mtunzi: Frank Titus KAPINGA
SEHEMU YA 03
Sasa akiwa anaendelea na safari mara ghafla njiani alikutana na wahuni wawili wakiwa wanavuta bangi, mkononi walishika bisibisi. Anshera alishtuka, mapigo ya moyo wake yalianza kwenda kasi. Fasta aligeuka nyuma akitaka kurudi alikotoka lakini kwa bahati mbaya alikutana na wahuni wengine wawili wakiwa wamebeba visu mkononi. Anshera alitaka kupiga kelele lakini alitulizwa kwa kuwekewa kisu shingoni.
"Kimya! Kimya! Kimya! Kimyaaa! usipige kelele. Hii ni sauti ya mtoto wa ibilisi, imekuaje hadi uingie kwenye anga zetu? hutuogopi au sio?"
"No! please don't hurt me!! I will give you Dollars..."
"Ooh unajikuta muingereza au sio? Unatuletea usomi? unaleta dharau... Haya unaiona ile nyumba? ile ndiyo itakuwa nyumba yako kwa leo, wewe utakuwa mke wetu mchana huu na usiku mzima... Songa mbele fasta kabla sijakutoboa jicho" Muhuni mmoja alimsukuma Anshera kuelekea kwenye gofu la nyumba.
"Niacheni pleasee!!... Niacheni mnanipeleka wapiii?... "Anshera alipiga kelele akiomba aachwe lakini hakuachwa, alizibwa mdomo kisha alivutwa kuelekea ndani ya jumba bovu. Alitupwa kwenye chumba kisicho na mlango, dirisha wala godoro.
Vijana wote wanne walionekana kuwa na papara sana. Walivurugwa na uzuri wa Anshera. Siku zote walizoea kufanya vitendo vibaya kwa mabinti wa uswazi, lakini siku hiyo walibahatika kupata mtoto mkali kutoka U.S.A, hawakutaka kumuacha salama. Muhuni mmoja alishika suruali ya Anshera, mwingine alikamata shati, mwingine alibana miguu na mwingine alikamata mikono.
"Mnataka kunifanyaje?...... Wananibakaaaa!" Anshera alipaza sauti kwa nguvu akiwa anahangaika kujitoa mikononi kwa vibaka. Katika purukushani za hapa na pale mara shati lake lilichanwa, suruali yake ilivutwa kuelekea chini lakini aliizuia.
Vibaka walianza kugombana wenyewe kwa wenyewe, kila mmoja alitaka aanze yeye. Ilikuwa ni patashika nguo kuchanika, watu walitiana makonde, huyu akishika paja mwingine alishika kifua!! Huyu akishika tumbo mwingine alishika kiuno. Anshera alichanganyikiwa, hakujua atatoka vipi. Aliendelea kupiga kelele za kuomba msaada.
Wakati tukio hilo likiendelea mara ghafla kukasikika "Paaah! Peee!! puuh!!" Mawe mengi yalirushwa juu ya bati. Vibaka walishtuka, walitazamana wakiwa wanashangaa. Kabla hawajakaa sawa mmoja wao alipigwa jiwe la uso, mwingine jiwe la pua! Mara walisikia sauti ikisema "Shika hao vibakaaa.... polisiii kamataa haoooooo... piga bastolaaa". Wahuni baada ya kusikia kauli hiyo walikurupuka walitoka nduki wakidhani wamevamiwa na polisi.
Baada ya vibaka kukimbia Anshera alizungusha macho huku na huko akidhani atawaona polisi lakini hakuwaona, badala yake alimuona Antura akiwa ameshika mawe mkononi.
"Vipi dada upo salama? Hawajakudhuru? Si unaona sasa, nilikuambia husipite kwenye njia hii" Antura aliongea akiwa anatupa mawe pembeni. Pia aliokota begi, simu na pochi ya Anshera; alimkabidhi vitu vyake.
"Shika vitu vyako! Una bahati hawajakuibia"
"Hao polisi wako wapi?" Anshera alimuuliza Antura
"Hawakuwa polisi, ni mimi ndiye nilirusha mawe juu ya bati kisha nilipiga kelele kwa kuwaita polisi. Nilifanya hivyo makusudi ili wale vibaka wakuache." Antura alijibu
"Kwanini unalitaja bure jina la polisi? inaonekana hueshimu jeshi la polisi si ndio? kama kweli una nguvu za kuniokoa kwanini hukupigana na wale majambazi? au wale vibaka ni watu wako? Isije ikawa mmenichezea mchezo, haiwezekani vibaka wanne wakukimbie wewe mtu mmoja. Unajidai umenisaidia kumbe mlipanga iwe hivyo ili upate nafasi ya kuongea na mimi. Aisee na ndio maana sikutaka kuja bongo, nilijua tu nitakutana na uswahili huu. Wabongo mnawaza kubakana bakana tu!! Ulitaka wenzio wanivue nguo kisha wewe uje uone mwili wangu si ndio? Sasa subiri nikukomeshe, nawapigia simu polisi waje wakukamate wakulaze rokapu ili iwe funzo kwa vibaka wenzio"
"Dada mbona sikuelewi? Yaani mimi nakusaidia halafu unasema nakuzunguka? nikuzunguke ili iweje?"
Anshera hakujibu. Alivaa nguo zake vizuri, alibadili shati kisha alipiga namba za polisi wa Tanzania. Alitaja mahali alipo. Aliunganishwa na polisi waliopo karibu yake, alitoa maelezo yote kisha alisubiri.
Licha ya kuitiwa polisi lakini Antura hakuogopa wala hakwenda popote, hakuwa na wasiwasi wowote. Baada ya dakika chache polisi waliwasili eneo la tukio kwa kutumia maelekezo ya google map (Ramani) waliyotumiwa na Anshera.
"Dada habari yako, wewe ndiye ulitupigia simu?" Afande mmoja alimuuliza Anshera
"Ndiyo ni mimi, na huyu mtu ndiye aliyewatuma vibaka waniteke na kunileta kwenye jumba hili. Walitaka kunibaka"
"Okay, eti kijana ni kweli?" Afande alimuuliza Antura
"Hapana. Hivi laiti kama ningekuwa nahusika na tukio hilo; je ningeendelea kuwapo hapa?. Kama waliokimbia ni wenzangu, kwanini wao wakimbie halafu mimi nibaki?." Antura alihoji kitu ambacho hata polisi kiliwashangaza.
"Ndugu polisi huyu mtu hasiwachanganye, yeye amebaki hapa kwa sababu alisema haogopi polisi" Anshera aliendelea kukazia.
"Ati nini? Kijana huogopi jeshi la polisi?" Afande mmoja alimuuliza Antura akiwa amemkazia macho.
"Naheshimu sana chombo hicho. Ndugu polisi, huyu dada ni mgeni kwangu japo yeye mwenyewe anadai kwamba ni mwenyeji wa maeneo haya. Lakini kwa uelewa wangu sidhani kama huyu dada ni mwenyeji wa mtaa huu"
"Kwanini unasema hivyo?"
"Kwa sababu wenyeji wote wanafahamu kwamba uchochoro huu haupitiki. Kuna wavuta bangi, vibaka, mateja na wezi wengi sana. Mabinti wengi wamekuwa wakifanyiwa vitendo vibaya maeneo haya, watu wengi wamekabwa na kuibiwa sana katika uchochoro huu. Huyu dada nilimwambia hasipite njia hii lakini hakunielewa. Alipita alikutana na vibaka ambao walitaka kumfanyia kitendo kibaya ndipo nikaja kumsaidia. Sasa nashangaa ananibadilikia, anasema kwamba mimi ni mmoja wa wale vibaka" Antura alijaribu kujitetea. Polisi walielewa vizuri sana maelezo ya Antura lakini utata ulikuwa kwa Anshera ambaye hakutaka kuzidiwa kete na kijana huyo.
"Muongo huyu anawadanganya, hajaniokoa yeye. Yeye baada ya kunikuta kwenye hali mbaya ndipo alinichania shati langu akitaka kunibaka... Laiti kama mngechelewa mngekuta nishabakwa kitambo tu" Anshera alizidi kugongelea msumari. Polisi walishindwa kujua washike lipi waache lipi.
Hata hivyo siku zote kwenye mambo ya kutafuta haki Mwanamke huwa anapewa kipaumbele sana. Antura aliwekwa chini ya ulinzi, alifungwa pingu kisha yeye na Anshera wote walipelekwa kituo cha polisi. Walijaza maelezo kuhusu tukio lao kisha Antura aliwekwa rokapu.
Anshera aliruhusiwa kuondoka. Safari hii hakutaka kwenda mwenyewe, alimuita dereva boda kisha alimueleza ampeleke nyumbani kwa mzee Brogoz Matuka. Safari ilianza, baada ya dakika chache walifika mjengoni. Anshera alipokelewa na wazazi wake pamoja na majirani ambao walikimbizana kutoka huku na huko, kila mmoja alitaka kumuona msomi kutoka marekani.
"Eeh jamani mwanangu huyooo!! mbona umebadilika sana?... Umekuwa mzuri kama mzungu vile" Mama Anshera alifurahi mara baada ya kumuona mwanae. Alimkimbilia akitaka kumkumbatia lakini Anshera alisogea pembeni.
"Mama subiri kwanza, utanichafua. Halafu mbona wewe na baba mmechafuka sana? nguo zenu ni zile zile, nyumba ni ile ile, mmeshindwa hata kuikarabati kidogo? Kwahiyo mimi nitakuwa nalala kwenye nyumba hii?"
"Ndio mwanangu, sasa utalala wapi? ina maana hujui kuwa hapa ndo nyumbani kwako?"
"Hata kama ila pamezidi kuwa pabaya. Na nyie majirani mnashangaa shangaa nini? ila wabongo kwa ushamba tu, hawajambo!! Yaani mnashindwa kukaa majumbani kwenu eti mnakuja hapa kunitazama mimi, mtanilipa au? ebu ondokeni haraka. Kila mtu akacheze anakochezaga" Anshera alifukuza majirani wote. Majirani waliondoka kwa aibu na fedheha kubwa!!
Baada ya majirani kuondoka; Anshera alichukua mizigo yake kisha aliingia ndani, alizungusha macho huku na huko, alitafuta sehemu ya kukaa. Hakujua akae wapi kwa sababu makochi yalikuwa machafu, viti vibovu, kwa hasira aliamua kukaa sakafuni kisha aliwaita wazazi wake akitaka kuwauliza maswali magumu.
HUYO NDIYE ANSHERA, ANA BALAA HUYO...HUSIKOSE KUMFUATILIA UONE ALIYOYAFANYA
MTUNZI: FRANK TITUS KAPINGA
MAWASILIANO: 0743857349 (WHATSAPP TU).