka kwake, wakati wapo kwenye gari daktari alizidi kuwadodosa kwa maana alihitaji kuwafahamu zaidi,
“Naitwa dokta Temba vipi huyo mdogo wako ulisema anaitwa nani vilee”
“Anaitwa Frank”
“Ohoo ana jina zuri sana”
“Eenhee Ndiyo maana nakapenda sana kadogo kangu”
“Mi pia nimefanikiwa kuoa juzi kati, bado sijapata mtoto kwa hiyo ninyi pia mtakuwa wanangu watakao zaliwa watakuwa wadogo zenu”
“Ooh jamani..yaani tunashukuru saana saana dokta”
“Wala msiwe na shida mtasoma mpaka mchoke wenyewe sitawahi kuwachukia kikubwa ni nyie muwe watoto wazuri msiwe wadokozi, sawa?”
“Usijali dokta hatutofanya hivyo”
“Ala! Usiniite dokta mimi baba yako sawa, emu niite baba”
“Baba”
Yalikuwa ni mazungumzo marefu sana yaliyojumuisha vicheko na furaha baina ya Dorini na dokta Temba.
Basi walifika nyumbani kwa dokta Temba na wakawa wameingia ndani baada ya kushuka katika gari na kuwatambulisha kwa mlinzi pale getini wakawa wameingia ndani.
Walipofika ndani walimkuta mke wa dokta Temba akiwa sebuleni kwenye sofa, Dorini alipomuona tu moyo wake ulibubujika furaha isiyo na kifani, huku macho yake marembo yakibubujika machozi ya furaha mithili ya chemchemi ya maji na kijasho chembamba kikawa kikimtoka, ni baada ya kumuona mama yake mbele ya macho yake yaani mke wa dokta Temba ndiye mama yao tena mama yao mzazi. Walitazamana sana kati ya mama huyo na Dorini huku Dorini akiendelea kujisogeza alipokuwa ameketi mama huyo ili amsalimie.
Basi Dorini alimfikia na kumsalimia ila mama huyo hakuonekana kumkumbuka kabisa. Kwanza msomaji mama huyu angemkumbukaje na wakati Dorini huyu wa leo siyo Dorini yule aliyemuacha kwa baba yake. Yule alikuwa mnene ila huyu kawa mwembamba kabaki mifupa tuu, yule alikuwa akinukia marashi ila huyu ananuka harufu ya dampo, yule alikuwa mweupe huyu kajaa masizi meusi kawa kama mkaa sasa anaweza kumkumbukaje kwa mfano. Dorini baada ya kuona mama yake hamkumbuki akawa amekaa kimya tu hakutaka amwambie mapema hivyo maana aliamini kuwa ipo saa atamkumbuka tu, basi mama huyo aliwakaribisha watoto hao akijikuta kawapenda isivyo kawaida. Basi baada ya Dorini na Frank kukaa chini mama huyo aliwaletea chakula wakawa wameanza kula. Wakati wanakula mama huyo akawataja kwa majina huku kila anapotamka jina alimnyoshea kidole mmiliki wa jina hilo,
“Unaitwa Dorini (akatikisa kichwa ishara ya kukubali) na wewe mwanangu wa kiume unaitwa Frank (kenyewe hakakujibu kalikuwa bize kula tu na kumpiga jicho la wizi kumlinganisha na mama yake).
Chakula kilikuwa kitamu maana chakula hicho alikuwa amekimisi si unajua huyu ni mtoto na alikizoea chakula kama hiki wakati anaishi na mama yake bwana.
Dorini akawahi kusema
“Mama usimuone huyu mdogo wangu hakujibu ukadhani ni dharau bali ni....”
Akakatishwa usemi na mama yake kwa kumalizia usemi huo
“Kwasababu ya njaa, najua huyu mtoto yupo bize kula maana kakimisi hiki chakula kutokana na mazoea ya chakula cha kutupwa dampo kilicho kichafu”
Dorini akadakia palepale na kusema
“Unaonekana mama unatufahamu”
Kabla mama huyo hajaongea mara dokta Temba akasema
“Nilimwambia hata kabla hamjaja so alijua ujio wenu ndiyo maana kawafahamu mapema”
Palepale Dorini akadakia
“Asante sana baba yani una karoho fulani hivi kazuuri”
Mama yule alimuangalia sana Dorini huku akimlinganisha na mtoto wake ila taswira ikawa inakuja na kupotea kisha akajisemea moyoni
“Mbona kama huyu ni mwanangu Dorini, hapana haiwezekani, maana mwanangu hawezi kuwa amechakaa hivi kwa muda mfupi ambao sipo nyumbani”
Wakati mama huyo anawaza hivyo kumbe na yeye Dorini alikuwa akiwaza na kujisemea moyoni
“Hapa dawa ni kutumia maneno ya zamani niliyokuwa nikipenda sana kuyatumia ili mama anikumbuke”
Ghafla bin vuu dokta Temba akawakurupusha kwenye mawazo yao na kusema
“Inabidi mkalale ili kesho niwapeleke kupima nguo za shule”
Dorini akadakia na kusema
“Dah! Wakati nikiwa na wazazi wangu mama alikuwa anapenda sana kunifundisha na alikuwa akiniasa nisome kwa bidii”
Mama huyo akaendelea kujiwazia na kujisemea moyoni mwake
“Ila ndiyo huyu huyu Dorini wangu maana yote yanaonekana waziwazi, ni mimi ndiyo nilikuwa nikimwasa mwanangu hayo sasa nasubiri uthibitisho wa mwisho maana nimemhisi kuanzia jina, sura mpaka maneno yake”.
Wakati uo huo na Dorini akawa akijisemea moyoni mwake
“mbona nilivyoanza kusema maneno ya zamani kawa kimya akionekana kuwaza sana au ameanza kunikumbuka, ngoja nidondoshe dongo la mwisho afu iwe la mwisho kwa leo, lazima atatukumbuka tu" alijisemea hayo Dorini.
Yaani mwenzako Dorini kaniaacha hoi kwa sababu ana akili mpaka zimepitiliza, yaani mtoto mdogo hivi anafanya maajabu makubwa kiasi hicho.
Dokta Temba akadakia akisema
“Hata huyu ni mama yenu kwa hiyo msiogope atakuwa akiwapeleka shule na atakuwa akiwashauri”
Dorini akasema huku akiwa na majonzi makubwa moyoni mwake
“Dah! kiukweli wewe ndiyo unastahili kuitwa baba mwema maana unajali, ila baba yangu wa kunizaa siyo baba mwema maana alimfukuza mama kwa sababu ya mwanamke mwingine eti anabadili ladha dah! Mama yetu mzazi akawa ameondoka”
Palepale mama yule akadakia kuuliza kwa mshangao
“Dorini!!, unaitwa Dorini nani?”
Kamoyo ka Dorini kakadunda pu! pu! pu! baada ya kuona mama yake anaelekea kuwakumbuka akasema
“Naitwa Dorini Thomas na mama yangu anaitwa Arisia Thomas tulipotezana siku nyingi sana baada ya baba kumsaliti mama”
Mara dokta Temba na mama huyo wakatazamana kisha dokta Temba akauliza
“Na mama yenu mnamchukia kwasababu aliwaacha au?”
Dorini akawahi kujibu
“Yeye hakututupa bali baba ndiye alimfukuza ila mama yeye anatupenda”
Mama huyo alihisi kupagawa huku akijiuliza imekuwaje watoto wake wachakae hivi na wakati baba yao alikuwa akijiweza kiuchumi na kifedha? Kwa hiyo akawa anajiuliza ni nini kimewasibu watoto hao.
Dokta Temba alitambua hilo mapema akawa amesema
“Mke wangu wewe kalale nitawaonyesha chumba chao mwenyewe, Dorini nifuateni huku”
Basi Dorini na mdogo wake waliongozana na baba huyo ili waende kuonyeshwa chumba chao watakachokuwa wakilala, wakati wanaenda Dorini aligeuka na kumpiga busu mama yake la hewani, (alibusu kiganja cha mkono wake wa kulia kisha kufanya kama anamtupia kitu) kitendo hicho kilizidi kumchanganya mama huyo maana busu la aina hiyo amekuwa akilipata kutoka kwa Dorini wake.
Kitendo hicho dokta Temba alikishuhudia kupitia kingo za miwani yake akatikisa kichwa chake kisha kuachia tabasamu.
Basi baada ya dokta Temba kuwapeleka wale watoto na kuwaonyesha chumba chao alirudi na kwenda chumbani kwake ambako huko alipigwa na butwaa kumkuta mkewe akilia sana, haraka akamkimbilia na kumshika begani kisha kusema,
“Mke wangu ni kweli na ninajua una maumivu mno, ila Mungu kakusaidia walau leo umewaona watoto wako”.
Palepale mwanamke yule alimgeukia dokta Temba na kusema
“Hao watoto nimewatoa kwenye hili tumbo langu, na nimewasikilizia uchungu mkubwa sana ila ona walivyo chakaa najiona mkosaji, sana”
Dokta Temba akazidi kumtia moyo
“Hawakuchukii mke wangu, maana hata wao wanajua kama baba yao ndiyo mwenye makosa”
“Nikwambie kitu baba, Huyu Dorini ni mwangu nimemzaa mwenyewe na akili zake nazijua vizuri tu, huyu mtoto ana akili kuliko binti wa miaka ishirini na tano, maana alianza kuongea vizuri tu hata kabla hajatimiza hata miezi nane, anauwezo wa kusovu jambo ukabaki unadhani ni mtu mzima mwenye umbo dogo”
“kwa nini useme hivyo mke wangu”
“Alipofika alinijua kwamba mimi ni mama yake, Kuna ishara aliifanya ambayo amekuwa akiifanya toka ana miaka mitatu ila mimi sikutilia maanani, pia akatambua kuwa mimi sijamkumbuka hakuwa na papala maana alijua kabisa ni kwa sababu ya jinsi alivyo konda ndiyo maana akawa anatumia visa vilivyopita ili nimkumbuke"
"Mimi mwenyewe nilipomuona hospitali nilidhani nitakapo muuliza miaka yake ataniambia ana miaka walau kumi au kumi na mbili kwa sababu alijieleza vizuri sana"
"Ndiyo hivyo..wale ni wanangu"
“Ndiyo hivyo ni wanao na mimi nitawalea kama wanangu, wahenga wanasema ukipenda boga penda na ua lake, ninakupenda wewe na wanao pia”
“Kwa hiyo unanipenda kiasi hicho?”
“Siyo kiasi hicho tu bali nakupenda sana kuliko vile wewe unawaza, wewe si unakumbuka nilivyokupata?”
“Hata sikumbuki, hebu nikumbushe kidogo”
“Kipindi hicho ulikuwa na mawazo mengi sana na makubwa ya kuachwa baada ya kutambua Thomas kaoa mke mwingine nami ndiyo nilikuhudumia pale hospitali mpaka ukapona hatimaye ukaniambia kama una watoto tulipoenda kuwaangalia watoto wako tukakuta walishauza nyumba tukawa hatujawaona na hali ile ilizidi kukusononesha, Ila leo Mungu kawaleta kwetu furahi sana mke wangu”
Walizungumuza mengi sana hatimaye mwanamke huyo akatulia tuli na furaha ikarejea tena baada ya kusikia kuwa dokta Temba atawalea watoto wake, wakawa wamelala kuingoja kesho ambayo ndiyo ndoto yao ifike.
Kama kawaida usiku hauwi mrefu sana kama ukipata usingizi mwanana na siyo ule wa mang’am ng’amu, uliojaa kushtuka shtuka. Hatimaye asubuhi ikawadia, kama walivyokuwa wamekubaliana usiku wa jana kuwa watoto hao wangepelekwa kununuliwa nguo za shule na matumizi yao mengine madogo madogo, basi walipelekwa na dokta Temba.
Mpaka wanatoka nyumbani akina Dorini hawakumtia machoni mama yao maana alikuwa akijiuliza ataanzia wapi kuwaomba msamaha au kuwambia kuwa yeye ndiyo mama yao huku wakiwa wamekonda hivyo, basi alijifungia bila ya kutoka nje kabisa ili asikutane na watoto wake mpaka waweze kupata nguo nzuri na sare za shule ndipo atajitambulisha kwao na hapo ndipo ataomba na pia kuwahoji watoto hao ili ajue nini kiliwasibu mpaka wachakae na kukonda kiasi kile, mpaka wafike kiwango cha kulala dampo na kufikia hatua ile iliyo muumiza zaidi ya wanawe kugombaniana chakula na inzi kule dampo na huku wazazi wao wote wawili wangali hai.
Basi dokta Temba aliwapeleka na wakawa wamepanda gari, baada ya kumsalimia mlinzi wake wa getini na kwa mara nyingine kuwatambulisha mabosi wapya wa kwenye hiyo nyumba, walipokuwa wakiondoka mlinzi akawa anafunga geti huku akijisemea mwenyewe kwa sauti ya chini,
“Yewegawee! sasa huvu vutoto ni vwa nani kati ya bosi na mke wake maana anavupenda na tangu nimefanya kazi na dogta Temba sijawahi kumuona na vudemudemu humu ndani, miaka ishirini anaishi singo kwenye huu mjumba mpaka anamuoa mwanamke huyu, ene way! Mi niko najali kazi yangu, maisha ya matajiri wangu nisitake kuyapeleleza”
Baada ya mlinzi huyo kujisemea hayo alichomoa sigareti yake aina ya gozo, akaiwasha na kuanza kuvuta huku akichungulia mlangoni mama mwenye nyumba asije mfuma na sigara maana amewahi kumzuia utumiaji wa hizo tumbaku kwenye nyumba yao.
Basi walitoka nyumbani wakaendelea na safari wakiwa kwenye gari maana kutoka alipokuwa akiishi dokta Temba mpaka Kariakoo sokoni kulikuwa na mwendo si haba na ukilinganisha na msongamano mkubwa wa magari dokta Temba akajikuta akiendesha gari polepole, ila ule upolepole wa gari lao uliwasaidia wao kuendelea kupiga soga.
Baada ya ukimya kidogo kupita dokta Temba alimuangalia sana Frank kisha akauliza,
“Hivi mbona Frank haongeagi? maana tangu nimemtia machoni sijawahi kusikia kinywa chake kikiongea au hajajua kuongea bado”
Dorini akadakia
“Anajua kuongea vizuri sana ila hata mimi sijajua kwa nini haongei akiwa mbele ya watu ila tukiwa wawili yaani mimi na yeye tunaongea vizuri tuu”
Dokta Temba akauliza tena
“Au kuna.….”
Mara alikatishwa baada ya Frank kuongea kwa hasira kidogo
“Dadaa ona baba si yule pale”.
Wote wakageuza vichwa vyao ili waone kama ni kweli ni baba yao, Alahaulaa, ni kweli kabisa alikuwa ni baba yao akinywa kahawa na wazee wengine huku wakiendelea kucheza bao la kete, palepale machozi yalimtoka Dorini huku akilalama kuwa baba yao ni katili.
Basi waliendelea kumuangalia baba yao huku dokta Temba akiwaangalia kwa huruma sana akawa amewauliza
“Nisimamishe gari?”
Palepale Frank akadakia haraka kusema
“Kwanini uchimamiche gari?”
Dokta Temba kwa mshangao kidogo huku akijiuliza kama huyo Frank ana miaka mitatu kweli au ana miaka mingi, maana alimshangaa Dorini ila sasa kwa akili aliyo nayo Frank akaona kumbe hii ni asili yao, ndipo hapo ikabidi amjibu Frank akasema
“Ili mumuone baba yenu na mumsalimie”
Frank akazidi kumshangaza dokta Temba akadakia juu kwa juu akasema
“Mimi siwezi kumchalimia mume wa chetani mamdogo, kwachababu walitufukuja kwetu na tukatecheka labuda da Dori amchalimie”.
Dorini naye akadakia huku akifuta machozi na kujijaza ujasiri
“Alichokisema Frank ni hichohicho siwezi kumsalimia mume wa shetani mamdogo, kwasababu walitufukuza kwetu na sisi tukateseka na isitoshe alimufukuza mama yetu kipenzi”.
Dokta Temba akashangaa kisha akasema
“Kwa hiyo hamumtaki baba yenu?”
Frank akadakia akisema
“Baba yetu ni wewe uliyemchukuwa mama yetu na kumtunja na chichi ukatuchukuwa kutulea”
Dorini alishtuka na kumuangalia mdogo wake kisha kwa udadisi akamuuliza
“Mama yetu umemuona wapi?”
Frank alijibu haraka
“Chi nimemuona tulipokuwa jana uchiku nyumbani kwa baba Temba”.
Dorini hakutaka mdogo wake aropoke mbele ya dokta Temba akawa amesema huku akichekacheka kuonyesha kuwa kapuuzia
“Msamehe bure mdogo wangu ni kwa sababu kapagawa na hizi shida na amemmisi mama yake ndiyo maana alipomuona mke wako akaona kama ni mama yetu msamehe bure”
Dokta Temba huku akimuangalia Dorini kwa macho ya wizi maana alikuwa akiendesha gari akasema,
“Dorini najua kabisa yule ni mama yenu na kama hukujua yule ni mama yenu kweli basi jua hivyo, kama anavyosema Frank maana jana mliyokuwa mnayasema yaliendana na aliyo yapitia mama yenu hivyo nikatambua kabisa yule ni mama yenu, ila msiogope nitawalea kama wanangu mtasoma mpaka mchoke wenyewe nitawapatia mitaji ili Frank asije shindwa kulea familia yake na wewe usijemtegemea mume wako kwa kila kitu”.
Dorini na Frank walilia sana huku wakimuangalia dokta Temba kisha Dorini akasema
“Kuna siku mama aliniambia eti licha ya uwepo wa watu wabaya pia kuna watu wema sana Mungu kawahifadhi ndani ya ulimwengu huu uliozungukwa na maovu mengi sana kila kingo. Akaniambia eti ninaweza kukataliwa na ndugu yangu wa damu ila nikakubaliwa na mtu baki ambaye hanijui wala hatuna undugu hata kidogo, ndiyo wewe, kipindi unatuchukua hukuwa ukijua kuwa sisi ni watoto wa mkeo ila sasa umejua na tena umekubali kutulea nakupenda sana kama wanao”.
Dokta temba akashika kichwa cha Dorini kwa mkono mmoja huku mkono mwingine ukiwa katika usukani wa gari ukiendelea na shughuli ya kuliongoza gari lake, kisha akasema
“Msijali, mama yenu hakukosea ni kweli kuna watu wabaya na kuna watu wazuri ila ninachowaomba msimchukie baba yenu hata kama aliwaacha mkateseka peke yenu”
Frank akadakia kusema
“Ila baba ni katiri sieti baba?”
Dokta Temba alimuangalia Frank kisha akasema
“Hapana baba yako siyo katili sema ana ujasiri wa kuwaacha mteseke ila msimchukie sawa”
Wote walitikisa vichwa vyao ishara ya kuwa wamekubali kutomchukia baba yao. Basi waliingia sokoni na wakapelekwa kwenye nguo, walichagua walivyo penda na pia wakapelekwa kwenye viatu wakachagua walivyopenda. Sasa baba yao aliwapeleka kwenye duka lingine lililopo mkabala tu na soko kuu la Kariakoo ili wachague mabegi na hasa Dorini achague vijibegi vya kike.
Walimaliza kuchagua na mara walipoenda kwenye malipo…katika hali ambayo hawakuitegemea kabisa wakamkuta mwenye hilo duka kumbe ni mama yao mdogo, namzungumzia yule bimdogo Lissa. Ni yule yule aliye mpigisha deki Frank wakati akiwa na miaka miwili, na walikwisha jenga chuki juu yake. Manunuzi yao ya mabegi yalikuwa yamegharimu kiasi cha shilingi laki moja na nusu na hawa wateja wake walionunua vitu hivyo ni wale wale aliokuwa akiwatesa na kuwanyanyasa miaka ya nyuma kidogo.
Dorini na Frank walimkazia macho mama huyo kisha Frank kwa haraka akawahi kujificha nyuma ya dokta Temba akionekana kumuogopa mama huyo, upande wa Dorini mabegi aliyokuwa ameshika yalimdondoka na kubaki ameduwaa akimuangalia mama huyo ambaye alipo watazama kwa umakini aliwakumbuka, kisha akamwangalia dokta Temba na kumuuliza
“Hawa watoto una undugu nao?”
Dokta Temba aliwaangalia wale watoto jinsi walivyo patwa na wasiwasi mara tu baada ya kumuona mama huyo, alishangaa ila hakutilia maanani akawa amemjibu mama huyo
“Hawa watoto nawapenda sana ni wanangu ijapokuwa siyo mbegu yangu”.
Mama yule akatikisa kichwa kisha akatoa tabasamu la tashwishi na kusema
“Hujanielewa dokta Temba nacho maanisha ni kwamba hawa watoto mna undugu?”
Palepale Dorini akadakia huku akiwa amemuangalia mama huyo kwa hasira yenye woga ndani yake
“kwa hiyo wewe ulidhani kwamba Mungu atatutupa mkono mpaka mwisho wa uhai wetu! ndiyo hivyo tena tumepata msaada. Akamgeukia dokta Temba ambaye kwa muda huo alikuwa akishangaa sana. Baba tuondoke, twende tukanunue nguo mahali pengine, hapa hapatufai kabisa naogopa kugeuka shetani kama mwanamke huyu”
Frank akadakia huku akiwa bado nyuma ya dokta Temba
“Dada sasa rudisha vitu vyake usije kugeuka kuwa shetani”
Dorini palepale aliirudisha ile mikoba na mabegi waliyokuwa wamesha chagua, yote hayo yalimshangaza sana dokta Temba, akabaki amepigwa na bumbuwazi kwa yale maamuzi ya ghafla yaliyofanywa na watoto hawa baada ya kumuona mwanamke huyo kisha dokta Temba akiwa bado katika hali ile ya bumbuwazi na butwaa akauliza
“Huyu aliwafanyaje? eti Frank”
Haraka haraka Frank akadakia kwa kusema
“Huyu ndiyo mamdogo aliye tufukuza kwetu tukiwa na baba hadi tukateseka”
Palepale dokta Temba akamuangalia mama huyo kisha akasema
“Lissa mdogo wangu kumbe wewe ni shetani kiasi hicho?”
Mama yule akadakia kwa kusema
“Mi sikuwafukuza kaka, wananisingizia tu, sasa mimi nimewafukuzaje”
dokta Temba akasema
“Sihitaji kukuamini wala sihitaji kumuamini mtu yeyote nitafanya uchunguzi, ole wako nikute ni kweli ulishiriki kuwatesa hawa watoto haki ya Mungu tutauvunja undugu”
Baada ya kusema hayo akawaomba wale watoto waondoke na hiyo mikoba wataifanyia maombi ili ule ushetani utoke, na ndiyo hivyo tena kwa kuwa watoto hawana makuu hawakukataa, wakakubali wakaichukua tena.
Wakati wapo njiani kurudi nyumbani Dorini alikuwa akiwaza jina alilolisikia akilitamka dokta Temba kumuita mwanamke yule aliye wahi kuwafanyia ukatili. Akamuuliza dokta Temba
“Baba nimesikia unamuita yule mwanamke dada, mna undugu?”
“Ndiyo, tena tumbo moja, baba mmoja na mama mmoja” Alijibu dokta Temba.
“Sasa mbona wewe siyo katili kama yeye? wewe una roho nzuri”
“Dah! Hata sijui, nashidwa kuelewa kawaje katili kiasi hicho hebu nihadithie ilikuwaje?”
“Baba alipomfukuza mama alimleta huyo mwanamke na yeye alitutesa sana, baadaye baba alituuliza baada ya kukuta mcho yetu ni mekundu sana ijapokuwa mamdogo alituonya eti tusiseme ukweli yaani tuseme uongo na sisi mama alitwambia tusiwe waongo tuseme ukweli. Basi tukasema tu ukweli kuwa mama mdogo anatutesa. Ndipo baba aliinuka na kumpiga mama mdogo, sisi tulikuwa tunafurahi sana, baadaye mama mdogo akaomba talaka basi baba akajikuta anaambiwa wagawane pasupasu yaani baba auze kila kilicho chake wagawane, basi waligawana na sisi na baba tukaenda kupanga. Baba alikuja kumkumbuka mama, alimtafuta akamkosa basi akawa mlevi wa kupindukia, hela zilipoisha akatutelekeza na kutuacha na sisi tukawa tumeenda kuishi kwenye dampo la kutupia taka zote za mji zikingoja kuoza ili zitumike kuwa mbolea, kilichonikuta hapo dampo kwa mara ya kwanza kabisa tunaanza kulala hapo sina hamu" (anaanza kulia na anazidi kumshangaza dokta Temba)
“Nini kilikukuta Dorini wangu mimi ndiyo baba yako wa sasa usiogope kuniambia”
“Nilipoteza usichana wangu nikiwa na miaka sita yaani nilibakwa na mtu mmoja anayeitwa Emma”
“Ulibakwa!!!!”
“Enhee baba nilibakwa na siku hiyo ilikuwa mbaya saaana mana usiku wa saa sita niliwaona wacha..”
Hata kabla hajamalizia kusema mara Frank alianza kulia na kulalama maumivu ya kichwa huku akisema eti Dorini hicho anachotaka kusema hakistaili, mara sauti ya yule mchawi kiongozi ilisikika ndani ya gari lote ikisema
“Wee mtoto, ukijichanganya kusema utajuta maana mdogo wako atakufa hapohapo kwasababu ya ulimi wako, ole wakooooo”.
Sauti hiyo aliisikia Dorini peke yake na aliweweseka kujaribu kuziba masikio yake huku akiangalia kulia na kushoto maana sauti hiyo ilikuwa ikiziumiza ngoma za masikio yake, baada ya sauti hiyo kutulia Dorini akawa ametulia akawahi kumuangali mdogo wake kama yupo sawa au amekufa, akakuta yupo sawa kabisa. Kitu hicho kilimshangaza sana dokta Temba maana alishangaa iweje kabla Dorini hajaongea neno fulani mara mdogo wake aanze kuumia kichwa na baada ya kuacha kusema neno hilo mara na Dorini mwenyewe akawa akiweweseka na kuziba masikio yake, haraka dokta Temba akasema
“Dorini, mbona unaweweseka?”
“kwani baba husikii sauti ya mtu kunionya”
“Sauti!”
“Eee sauti”
“Mbona mimi sijasikia sauti yoyoye we Frank umesikia (anatikisa kichwa kukataa)
“Kwahiyo nimesikia peke yangu?”
“Ilikuwa inasemaje?”
“Hamna litakuwa wenge tuu baba”
“Oke sawa, enhee hebu endelea na stori yako..ule usiku uliwaona wakina nani..?”
“Baba, bora nilione Chozi la Mdogo Wangu niumie ila nimuone mbele ya macho yangu sitaki mdogo wangu afe”
“Sasa habari za kufa umezitoa wapi? we nihadithie ulichokiona”
“Sasa baba si umeona nilivyokuwa naanza kusema jinsi mdogo wangu alivyoanza kuumia?”
“Eenhe, nimeona kwa hiyo kuumia kwake ni kwasababu ya wewe kutaka kusema ulichokiona”
“Eee, si unaona nilivyo ahirisha kusema yeye akawa poa nikafuata mimi kusikia masauti ya ajabu ajabu”
“Au uliona wachawi?”
“Nini!!”
“ Wachawi”
“Weee! jamani wewe ndiyo umesema mimi sijasema nilicho kiona, naogopa baba nisamehe mpaka kifo changu sitathubutu kukwambia nilichokiona usiku ule, siyo wewe tu mpaka mama yangu wala mtu yeyote. Jamani mmesikia mi sijasema chochote mdogo wangu mumuache salama”

Follow page yangu
Story Riwaya Tanzania.
   

X
SHARE TO SOCIAL MEDIA

Chozi la mdogo wangu SURA YA SABA   >>> https://gonga94.com/semajambo/chozi-la-mdogo-wangu-sura-ya-saba
#Nk #gonga94 #trending #instagood #explore #viral #challenge #simulizi #hadithi #israel #iran #war 

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on LinkedIn
Share on Pinterest
 

never give up harmonize
SIMULIZI NA SAUTI
gonga94ads - The Best Popunder Adnetwork
offa ya msimu wa nanenane
offa ya msimu wa nanenane

RATIBA YA SIMULI ZETU

Hakuna ratiba iliyopangwa kwa sasa.


Home Login Signup
Top 20 Popular Contact us
Terms & Conditions About us Latest